MWILI
wa aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi
aliyefariki dunia Afrika Kusini, unatarajia kuwasili nchini leo.
Taarifa ya awali kutoka NCCR Mageuzi alikokuwa Mkurugenzi wa Sheria,
Katiba na Haki za Binadamu ilisema baada ya mwili huo kuwasili kwa ndege
ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini utapelekwa katika Hospitali ya
Jeshi ya Lugalo.
Kesho
kutakuwa na ibada ya kumuaga itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph na kisha kuagwa kwenye Viwanja vya Karimjee.
Baada
ya Karimjee, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi ambako
utalala na Jumapili itafanyika ibada nyumbani kabla ya kusafirishwa
kwenda Kisangara Juu, Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa maziko Jumatatu.
Shein
amlilia Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein
amempelekea salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Jaji Joseph Warioba kutokana na kifo cha Dk Mvungi.
Katika
salamu hizo, Dk Shein alieleza kusikitishwa na kifo hicho
alichokielezea kuwa pigo kwa maendeleo ya Taifa na msiba wa Watanzania
wote.
Dk
Shein alimwelezea marehemu Mvungi kuwa mzalendo mwenye upendo mkubwa
kwa nchi yake na mtaalamu wa sheria aliyebobea, mwanasiasa shupavu na
makini. Aliongeza kuwa binafsi, wananchi na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) wamehuzunishwa na kifo hicho.
Watuhumiwa
bado Wakati huo huo, hatma ya watuhumiwa wa uvamizi wa Dk Mvungi ambao
wanashikiliwa bado haijajulikana. Dk Mvungi alifariki dunia juzi alasiri
katika Hospitali ya Milpark jijini Johannesburg Afrika Kusini alikokuwa
akipatiwa matibabu baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, usiku wa
Novemba 2. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova alisema jana kuwa:
“Nitafanya
mkutano na waandishi wa habari ili kuzungumzia suala hilo ili umma
uweze kujua ni watuhumiwa wangapi kwa ujumla na lini watafikishwa
mahakamani.”
Hata
hivyo, akizungumza na waandishi wa habari, Kova alisema hadi juzi
watuhumiwa 10 walikuwa wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Alisema Polisi inaendelea na msako dhidi ya wahusika wote ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment