KILA mwaka, madini aina ya Tanzanite
huiingizia Tanzania kiasi cha dola milioni 20 (zaidi ya Sh bilioni 30).
Duniani kote, madini hayo hayo huingiza wastani wa dola milioni 500
(zaidi ya Sh bilioni 800).
Wakati mabilioni yote hayo yakiingia
mfukoni mwa serikali na wafanyabiashara, mgunduzi wa madini hayo,
Jumanne Mhero Ngoma (74), anaishi kwa kutegemea ruzuku za watoto. Mapato
yake kwa mwaka ni shilingi za Tanzania sifuri!(P.T)
Nilikutana na Mzee Ngoma siku chache
zilizopita jijini Dar es Salaam katika ofisi ya mmoja wa wanawe. Pamoja
na masahibu na mikasa mbalimbali iliyomkumba katika maisha yake, bado
aliweza kunipokea kwa bashasha na tabasamu.
Amefanya mahojiano na vyombo
mbalimbali vya habari na pengine ameanza kuchoka sasa. Mvi kichwani
kwake na kwenye eneo la ndevu ni ishara kwamba umri unaanza kumtupa Mzee
Ngoma.
Nimekaa namtazama. Huyu ndiye mtu
aliyegundua madini ya Tanzanite. Alipaswa kuwa utambulisho wa
Watanzania. Katika nchi nyingine zinazothamini watu wake, huyu alitakiwa
kufahamika na watu wote waliomaliza elimu ya msingi.
Kama ambavyo watoto wote wa Kimarekani
wanavyomfahamu Thomas Edison (mbunifu mashuhuri na mfanyabiashara wa
karne kadhaa zilizopita) . Lakini mbele ya macho yangu, alikaa mzee
mmoja ambaye kama ningekutana naye kwenye daladala (na ndiyo usafiri
wake mkuu), nisingemtazama mara mbili.
Namuuliza swali moja la msingi kwamba
ilikuwaje yeye aliyagundua madini ambayo wakoloni (wazungu) walishindwa
kuyabaini kwa muda wote waliokaa hapa nchini.
"Nakumbuka kila kitu kuhusu mara yangu
ya kwanza kuona madini hayo. Mara ya kwanza kuyagundua madini haya
nilikuwa mdogo sana. Nilikuwa na umri wa chini ya miaka 20 na nilikuwa
porini nikichunga mifugo.
"Nilikuwa kwenye msitu ambao Wamasai
walikuwa wameupa jina la Lalouo. Eneo ambako niliyaona lilikuwa
linafahamika kwa jina la Naisunyai ambako kwa kawaida Wamasai walikuwa
wakilitumia kunywesha mifugo yao.
"Siku hiyo niliona vitu vinavyowaka.
Nikawa nashangaa vitakuwa ni vitu gani. Awali nilidhani pengine ni nyoka
au wanyama wa hatari. Nikasogea nikiwa na upinde na mshale wangu tayari
kwa lolote.
"Nilipogusa na mti niliokuwa
nimeushika, nikashangaa mawe yanayong'aa yakitoka ardhini. Vipande
vidogo vidogo vyenye rangi ya bluu. Kwa kweli nilivipenda sana.
"Nilishangaa sana lakini ghafla
nikakumbuka kuwa nilikuwa nachunga mifugo. Kumbe ng'ombe na mbuzi
niliokuwa nawachunga walikuwa wamekimbia tayari. Nikaacha shughuli hiyo
na kwenda kuwafuata.
"Kwa bahati nzuri, nilifuatilia njia
walizopita hadi nikawapata wote. Lakini ilikuwa kazi ngumu maana ule
ulikuwa msitu mkubwa. Nikarudi nyumbani nikiwa na mifugo ile na nikawa
nimesahau kabisa habari za madini yale kwa muda ule," anasema.
Mtoto wa Ngoma aitwaye Asha aliyekuwa
mwenyeji wetu kwenye ofisi ile ananiuliza kama naweza kutumia kinywaji
chochote. Namwomba samahani kwa kuwatia hasara maana nikaagiza vinywaji
viwili badala ya kimoja. Maji na soda. Kwenye dunia hii ya kisukari,
kunywa soda pekee bila kuchanganya na maji kunaleta hatari ya kuongeza
sukari mwilini.
Mzee Ngoma yeye anaomba maji tu. Tunasubiri kidogo. Tunapiga mafunda mawili matatu na kisha tunaendelea na mazungumzo yetu.
Hata hivyo, mwaka 1966 ilitokea bahati
iliyobadilisha maisha yangu. Mwanzoni mwa mwaka huo, serikali
ilitangaza kuwepo kwa mafunzo kuhusu utafiti wa madini yaliyopangwa
kufanyika mkoani Morogoro.
"Mimi wakati huo nilikuwa nafanya
biashara zangu tu lakini nilikuwa mpenzi sana wa masuala ya madini na
ndiyo nilipoyaona madini yale ya Tanzanite kwa mara ya kwanza nilishikwa
na hamu ya kutaka kuyajua.
"Ulitakiwa kujilipia mwenyewe nauli na
gharama nyingine halafu serikali inakulipia mafunzo hayo kwa muda wa
wiki tatu. Nikazungumza na mke wangu kuhusu hilo na akaniruhusu niende
kwenye mafunzo.
"Nilikwenda Morogoro na hatimaye
nikafaulu kwenye mafunzo hayo. Ilipofika tarehe sita, mwezi wa sita
mwaka 1966, nikapewa cheti cha utafiti ambacho ninacho hadi leo. Pamoja
na mambo mengine, cheti hicho kilikuwa kinakuwezesha kufahamu madini na
sifa zake mbalimbali," anasema.
Ni mafunzo hayo ambayo baada ya kuyamaliza yalimfanya Ngoma aweze kugundua madini hayo ya Tanzanite.
Lakini kabla ya madini hayo, mzee huyu
kwanza aligundua madini aina ya Gypsum ambayo sasa yanatumika katika
nyumba nyingi za Watanzania wenye kipato kuanzia cha kati hadi cha juu.
Aliyagundua madini hayo katika eneo la Chankoko, Makanya mkoani Kilimanjaro.
"Wakati nikigundua madini hayo,
hayakuwa na kazi sana. Watu wengi hawakujua kazi yake. Kwa bahati nzuri,
katika wakati huohuo, kukawa na kiwanda cha saruji cha WAZO ambacho
kilitaka kuanza kufanya shughuli zake na gypsum ilikuwa ni malighafi
nzuri sana.
"Kuna bwana mmoja aitwaye Petro Gerson
Kizigha akanikutanisha na wazungu waliokuwa wakitaka kuanzisha kampuni
hiyo na tayari wakiwa na taarifa za gypsum niliyoigundua.
"Nakumbuka majina ya wazungu hao
yalikuwa ni Florench, Carter na Habel. Walikuja hadi Makanya kwa ndege
binafsi na walishukia katika shamba la katani la bwana mmoja aliyekuwa
akiitwa Hassan.
"Walipoona gypsum ile wakaipenda sana.
Wakaagiza mara moja mzigo wa tani 36 ambao tuliupakia kwenye mabehewa.
Kuna barabara kutoka Chankoko hadi stesheni ya reli ya Makanya yenye
urefu wa kilomita 10 ilijengwa ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa
hiyo.
"Mimi ndiye niliyepewa jukumu la
ujenzi wa barabara hiyo. Nilipewa na wazungu wale kiasi cha Sh 8,000 kwa
ajili hiyo. Kwa wakati huo, hiyo ni hela nyingi sana. Wajenzi walikuwa
wakilipwa shilingi nne kwa siku na zilikuwa nyingi kiasi kwamba watu
walikuja kuomba kazi kwa wingi hadi wengine nikawakataa, anasema.
Pamoja na mafanikio hayo katika
biashara ya gypsum, kuna kitu kimoja kilikuwa kinamsumbua Ngoma kichwani
kwake. Yale madini aliyoyaacha kule Umasaini, Marerani yalikuwa ni
madini gani?
"Ndipo siku moja nikawachukua ndugu
zangu na kuwaomba wanisindikize kwenda kwenye ule msitu wa Lalouo ili
nikayachunguze tena yale madini. Niliomba kusindikizwa kwa sababu ule
msitu ni mkubwa na nilitaka pia nipate watu wa kunisaidia kubeba.
"Nakumbuka tulichimba karibu kilo sita
za madini hayo. Kuna jiwe moja lilikuwa na ukubwa wa takribani gramu 55
hivi. Jiwe kubwa tu. Ndilo lililokuwa kubwa zaidi.
"Nikalipeleka Moshi kwenye Ofisi ya
Mkaguzi wa Madini aliyekuwa akiitwa Bills wakati huo. Mzungu huyo.
Akayatazama na akasema hajawahi kuona kitu kama kile. Akahisi yanaweza
kuwa Blue Tomaline, lakini tukakubaliana kuwa si yenyewe.
"Mimi nikamuuliza sasa mwenzangu
unadhani haya ni madini gani? Unajua wazungu ni watu wakweli kidogo.
Wana matatizo yao lakini hawapendi kusema uongo. Akasema kwa kweli
siyajui. Inabidi tuyapeleke kwenye maabara ya serikali iliyokuwa iko
Dodoma.
"Nikampa sampo yote niliyokuwa nayo
lakini lile jiwe kubwa zaidi nikabaki nalo. Alipoliona, mke wa bwana
Bills akawa amelipenda sana. Akaniomba abaki nalo.
"Nikakataa. Nikamwambia kama nikikupa,
nitakuwa nakupa nini? Maana mumeo ambaye ndiye mtaalamu wa mambo haya
ameshindwa kuyajua. Siwezi kukupa na nitabaki na hili kama kumbukumbu
yangu.
"Ilipofika Septemba 23 mwaka 1967,
ndipo nikapokea barua rasmi kutoka maabara ya Dodoma. Vipimo vikaonyesha
madini yale yanafahamika kwa jina la Zoisite. Ndiyo maana tunasema
madini hayo yaligunduliwa rasmi mwaka huo wa 1967 kwa sababu ndipo cheti
kile cha maabara kilipotoka," anasema.
Katika simulizi kuhusu gunduzi
mbalimbali za madini hapa nchini, zipo zinazoeleza namna wananchi wa
Shinyanga walivyokuwa wakicheza bao kwa kutumia almasi kwa sababu
hawakujua thamani yake.
Hali iko hivyo kwa Mzee Ngoma ambaye
alikuwa akilitumia jiwe hilo la gramu 55 kwa ajili ya kuzuia karatasi
zake zisipepee kutoka mezani kwake. Lilikuwa jiwe la kawaida kabisa
ndani ya nyumba yake.
Nimeangalia bei ya sasa ya Tanzanite
ili upate picha ya nini mzee huyu alikuwa nacho ndani kwake. Kwa sasa,
bei ya madini hayo katika soko la dunia inacheza kati ya dola 500 hadi
700 kwa karati moja.
Zipo taarifa kwamba zipo sehemu
duniani ambako watu wanauziwa hadi dola 1000 kwa karati moja. Tuseme
wastani ni dola 600 (sh 800,000) kwa karati moja.
Karati moja ni sawa na gramu 0.2.
Gramu 55 maana yake ni karati 275. Kama bei ya karati moja ni Sh
800,000, bei ya karati 275 ni sawa na takribani Sh milioni 220.
Mzee Ngoma alikuwa anatumia Sh milioni
220 kuzuia karatasi na magazeti yasipeperuke kutoka mezani kwake ! Mzee
huyu hakujua kitu wakati huo.
Jiwe hilo kipenzi la mgunduzi huyu
likaja kumpotea katika mazingira ya kutatanisha. Simulizi yake,
ilinifanya niombe mahojiano haya yapumzike kidogo ili niweze kuvuta
pumzi.
"Nilikuwa na marafiki wawili wenye
asili ya kihindi waliokuwa wakiishi Handeni mkoani Tanga. Mmoja akiitwa
Habib Esack Ismail na mwingine akijulikana kwa jina la Nuru Skanda.
Walikuja siku moja nyumbani kwangu na wakaliona lile jiwe.
"Wakaniomba waende nalo kwao (Handeni)
ili wakawaonyeshe wazazi wao wajue la kufanya. Wakati huo, Zoisite ama
Tanzanite kama inavyofahamika sasa, haikuwa maarufu sana na matumizi
yake hayakuwa yakijulikana.
"Walisema watalirudisha baada ya siku
tatu. Nikawapa na wakaondoka nalo. Hawakurudi baada ya siku tatu na
sijawaona tena tangu wakati huo. Siku moja nilikutana na aliyekuja kuwa
Kamishina wa Madini hapa nchini aliyejulikana kwa jina la Luwena na
akaniambia lile jiwe liko Ujerumani na waliuziwa kwa Sh 6000 kwenye
miaka hiyo.
"Hizo ni hela nyingi sana. Ina maana
akina Habib waliliuza na wakaondoka zao. Lile jiwe linaniuma sana maana
kama ningebaki nalo pengine lingeweza kunipa fedha nyingi," anasema
Ngoma.
Machungu ya Mzee huyu hayakuishia hapo. Kuna unyama mwingine mkubwa zaidi ambao alifanyiwa.
Baada ya kuibiwa jiwe lake hilo, akili
ya Ngoma ilifanya kazi haraka na akaamua kwenda kupata leseni ya
umiliki wa eneo ambako aliyapata madini yale.
Akapewa viwanja nane kwenye eneo lile
la Lalouo ambako alilipia kiasi cha Sh 15 kwa kila kimoja. Akaweka alama
zote muhimu na kuamini kwamba lile ni eneo lake halali kisheria na mara
wakati utakapofika, ataanza kuchimba madini hayo.
"Siku moja mwezi Februari mwaka 1968,
nikaenda kutembelea kwenye eneo lile. Nikamkuta kijana mmoja anaitwa
Daudi Mayaya akiwa anachimba madini hayo kwenye eneo langu. Alikuwa
ameyajaza kwenye ndoo.
"Nikamwambia kwanini amechimba madini
hayo kwenye eneo langu? Akanijibu kwamba lile si eneo langu bali ni la
mtu mmoja aiwaye De Souza (Huyu nitamweleza zaidi baadaye).
Nikamwonyesha alama zangu zote nilizoweka pamoja na nyaraka nilizokuwa
nazo.
"Nilipoenda kushitaki Polisi kuhusu
huyu mtu anayeitwa De Souza, nikaambiwa ataitwa na atafika Jumatatu.
Bila ya taarifa, kumbe huyo bwana akaja Jumamosi na akazungumza na
polisi mapema.
"Mkuu wa Polisi kwenye eneo letu
alikuwa akifahamika kwa jina la Herbert Kitenge. Huyu bwana akaniita
Polisi na akaniambia ameamua kumpa De Souza vitalu (viwanja) vinne kati
ya nane nilivyokuwa navimiliki.
"Sasa mimi nikabaki nimeshangaa,
inakuaje mtu anapewa vitalu vyangu. Lakini afande Kitenge akasema ama
nikubali hiyo dili au nitanyang'anywa vyote. Nikakasirika sana na
nikasusa kabisa. Sikurudi tena kule kwenye machimbo. Nikaenda kufanya
biashara zangu," anasema kwa huzuni.
Mzee Ngoma anamtaja De Souza mara
nyingi katika maelezo yake. Manuel De Souza, mzaliwa wa Goa nchini India
alikuja nchini Tanganyika mnamo mwaka 1933 akiwa na umri wa miaka 20 tu
na tayari akiwa fundi cherehani mzuri.
Taarifa katika mitandao mbalimbali
duniani inamtaja yeye kama mvumbuzi wa Tanzanite. Mtandao wa Ilios
Jewellers unadai kwamba Julai mwaka 1967, kundi la Wamasai, lilimpeleka
Mhindi huyo kwenye eneo ambako aligundua madini hayo.
Kwenye mtandao unaoheshimika zaidi
duniani wa Wikipedia unamtaja fundi cherehani, Emmanuel Merishiek Mollel
kama mgunduzi wa madini hayo. Katika maelezo yake, mtandao huo unadai
kwamba ni Mollel ndiye aliyempa De Souza madini hayo na yeye akayapeleka
kwa wataalamu ambao waliyabaini kwamba ni Tanzanite.
Hata historia inapindishwa ili Mzee Ngoma akose hadhi na heshima anayostahili !
Kabla ya kuitwa Tanzanite, madini haya
yalikuwa yakifahamika kwa jina la Zoisite. Jina hilo, kwa mujibu wa
maelezo ya nyaraka mbalimbali, lilitokana na raia wa Austria, Siegmund
Zois, ambaye alikuwa akifadhili safari mbalimbali za watu waliokuwa
wakitafuta madini mbalimbali.
Kwa Kijerumani, neno Zoisite
linafanana kimatamshi na neno la Kiingereza Suicide. Kampuni iliyokuwa
ikifanya biashara ya Tanzanite ya Tiffany& Co. ndiyo ikaamua
kubadili jina hilo na kuyaita madini hayo Tanzanite ili liwe na mvuto.
Hakukuwa hata na mmoja aliyeona yanafaa kuitwa Ngomanite au Ngomasite !
Mwaka 1984, serikali iliamka kutoka
usingizini na kumtaja Mzee Ngoma kama mvumbuzi wa madini hayo. Kama
zawadi yake kwa uvumbuzi huo wa kihistoria, serikali ilimpa mzee huyo
Ngao, cheti cha kumtangaza kama mvumbuzi na fedha taslim Sh elfu 50,000.
Kwa mujibu wa Wikipedia, katika
kipindi cha kati ya mwaka 1967 hadi mwaka 1972 wakati serikali ilipoamua
kutaifisha shughuli za uchimbaji wa Tanzanite, kiasi cha karati milioni
mbili zilikuwa tayari zimechimbwa kutoka Mirerani.
Kwa bei ya sasa ya karati moja, maana
yake ni kwamba kwa miaka hiyo mitano pekee, De Souza, washirika wake
kama vile Ally Juyawandu na askari jeshi mmoja aliyekuwa na asili ya
Ugiriki aliyefahamika kwa jina moja tu la Papanichalou, walifanikisha
biashara yenye thamani ya takribani Sh trilioni 1.6 kwa thamani ya sasa !
Watoto wa De Souza aliyefariki dunia
mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 56 kwa ajali ya gari, wametapakaa
katika nchi mbalimbali kama vile Denmark, Malta na Uingereza, pengine
wakila faida ya 'ugunduzi' wa baba yao.
Kwa upande mwingine, Mzee Ngoma
amejibanza katika ofisi ndogo ya mwanaye Asha katikati ya jiji. Fedha
pekee ambayo ameitengeneza kutokana na kuipa Tanzania sifa na utajiri
huu wa kipekee ni Sh elfu 50,000 zile alizopewa na Hayati Rashid Mfaume
Kawawa !
Namuuliza shujaa huyu wa taifa anataka
nini kutoka kwa serikali; "Sihitaji mambo makubwa sana. Ninachohitaji
ni kuishi maisha yanayofanana na Tanzanite. Nataka mtu akiniona mimi
aone Tanzanite," anasema.
Ni ombi ambalo linanisisimua.
Watanzania wanapaswa kuwafahamu watu kama akina Ngoma. Serikali inapaswa
kuwaenzi watu kama akina Mzee Ngoma.
Hawa watachochea watu wawe wagunduzi
zaidi. Simulizi zao zitafanya watu wajenge akili ya kuhoji kila
wanachokiona. Nani ajuaye, pengine kuna 'Tanzanite' nyingine katika
maeneo mbalimbali hapa nchini lakini hazijulikani kwa vile hakuna akina
Ngoma?
Nani atataka kuwa mgunduzi wa vitu vya
thamani iwapo wagunduzi waliopo tunapanda nao daladala, tunashinda nao
njaa na hawathaminiki?
Serikali imfanye Mzee Ngoma afanane na faida ambayo Tanzanite imeiletea nchi yetu.
- Sourse:raiamwema.co.tz
No comments:
Post a Comment