Nairobi. Wakati Serikali ya Kenya
imeliomba Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumkamata Mwingereza
Samantha Lewthwaite (pichani), taarifa zinadai kuwa mwanamke huyo
alipitia mpaka wa Namanga, Arusha kwenda Nairobi ambako anahusishwa na
tukio la ugaidi.
Lewthwaite, ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Mjane mweupe’ inaaminika anashirikiana na kundi la magaidi la Al-Shabab la Somalia.
Kundi hilo ndilo linaaminika lilihusika na mashambulizi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, taarifa ya Interpol ilisema
kuwa alikuwa anatakiwa kujibu mashtaka ya kumiliki mabomu na kupanga
njama za ugaidi Desemba 2011.
Interpol haikuhusisha maombi hayo ya Serikali ya Kenya na mashambulizi ya Nairobi.
Pia Lewthwaite inasemekana aliingia nchini humo kwa kutumia mpaka wa Tanzania.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika
ya Kusini, vinasema mwanamke huyo alitumia pasi ya kusafiri ya nchi hiyo
kuingia Kenya kwa kutumia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.
Taarifa hizo zinasema mwanamke huyo
alitumia mpaka wa Lunga Lunga na Namanga kati ya Februari na Agosti
mwaka 2011 akitumia jina la Webb.
Habari hizo zinaeleza kuwa, awali
mwanamke huyo alikuwa anaishi Afrika Kusini ambako aliweza kukopeshwa
fedha benki na kuweza kupanga sehemu ya kuishi.
Wakati huohuo, watu wanaodhaniwa kuwa
magaidi wamefanya shambulio kwenye Kituo cha Polisi mjini Mandera na
kuua askari wawili, kujeruhi watatu kisha kuchoma zaidi ya magari 11
jana asubuhi.
Shambulio hilo ni la pili kufanyika
kwenye maeneo mawili tofauti ndani ya saa 24, baada ya lingine
lililofanyika kwenye Mji wa Wajir, muda mfupi baada ya taarifa za
kudhibitiwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa magaidi walioshambulia jengo la
kibiashara la Westgate mjini Nairobi.
Shambulio hilo limefanyika wakati kikosi
maalumu cha wataalamu wa mabaki ya mabomu wa Kenya na wale wa kimataifa
kikianza kufanya upekuzi wa jengo hilo, ili kubaini wahusika halisi wa
shambulio hilo na aina ya silaha zilizotumiwa.
No comments:
Post a Comment