11 September 2013

Aua mumewe kwa wivu wa mapenzi

WATU watatu wamefariki dunia mkoani Morogoro kwa matukio tofauti, likiwemo la mwanamke mmoja kumuua mumewe kutokana na wivu wa mapenzi. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, tukio la mke kumuua mume wake lilitokea Septemba 8 mwaka huu, katika Kijiji cha Mbingu wilayani Kilombero.

Shilogile alisema mwanamke huyo, Shida Mbalwa (45) mkazi wa Mbingu, alimpiga mumewe, Habibu Adamu (45) katika paji la uso upande wa juu ya jicho la kulia na kumsababishia kifo.

Alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo ni kutokana na wivu wa kimapenzi na kwamba mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi.

Katika tukio la pili, lililotokea Septemba 7 mwaka huu majira ya saa 12 jioni, mtu aliyefahamika kwa jina la Juma Mambi (50) alikutwa amefariki dunia baada ya kudondoka kwenye mnazi alipokuwa akigema pombe ya mnazi.

Kamanda huyo pia alisema tukio jingine linamhusu Peter Larondola, ambaye umri wake haujafahamika, ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kutuhumiwa kuiba madebe mawili ya mpunga.

Kamanda Shilogile alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 mwaka huu, katika Kijiji cha Mhelule, Tarafa ya Mang'ula, Wilaya ya Kilombero, ambapo alikutwa akiwa na debe mbili za mpunga ukiwa pembeni.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname