11 September 2013

RC Pwani awavutia pumzi madaktari wezi

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Hajjat Mwantum Mahiza, amewaonya madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo wenye tabia ya kuiba dawa na vifaa na kisha kupeleka katika maduka yao ya mitaani kuacha mara moja kufanya hivyo. Mkuu huyo wa mkoa alisema atakayebainika akiendelea na mchezo huo atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Mahiza, alitoa onyo hilo jana, wakati akizindua huduma za mpango wa madaktari bingwa zilizoanza katika hospitali hiyo. Mpango huo upo chini ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaoendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali.

Kauli ya Mahiza ilikuja mara baada ya kukabidhiwa vifaa mbalimbali kutoka mfuko huo, vitakavyotumiwa na madaktari bingwa wanne waliopelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu.

Alisema wapo baadhi ya madaktari wenye tabia ya kukwapua vifaa hivyo na kupeleka katika maduka yao binafsi, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili yao ya kazi.

“Leo mmepewa vifaa hivi bure ili viwasaidie katika kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa, lakini sipendi kusikia kuwa mnahamisha na kupeleka katika maduka yenu.

“Nawaambia hapo patachimbika, kwani madaktari wengine wamejawa na tama, hasa pale wanapoletewa vifaa vipya na atakayehusika kibarua kitaota nyasi,” alisema Mahiza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Beatus Chijumba, alisema madaktari bingwa wanne waliopelekwa kutoa huduma katika hospitali hiyo ni wale wa magonjwa ya upasuaji, magonjwa ya ndani, dawa za ganzi na masuala ya uzazi.

Alisema huduma hiyo itakuwa endelevu katika mikoa mbalimbali iliyopo nchini, ambapo hatua ya kwanza tayari madaktari bingwa wamepelekwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Kigoma na Pwani.
Chanzo: Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname