14 April 2012

Lulu agomea chakula cha gereza la Keko……Kajala ampa uzoefu wa gerezani



MSANII wa Filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyepo kwenye gereza la Keko anakoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya msanii Steven Kanumba aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita na kuzikwa Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, juzi aligoma kula chakula cha gerezani hapo.
Habari za uhakika kutoka gerezani hapo, zimedokeza kuwa Lulu aligoma kula chakula cha gerezani, hivyo ndugu zake wakalazimika kumpelekea chakula kwa vile sheria za magereza zinaruhusu. Binti huyo aliyepelekwa gereza la Keko juzi baada ya kusomewa mashtaka ya mauaji ya Kanumba kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, atarejeshwa tena mahakamani hapo Aprili 23.

Kwa mujibu wa habari zilizothibitishwa na ofisa mmoja wa gereza hilo ambaye hakutaka jina lake kutajwa, tangu Lulu afikishwe katika gereza hilo juzi, hajala chakula cha hapo.
“Sio kama amegoma kabisa kula, isipokuwa amegomea chakula cha gerezani, hivyo akipelekewa na ndugu zake, anakula. Chakula cha humu ndani hagusi kabisa tangu aje hapa”. Chanzo hicho pia kilipasha kwamba Lulu hajaugua kama watu wanavyodai.
Sayari iliamua kutafuta habari za Lulu gerezani hapo baada ya jana kuenea kwa taarifa kuwa, alikuwa anaumwa hadi kupepekwa hospitali ya Mwanyamala, kitu ambacho chanzo hicho cha uhakika, kilisema ni uzushi mtupu. Aidha, chanzo hicho kiliongeza kuwa, Lulu hana unyonge garezani, kwani amepata faraja baada ya kukutana na msanii mwenzake, Kajala Masanja.
“Lulu si mnyonge, yupo kwenye hali ya kawaida sana, amepata rafiki yake Kajala… wanazungumza na kucheka… wako na furaha tu,” kilisema chanzo hicho.  Juzi, msanii huyo maarufu kama Lulu (17), mkazi wa Tabata alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumuua msanii maarufu nchini Steven Kanumba kinyume cha kifungu cha sheria 7/4.
Mbele ya hakimu mkazi Kisutu, Agustino Mbando, mwendesha mashtaka wa serikali Elizabeth Kaganda, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican jijini Dar es Salaam. Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu hoja yoyote dhidi yake na upelelezi wa tukio hilo unaendelea. Kesi hiyo itatajwa tena April 23.

chanzo  jukwaahuru.com

1 comment:

  1. tunakosea sana watu ambao tunatoa habari za kiongo ivyomm naumia sana na ninaomba siku ziende harka mpaka tarehe 23 ili haki itendeke

    ReplyDelete

Comments system

Disqus Shortname