07 February 2016

Mbowe anamng'ata na Kumpuliza Zitto? aeleza sababu ya kumtosa Uwaziri Kivuli



Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana alitangaza orodha ya majina ya wabunge wa upinzani wanaounda baraza la mawaziri vivuli, huku akimtosa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
Mbowe na Zitto walikuwa marafiki wakubwa waliozunguka nchi nzima kuijenga Chadema kwa miaka kumi iliyopita, kabla ya kugeuka kuwa mahasimu wakubwa wa kisiasa ndani ya mwaka mmoja tu. Chadema walimtuhumu Zitto kwa usaliti na kufikia hatua ya kumtimua katika chama hicho.
Hata hivyo, uamuzi wa Chadema ulimpa Zitto akili ya ziada ya kuanzisha chama kipya cha siasa cha ACT-Wazalendo ambacho kilishiriki uchaguzi Mkuu na kumsimamisha mgombea urais, Bi. Anna Mghwira na wabunge wengi.
Lakini, kwakuwa siasa haina urafiki au uadui wa kudumu, katika mkutano wa pili wa Bunge la 11, Zitto Kabwe, Freeman Mbowe na wabunge wengine wanaounda Ukawa walionekana kushirikiana kwa karibu kupinga hoja za CCM na kutoka na msimamo mmoja.
Sio Mbowe peke yake, hata Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambaye alikuwa hasimu mkubwa wa Zitto akimshambulia kwa maandishi kwenye gazeti lake la Mwana Halisi, alionekana kuwa karibu naye na kushirikiana.
Kadhalika, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu aliyekuwa kinara wa kumtimua zitto Chadema na kusimamia kesi mahakamani kuhakikisha n Zitto anaondoka katika chama hicho, alishirikiana naye kwa ukaribu kuomba miongozo iliyowabana wabunge wa CCM. Hali iliyomuonesha Zitto kuwa ndai ya kundi la wabunge wa vyama vinavyounda Ukawa.
“Kushirikiana na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukifanya. Yapo majeraha mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi kuyatibu kwa siku moja. Yapo ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa kinawezekana,” Mbowe alieleza hivi karibuni.
Kutokana na kutomuweka Zitto kwenye orodha ya mawaziri vivuli, nafasi ambayo Zitto angeweza kuimudu bila shaka kutokana na uwezo wake kisiasa, Mbowe alilazimika kueleza sababu na vigezo walivyotumia kumkata.
“Ukawa tulisaini tamko la pamoja la ushirikiano na hiyo ilikuwa katika Bunge la Katiba. Kumbuka tumeshirikiana katika Uchaguzi Mkuu na kupata madiwani na wabunge ambao ndiyo hawa wamezaa baraza hili,” alisema.
“Ushirikiano wetu upo katika halmashauri na majiji. Kutokana na jambo hilo huwezi kuiingiza ACT maana haikuwapo katika makubaliano ya Ukawa,” aliongeza Mwenyekiti huyo wa Chadema.
Pamoja na mambo mengine yaliyojitokeza Bungeni, Zitto aliungana na Ukawa kupinga kitendo cha Serikali kutangaza kuwa TBC haitaonesha ‘Live’ baadhi ya vikao vya Bunge na hata wote waliondoka bungeni na kukaa pamoja kuzungumza na vyombo vya habari.
Hata hivyo, baada ya Mbowe kutangaza baraza hilo kivuli, Zitto aliwapongeza na kuahidi kushirikiana nao.
Hongera sana dada yangu @halimamdee kuteuliwa kuwa Waziri Kivuli Fedha na Mipango. Nitakupa Ushirikiano katika kuisimamia Serikali

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname