11 February 2016

Dk Phillip Mpango Akataa Kuwa Waziri OmbaOmba......Asema Serikali Haipo Tayari Kukubali Ndoa Za Mashoga Kisa Misaada Ya Wahisani

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema hatua ya Serikali ya kukusanya kodi kwa nguvu kwa baadhi ya wafanyabiashara waliotorosha makontena bila kulipiwa ushuru, haikuwa lengo la kumkomoa mtu, bali ililenga kukusanya fedha za Serikali yenye lengo la kuifanya nchi iache utegemezi wa wahisani.

Waziri huyo ambaye jana alikutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara ofisini kwake Dar es Salaam, alisema yeye kama waziri wa fedha asingependa kuwa waziri ombaomba kwa wahisani, ambao alidai baadhi yao wana masharti magumu, ambayo hayatekelezeki kwa maadili ya Watanzania.

“Nimewasindikiza wenzangu huko nje kuomba fedha sasa nimechoka, nataka kutembea kifua mbele, maana wana masharti magumu, wengine wanataka turuhusu homosexual (ndoa za jinsia moja), masharti haya kwa kweli yanakera sana,” alisema Dk Mpango ambaye katika serikali iliyopita alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango.

Dk Mpango aliongeza kuwa ili nchi isonge mbele, ni lazima ikusanye kodi ya kutosha; na jana aliahidi kuchukua hatua kadhaa, zitakazoiwezesha sekta binafsi kuwa mhimili wa kuimarisha uchumi wa nchi ili kufikia malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati.

Alisema Rais John Magufuli ni kiongozi ambaye akilala na kuamka, anawaza namna ambavyo atawahudumia wananchi wake, ambao wengi wako kwenye dimbwi la umaskini.

Alisema Rais atafanikiwa tu, pale Serikali yake itakusanya kodi ya kutosha na kuwahudumia wananchi hao.

“Kuna minong’ono kwamba eti Serikali ya Awamu ya Tano inawanyanyasa wafanyabiashara wakubwa na kwamba hatua tulizochukua kukusanya kodi, ililenga kuwadhalilisha baadhi ya wafanyabiashara, hii sio kweli kabisa,” alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alisema Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua umuhimu wa wafanyabiashara, hivyo wizara yake itakuwa ya mwisho kuchukua hatua za kuwanyanyasa.

“Nawahakikishia kwamba nina dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana na ninyi wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili tutimize ndoto ya Rais,” alisema.

Alisema serikali yoyote duniani ni lazima ikusanye kodi, hivyo aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa kama bado kuna wafanyabiashara wanaokwepa au hawataki kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, serikali haitakuwa tayari kuwavumilia.

Dk Mpango alisema idadi ya watu wanaolipa kodi kwa sasa nchini bado wachache, hivyo aliwaagiza wafanyabiashara wote kujisajili wapatiwe Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN).

Pia, aliwataka waache tabia ya kufanya udanganyifu kwa kuwa na vitabu vingi vya utunzaji wa kumbukumbu za biashara. Aliwaagiza kuhakikisha wanatoa stakabadhi na suala hilo lisiwe hiyari.

“Tunajua kwamba mnatoa vitisho kwa wanunuzi kuwa kama wanataka risiti bei ni ya juu, hiki mnachofanya ni hatari kwa nchi,” alisema na kuwataka wote watumie mashine za EFD na serikali inaendelea na mpango wa kununua zingine ili wagawiwe bure.

Aliwataka kutoa taarifa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, kama kuna mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) au wa Halmashauri ya Wilaya, ambaye atadai hongo au atawanyanyasa wakati wa kudai kodi.

Katika kutekeleza hilo, aliwapatia namba zake pamoja na za Kamishna na kuwataka waache tabia ya kutoa rushwa ili wasilipe kodi.

 Dk Mpango alisema baada ya wafanyabiashara kufanya kikao na Rais Magufuli, Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia kero zote, zilizotolewa na Baraza la Biashara na mojawapo ni kufuta utiriri wa kodi ili kuwapa wepesi wawekezaji kufanya biashara nchini na kumpungumzia mzigo mkulima.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname