TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI WA MABONDENI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Utangulizi
Nchi yetu ina kingo za mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo
watu wanaishi kinyume cha sheria, huku wakiharibu mazingira na
kuhatarisha maisha yao. Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya
zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto
Msimbazi.
Serikali za awamu zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi
wa maeneo ya mabondeni wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria
lakini mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.
Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa
sheria za nchi, imeanza jitihada za kuwaondoa wakazi hawa.
Tuliamua kuanza na Bonde la Mto Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu
wengi na athari kubwa.Sababu zetu kuu za kufanya zoezi hili ni kusafisha
mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na mazingira yanayozunguka
ni:-
Kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo
la Bonde la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi
binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.
Kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa
kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa
wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu,
hasa wakati wa mvua;
Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo
nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na
iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio
zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa.
Baada ya hapo, mkazi hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.
Kutokana na utaratibu huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa wenyewe.
Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi
hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni
wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama.
Serikali pia imeweka Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini ya Zoezi
Jana, terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa
mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali,
inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira,
ambayo, pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya
kubaini makazi yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la Mto
Msimbazi imekamilika.
Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa, wananchi katika nyumba 774 wamehama
na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa
kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa.
Kutokana na uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za
makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi.
Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi hilo.
Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: -
1.Zoezi la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo
hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu
kwa wananchi;
2.Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3.Kwa wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao
yamo NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na
kwenye KINGO za mto;
4.Wale watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma,
zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo,
hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa
umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria;
5.Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
6.Serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na
baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe
haraka ili taratibu zinazofuatia zifanyike;
7.Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha
zoezi hili kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa, na kinyume na
misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka alama za X zaidi ya mita
zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la malalamiko katika Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au
maswali kuhusu zoezi hili.
8.Nyumba na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya
kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa
isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika
makazi hayo watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na
kujiokoa na maafa;
9.Serikali haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi
yaliyo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli
haya watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa
Sheria.
10.Serikali inaweka uratibu wa karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake
ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe chanzo cha taharuki
katika jamii.
11.Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha
kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali
haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha
mvua kubwa maisha yao yapo hatarini.
Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio
mabondeni walipoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali
ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko zilizowahi
kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
12. Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa
juu ya taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba ya
Mchungaji Rwakatare. Ilielezwa kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga
nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto kwa kujaza kifusi ili
kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume kabisa na
Sheria tatu muhimu.
Pia ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za
kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini
ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa
nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani.
Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza,
yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11
Mei 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa
niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba
ya Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei
2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi
Oktoba 2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano
ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata
taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa
mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa TAKUKURU.
Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza Baraza kufungua shauri
mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na Mchungaji Rwakatare
yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya udanganyifu. Shauri
hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu hoja inayozungumzwa kwamba wananchi
wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni lakini mradi wa DART
umeachwa.
Mkutano ulielezwa kwamba Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa
nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa
kufanyika katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri mwenye dhamana ya
mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo
zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira.
Mradi wa DART ulipata kibali hicho na una mkataba na Baraza la
Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya mazingira zinazopaswa kutekelezwa
katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
No comments:
Post a Comment