Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limezuia maandamano ya Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo(Chadema) yaliyopangwa kufanyika Kesho Novemba
03,2015 katika mji wa Shinyanga kwa lengo la kupinga matokeo
yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktoba 25,2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo asubuhi kamanda wa polisi mkoa wa
Shinyanga SACP Justus Kamugisha amesema wamezuia maandamano
yaliyopangwa na Chadema kufanyika Novemba 03,2015 asubuhi akidai kuwa
katika kipindi hiki hawaruhusu kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa
sababu jeshi la polisi limejikita katika kuangalia hali ya usalama
utawale ili kusubiria kuapishwa kwa rais mteule na wabunge.
Amesema pia wamezuia mikusanyiko yoyote isiyo rasmi ambayo inaweza
kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani kwani kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Kamugisha amesema Chadema wametoa taarifa kuwa Kesho wanataka
kuandamana kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya taifa
ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25,2015 na baada ya kufanya maandamaano
hayo wanataka kutoa ujumbe kwa serikali.
Amewashauri wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga wasishawishiwe na
viongozi wa vyama vya siasa,na kuwaomba wabaki majumbani,waendelee na
shughuli zao na kutokubali kurubuniwa au kushawishiwa kuandamana kwani
wanaowashawishi hawatakuwa mbele .
Katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga mjini
George Kitalama amesema hawajapata taarifa wala maelekezo yoyote kuhusu
kuzuiwa kwa maandamano yao na wanaendelea kujiandaa na wanachama wao kwa
maandamano kama walivyopewa maagizo na viongozi wao wa kitaifa.
Amesema kesho 03.11.2015,watafanya maandamano
ya amani kuanzia ofisi za Chadema wilaya kisha kuzunguka mji mzima wa
Shinyanga kuanzia saa tatu asubuhi kupinga matokeo ya uchaguzi
yaliyotangazwa na tume,na kwamba ni maandamano ya nchi nzima siyo
Shinyanga pekee

No comments:
Post a Comment