Wanachi wakitaharuki vyombo vilivyoweka juu ya kaburi marehemu, Jesca Onesmo.
Wahenga walisema ukisitajabu ya Musa utaona ya Farao, hivi ndivyo
ilivyokuwa kwa wananchi wa mji wa Bariadi mkoani Simiyu waliofurika
katika kaburi la marehemu, Jesca Onesmo (28), ambaye alifariki kisha
kuwekewa samani na vyombo vyake mbalimbali juu ya kaburi lake.
Marehemu, Jesca Onesmo enzi za uhai wake.
Ilikuwa asubuhi ya saa mbili, Julai 7, mwaka huu ambapo baadhi ya
wananchi wa Mtaa wa Marambo, Bariadi waliokuwa wamepata msiba
walipokwenda eneo la Makaburi ya Kidinda kwa ajili ya kutafuta mahali pa
kuchimba kaburi, walipofika eneo hilo walipigwa na butwaa baada ya
kuona kaburi moja likiwa limewekewa vitu juu, hali ambayo ilitafsiriwa
kuwa amezikwa navyo.
Uwazi baada ya kupewa habari hiyo lilifika katika eneo hilo na kukuta
samani za ndani, godoro na vyombo mbalimbali vikiwa vimerundikwa juu ya
kaburi hilo na baada ya uchunguzi ikajulikana kuwa ni kaburi la Jesca.
Mwananchi mmoja ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema:
“Kwa kweli hili ( la kurundikwa vyombo vyake juu ya kaburi)
limetushangaza sana na ni la kwanza kutokea hapa Bariadi, hata sisi
hatujui sababu lakini labda ni ushirikina.”
Baada ya tukio hilo polisi waliarifiwa ambapo walifika makaburini na
kuamua kuvipakia vyombo hivyo kwenye gari la polisi na kuvipeleka
kituoni na baada ya kufika huko walivifanyia upekuzi na kugundua vitu
mbalimbali.
Habari za kipolisi zinasema walikuta pochi ya marehemu ambayo ndani yake
ilikuwa na shilingi 13,000 pamoja na simu ndogo lakini pia walifanikiwa
kukuta cheti cha hospitali kilichoonesha marehemu alikuwa mgonjwa na
alikuwa anatumia dawa kila siku.
Aidha, walipata pia daftari la mchango wa kifo ambalo lilionesha kuwa
alichangiwa na walipata jina na namba za simu ya dada yake (jina
linahifadhiwa) ambaye inadaiwa kuwa ndiye aliyehusika kumzika ingawa
baada ya kumpigia simu hakupokea na walipomfuatilia walikuta ametoroka
na familia yake, hadi sasa haijafahamika alipo.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo kutangazwa na vyombo vya habari baadhi
ya wananchi walidai kuwa marehemu alikuwa anaishi na mume wake huko
wilayani Kahama na hawakujua nini kilitokea hadi kuzikwa na kurundikiwa
vyombo juu ya kaburi lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Gemini Mushy amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
“Tukio hilo lipo lakini tunaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo
chake na sababu ya kumzika na vyombo vyake,” alisema kamanda huyo.
No comments:
Post a Comment