06 January 2014

ZITTO AANIKA UFISADI WA MBOWE,JIONEE HAPA





MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ameshusha tuhuma nzito dhidi ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, zikimhusisha na ufisadi.

Hata hivyo, Mbowe naye amejibu tuhuma hizo akisema ni busara zaidi kwa mhusika kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake badala ya kuibua tuhuma nyingine.

Madai hayo ya Zitto kwa Mbowe ni kilele cha siasa za kuchafuana, kutukanana na kuvunjiana heshima kilichodumu kwa takribani miezi mitatu sasa kupitia vyombo tofauti vya habari.

Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa facebook jana jioni, Zitto alisema Mbowe hawezi kumnyooshea yeye kidole kuhusu masuala ya maadili kwa vile yeye mwenyewe (Freeman) ndiye mvunja maadili namba moja ndani ya chama hicho.
 
Jana mchana, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba Zitto amepewa magari mawili na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono; ambaye ni mmoja wa watu waliotajwa na chama hicho kama mafisadi.

"Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Mbowe Sh. milioni 40 ili Mbowe asifanye kampeni Jimbo la Musoma Vijijini.

“Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman Sh. milioni 20 za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa.

“Nadhani alimwambia pia kuwa mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe Sh. milioni 200 za Kampeni ya Slaa. Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe Sh. milioni 100 za kampeni. Lissu anajua....?

“Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda.

“Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu. Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Kinana na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya Umma ilipo Club Bilicanas.

“They must know I am not a push over (Ni lazima wafahamu kwamba mimi si mtu wanayeweza kumchezea wanavyotaka). Chacha (Wangwe) died, I won't (Chacha Wangwe alikufa, Mimi Hawaniwezi.”

“Mtu ambaye hawezi kuheshimu ...... hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili," aliandika Zitto katika ukurasa wake wa facebook baada ya Tundu kutoa tuhuma zake.

Lissu alikuwa akizungumza katika mkutano ambao Chadema ilitangaza kuwafuta uanachama wanachama wake wawili; Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.

Zaidi ya kuwafukuza akina Kitila, chama hicho jana kimewaagiza viongozi na wanachama wake kutoshirikiana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia chama hicho, Zitto Kabwe.

Zitto alifungua kesi wiki iliyopita akitaka kamati hiyo isijadili uanachama wake, lakini hatua hiyo ya kamati kuu kuwaagiza viongozi wake wasishirikiane na Kabwe kwenye masuala ya Chadema, imetafsiriwa kama kumfanya si mwanachama.

Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando, ameliambia gazeti hili jana kwamba ilichofanya Kamati Kuu (CC) kwenye kikao hicho kuhusu Zitto ni “kuingilia uhuru wa mahakama” kwa vile tayari wameshampa adhabu wakati Mahakama inasikiliza shauri lake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alisema wamechukua hatua hiyo kwa sababu wamebaini Kitila na wenzake walikuwa na lengo la kubomoa Chadema.

“Viongozi hawa walikuwa wameandaa mkakati wa muda mrefu wa kukibomoa chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi,” alisema Slaa.

Slaa alikuwa akizungumzia waraka wa siri ulioandaliwa na Kitila na Mwigamba uliotaka kufanyika kwa mabadiliko katika ngazi ya juu ya uongozi wa chama hicho.

Majibu ya Mbowe

Akizungumza na mwandishi wetu Mbowe alisema ni utoto kukwepa kujibu hoja kwa kuanzisha tuhuma dhidi ya mtu mwingine ambazo si za kweli.

“Mimi nimekuwa nikisimamia ukweli, mtu anapotuhumiwa ni lazima ajibu tuhuma hizo. Ni utoto kuacha kujibu tuhuma na kuzusha tuhuma nyingine. Anapaswa kufanya utetezi wa tuhuma zinazoelekezwa kwake.

“Mimi ni mbunge, bungeni nimekuwa nikichangia watu mbalimbali mimi kama Freeman, si ajabu watu wengine kunichangia. Hapa jambo la msingi ni kwamba unapewa pesa kwa sababu gani, kwa nia ipi? Kupewa pesa na Kikwete au CCM si tatizo lakini unapewa pesa kwa sababu zipi, kwa malengo gani?” alihoji Mbowe.

Mbowe alilaumu baadhi ya vyombo vya habari kushiriki kumchafua kwa taarifa za kutunga kutoka kwa watu anaodhani wamekuwa na uhusiano na Zitto.CHANZO JF

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname