MHESHIMIWA Rais wangu, Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa salamu ya utii inayotambua na kuheshimu
kwa dhati mamlaka makubwa na ya juu uliyonayo kama mkuu wa taifa letu
ambalo mazingira yake ya leo yanapaswa yawe wenye mwelekeo wa
kushangilia kama si kujivunia uhuru ambao tuliupata mwaka 1961 na 1964
kwa kutegemea upande tulipo katika muungano wetu.
Mheshimiwa Rais, najisikia faraja
iliyojaa majonzi moyoni kupata fursa hii adhimu kukuandikia waraka ambao
msukumo wake unasukwasukwa na dhamira njema kabisa ambayo aghalabu
kiini chake si kingine bali mapenzi mema kwa nchi na viongozi wetu wote.
Ni faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali
na adimu ya kuteta na kiongozi wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa
kujiamini, huku nikiwa na uchungu pia kwa sababu ujumbe ambao unabebwa
na waraka huu ni wa kuumiza sana nafsi, roho, akili na mwili.
Mheshimiwa Rais, wewe ni kiongozi wa
Watanzania wote tukiwamo sisi ambao baadhi ya wateule wako wameamua kwa
sababu wanazozijua wao na wakati mwingine wakidai kwa maelekezo ya wakuu
wao kutujengea taswira zinazotufanya tuonekane tu watu wa ovyo na kada
ya wanajamii waliokosa utu na eti tunaopaswa kufundishwa hekima na somo
la uzalendo ambalo limekuwa sehemu ya makuzi yetu nyumbani, shuleni,
jeshini na ndani ya jamii.
Kabla sijafikisha ujumbe ambao
nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito moyoni, napenda kwanza kupitia fursa
hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na neema kwa
kuniwezesha kuuona mwanga wa siku hii njema ya leo ambayo kama si kwa
kudra na mapenzi yake, yumkini ingeongeza hesabu za siku ambazo
kiwiliwili changu kingekuwa katika kaburi la sahau ambalo kila kukicha
linameza roho za makumi kama si mamia ya Watanzania wasio na hatia
wanaopoteza maisha kutokana na kazi za mikono ya majahili, miungu watu
waliojitwalia haki ya kuchagua aina ya maisha na vifo vya watu wengine.
Baada ya hilo, kwa niaba ya mamilioni
ya Watanzania wenzangu ambao hawana fursa ya kuwasiliana nawe kwa njia
kama hii ya waraka niliyoitumia, napenda kutumia pia wasaa huu
kukushukuru wewe binafsi kwa namna ulivyojitoa usiku na mchana pasipo
kuchoka kuliongoza taifa hili katika mazingira magumu yaliyojaa
changamoto za kila namna ambazo wakati mwingine sina shaka hata kidogo
kwamba zimekuwa zikikunyima raha na kukosa usingizi.
Wakati nikikuandikia ujumbe huu, picha
na taswira yako inayonijia ni ile ya Machi 8, mwaka huu siku
uliponitembelea kando ya kitanda nilichokuwa nimelazwa katika Hospitali
ya Milpark, Johanesburg kule Afrika Kusini ikiwa ni siku mbili tangu
nilipovamiwa, nikajeruhiwa na kupewa ulemavu na majahili ambao hadi leo
hii wameweza kuukwepa mkono mrefu wa vyombo vya dola unavyoviongoza.
Mheshimiwa Rais, japo nilikuwa nina
maumivu makali na machungu ya kupoteza jicho, kidole na kupasuliwa kwa
mifupa ipatayo minane katika paji langu la uso, ukiacha taya
lililoachanishwa kikatili na watesi wangu wale, bado ninaweza kukumbuka
kwa ufasaha namna ulivyozungumza nami ukionyesha jinsi ulivyokuwa
ukiguswa na kuumizwa sana na tukio lile.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba,
tangu niliporejea nchini miezi sita iliyopita sijapata kukutana nawe ana
kwa ana ingawa nilipata fursa ya kukutumia salamu zangu za shukrani
kupitia kwa marafiki zako kadhaa akiwamo msaidizi na mshauri wako
nambari moja, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote
wakati nikiwa katika matibabu nchini Afrika Kusini na hata baada ya
kurejea nchini, alionekana kuwa mtu wa kukosa amani kabisa pasipo
kunijulia hali kwa njia ama ya simu, wasaidizi wake na mwisho kwa
kuonana nami ana kwa ana.
Nayarejea haya yote huku nikitambua
kwamba, wakati ninapoandika waraka huu ndiyo kwanza umerejea kutoka
nchini Marekani ambako ulikwenda kuchunguzwa afya yako ambayo nina
matumaini makubwa ni njema hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa, ulikwenda
huko siku chache tu baada ya kuiwakilisha vyema nchi yetu katika msiba
mzito wa shujaa wa mapambano ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,
mzee wetu, Nelson Mandela.
Ninapoyatafakari matibabu ghali
niliyopata nchini Afrika Kusini kwa msaada wa mwajiri wangu na safari
yako nchini Marekani, vinanikumbusha swali la mmoja wa wasaidizi wangu
hapa ofisini aliyetaka kujua ni sababu gani hasa ambazo zimekuwa
zikisababisha wasomi na viongozi wetu kuchunguzwa na kutibiwa katika
hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa kwa Madiba ambaye kwa nyakati
zote tangu afya yake ianze kumtatiza alikuwa akipata matibabu huko huko
kwao Afrika Kusini?
Niseme kweli, japo nilikuwa na jibu au
majibu ya swali lake, sikuwa na maelezo ya kutosheleza yaliyokuwa na
mwelekeo wa kukata kiu ya swali lake, ingawa kwa kupapasa nilifanya kila
juhudi kuutetea utaifa wangu na viongozi wake ilhali miye mwenyewe
nikiendelea kukosa raha kwa namna nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo
yalikuwa yakionyesha hali ya kuukubali unyonge, kukiri ufukara, kuficha
udhaifu wetu kama taifa na kutetea makosa ambayo aghalab ninyi viongozi
wetu na wale wa kabla yenu mngeweza kuwa watu mliostahili kuwa na majibu
halisi.
Rais wangu, swali na majibu
vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali mengi mengine na moja ya
maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia hata tukafikia hatua ya
kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu waliokata tamaa, wanaoteswa na
ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina ya kero na karaha zinazozonga
maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Rais, hali hiyo ilinipeleka
moja kwa moja nchini Afrika Kusini na hususan katika Hospitali ya
Milpark ambako huko ndiko miye mwenyewe na Watanzania wenzangu wengine
tulikonusuru maisha yetu, huku baadhi kama ilivyo kwa Dk. Sengondo
Mvungi wakipoteza maisha yao baada ya kukimbizwa huko.
Mheshimiwa Rais, naomba unisamehe kwa
kulisema hili nitakaloliandika hapa kwamba, jibu nililolipata haraka
haraka kuwa moja ya chagizo la matukio ya namna hii kutokea, halikuwa
jingine bali ni kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa viongozi wetu hususan
wale tuliowapa dhamana ya kuongoza sekta kadhaa nyeti kama ya afya na
ustawi wa jamii.
Ushahidi wa kupwaya huko kwa viongozi
hususan wale walio chini yako, ndiko huko huko ambako kumedhihirika pia
wiki iliyopita bungeni Dodoma, ambako tulishuhudia zahama nyingine
iliyowang’oa madarakani mawaziri wako muhimu wanne kwa sababu kama hizo
hizo za mkwamo wao au watendaji wa chini yao katika kusimamia ipasavyo
na kuchukua hatua kwa wakati, kila yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo
wanayoyaongoza.
Nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu,
mheshimiwa Rais iwapo nitaficha shauku ya moyo wangu ambayo ilikwenda
sambamba na tukio lile la Dodoma lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao
anguko lao linaweza likaelezwa kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia
msamiati ulioutumia wewe mwenyewe kwa mara ya kwanza ulipozungumzia
tukio la kujiuzulu kwa waziri wako mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.
Haja ya moyo wangu, nikiwa mhariri,
mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na mdadisi
wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa kuona anguko la namna hiyo hiyo
likimfika Waziri wa Habari ambaye amethibitisha pasipo na shaka kuwa
pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya Falsafa (Phd), ni kiongozi asiyejua
anachofanya kwa kiwango cha kuwa mtu ambaye vichwa vya watu wengine
ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.
Nilitamani afikwe na zahama hiyo si kwa
sababu ya kuwa na hasira au kumchuria mabaya, bali kwa kuzingatia
ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye bado anasongwa na matongotongo ya mfumo
wa kibabe wa zama za magazeti ya Serikali na yale ya chama tawala,
ambayo yanalazimika kuandika yale tu yanayofurahisha nyoyo na akili za
watawala.
Mheshimiwa Rais, ingawa natambua na
kuheshimu ukweli mchungu kwamba, suala la nani awe waziri na nani asiwe
ni jambo la wewe mwenyewe kupenda na kuchagua na kwamba ulishasema
mapema kabisa mbele yetu kwamba urais wako hauna ubia, bado naamini pia
kwamba, wewe ni mtu msikivu na mkweli uliye tayari kusikia na
kustahimili mambo mengi machungu unayokabiliana nayo kila siku.
Kwa sababu hiyo, basi napenda kukueleza
kwa kuweka kumbukumbu sahihi ili mbele ya safari kabla na baada ya
kumaliza urais wako uje kuyatafakari na kuukumbuka ushauri huu kwako
kwamba, waziri uliyempa dhamana ya kulea na kuendeleza vyombo vya
habari, ni mtu wa kuhofiwa, jeuri, mwenye kiburi, asiyeshaurika na
dikteta asiyekutakia mema wewe binafsi, vyombo vya habari, serikali yako
na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa rais sijui kama unajua
kwamba tangu umteue amefanya kazi na vyombo vya habari vya umma na hata
baada ya sisi kufanya juhudi kubwa ya kuwa karibu naye kikazi kwa
makusudi na kwa ujeuri mkubwa, amekataa wito na kupuuza maoni na ushauri
wetu na kwa namna ya kusikitisha amesikika akitamba waziwazi kwamba
anao uwezo wa kulifungia au kulifutia usajili gazeti lolote ambalo
ataliona linakwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari.
Waziri huyu ambaye alitarajiwa kuwa na
silika za kuwa mlezi bora kutokana na jinsia yake na historia yake ya
kupata kuwa mwanaharakati kabla ya kuingia serikalini, ndiye ambaye
mamlaka makubwa uliyomtwisha, ameyageuza na kuwa mwavuli wa
kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye uthubutu wa kukosoa serikali na
kuandika ukweli mchungu ambao asingependa kuona ukiripotiwa.
Mheshimiwa Rais, pengine baya zaidi kwa
tasnia hii ni kwamba waziri huyo ana bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa
wasaidizi na washauri wake katika sekta yetu ya habari ambaye naye,
hulka zake tangu aingie katika tasnia ya habari amekuwa ni mtu wa
kujipendekeza, kupenda makuu, kuzusha na kutokuwa na mawazo huru. Huyu
si mwingine bali Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
Ni jambo la bahati mbaya kwamba waziri
huyu msomi pengine kwa sababu ya kutojua vyema rekodi na historia ya
msaidizi wake huyo, ambaye japokuwa naye pia ni mteule wako, amejikuta
akiwa mhanga wa fikra pandikizi zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu
mahususi unaofanywa na baadhi ya wateule wako ambao wameshaanza
kujipanga kusaka urais baada ya wewe kustaafu.
Mheshimiwa Rais, nimelazimika kuyasema
yote haya baada ya kula kiapo cha moyoni huku nikirejea mafunzo
tuliyokuwa tukikaririshwa utotoni chini ya imani ya wana TANU, ambayo
hata sisi ambao hatukuwa wanachama wa chama hicho tulilazimika kuikariri
kwa kuitamka kila kukicha; ‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.’
Rais wangu, gazeti la MTANZANIA
limerejea tena mitaani. Japokuwa ni rahisi kuhesabu miezi, napenda
kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi mitatu michungu sana kwetu kihisia na
katika hali halisi.
Nitakuwa mzushi sawa sawa na hao
ninaowashangaa leo, iwapo nitasema kulikuwa hakuna hitilafu au makosa ya
kiuandishi ambayo yaliwapa kisingizio cha mikakati waliyoipanga mapema
kabisa, wasaidizi wako hao kwa kulifungia gazeti letu hili.
Mheshimiwa Rais, nasema haya kwa sababu
ni ukweli ulio bayana kabisa kwamba, habari zilizoandikwa na kutoa
mwanya kwa serikali yako kutuadhibu gazeti hili, hazikulenga kuchochea
na wala hazikuchochea kabisa chuki yoyote dhidi ya yeyote na mamlaka
unazoziongoza kwa namna na kwa njia yoyote ile.
Siyo siri hata kidogo, mkurugenzi
aliyetangaza uamuzi huo alifanya hivyo akijua watu wengi hawajui mapito
na dhamira yake. Tunajua yeye alimshauri vibaya waziri na serikali huku
akijua vyema kwamba, yuko hapo alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la
watu wenye malengo binafsi ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati
wowote na mahali popote kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati
utakapotaka kuchukua maamuzi ya haki na kweli ujue undani halisi wa
mambo haya.
Leo hii wakati tukirejea tena sokoni,
tayari tumeshasikia kuendelea kuwapo kwa mikakati ile ile ya kuhakikisha
gazeti hili na jingine ambalo halipendwi na watu hao hao kwa sababu
binafsi yakiinaingizwa tena mtegoni na kufungiwa kifungo kingine kama
hiki tulichomaliza au kinachofanana na kile kilichoifika MwanaHalisi.
Mheshimiwa Rais, naandika waraka huu
nikikumbuka semi zako mbili unazotumia; ‘tunajenga nyumba moja kwanini
tugombee fito?’ na ile ya ‘akili za kuambiwa changanya na zako’ ambazo
kwa muktadha wa waraka wangu huu kwako zinaweza zikawa za msaada sana
kwako na pengine kwetu sisi wa MTANZANIA ambao tunashangilia kurejea
mtaani kwa gazeti letu lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa muda wa
siku 90.
Nimelazimika kukutumia wewe Rais si kwa
lengo la kuchosha akili zako au kukupotezea muda, isipokuwa kwa
kutambua hadhi, heshima na mamlaka makubwa uliyonayo juu ya wateule wako
hao ambao wameamua kwa sababu ya jeuri za kimamlaka walizonazo kuumiza
watu na kutupa sifa na majina mabaya tusiyostahili. Hakika wazungu
walikuwa sahihi waliposema ‘power currupts’.
Mheshimiwa Rais, lingekuwa ni jambo la
kheri kwa Serikali na kwa taifa letu zima iwapo kusudi la kufungia
magazeti linalopangwa na wateule wako kuwa utamaduni wa kudumu,
lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema kwako wewe binafsi, chama chako,
Serikali unayoiongoza na nchi yetu kuliko hili la sasa lenye dhamira ya
kufunga watu midomo, kutesa, kuzusha na kuharibu taswira yetu kama watu
binafsi, taasisi na taifa.
Ni kwa sababu hizo, mheshimiwa Rais
ndiyo maana baada ya kusukwasukwa na moyo na kuumizwa mno kifikra
nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu na haki za maelfu ya
Watanzania ambao tunaamini wanahitaji huduma ya magazeti haya katika
kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha, kielimu na kiufahamu kila
kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani zikiendelea kuongoza sekta
yetu.
Mheshimiwa Rais, siyo siri hata kidogo
kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi ya uhuru wa kikazi na kiwajibikaji wa
vyombo vya habari na wanahabari yanaonekana kutawala kauli na maamuzi ya
baadhi ya viongozi na washauri wako kwa kiwango cha kukushawishi hata
wewe binafsi kukubaliana nayo, ukweli ni kwamba, nyuma ya maneno matamu
wanayotumia kutupaka matope, kutujeruhi na kutupa kila aina ya sifa
mbaya kuna ajenda za kutuharibia sisi, kukuharibia wewe, kukomoa,
kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.
Nitakuwa mhariri nisiyewajibika, iwapo
nitakaa kimya ilhali nikijua fika kwamba, leo hii ndani ya wizara
iliyopewa dhamana ya kulea vyombo vya habari, baadhi ya wateule wako na
watendaji wake wamekalia viti walivyonavyo si kwa sababu ya kuwa kwao na
uwezo kustahimili ukosoaji, au upeo wao wa kuchochea maendeleo ya
kitaaluma, bali kwa kuendeleza na kuyatumikia matakwa ya utarishi wa
kifikra na kimatendo.
Kwa waraka huu mheshimiwa Rais, wakati
tukikuahidi kwa dhati kabisa wewe binafsi na Watanzania wenzetu kwamba,
tutaendelea na kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa
habari, sambamba na kuheshimu sheria zilizopo, tunapenda kuliweka hili
bayana kwamba, tutakuwa wa mwisho kuwatii viongozi dhalimu, madikteta,
waliokosa utu na ambao kwao hila ndiyo msingi mama wa kupotosha na
kupindisha mambo kwa sababu tu ya kulinda maslahi na malengo yao binafsi
au yale ya makundi yenye hila.
Rais wangu, nimeona nitakuwa mtu
nisiyekutakia mema wewe binafsi na taifa kwa ujumla, iwapo nitakaa kimya
na kuruhusu fikra za kikaburu zikijijenga vichwani mwa viongozi wetu.
Mheshimiwa Rais, tutakuwa tumeshindwa
kutimiza wajibu wetu kama wanahabari, wahariri na viongozi iwapo
tutahalalisha kwa sababu ya ukimya wetu majina mabaya tunayoitwa leo na
wateule wako kama wasaliti, wachochezi na wazushi.
Miye binafsi naamini kwa dhati kabisa
kwamba iwapo wewe utaamua kwa moyo na nia njema kulinusuru taifa letu na
majahili hao walio ndani ya Serikali yako, basi siku moja historia
itakuja kuandika kwa usahihi na ufasaha jina lako na letu..
No comments:
Post a Comment