Dar es Salaam. Chama cha Wasafirishaji
wa Mafuta Tanzania (Tatoa), kimesema Rwanda na Uganda zitajitoa kutumia
Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa Tatoa, Zacharia
Hanspope aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kukutana na Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa nchi hizo zinajitoa kutokana na
matatizo mbalimbali ambayo kwa muda mrefu zimekuwa zikiyalalamikia
lakini Serikali haikuchukua hatua.
Hanspope alisema ushuru wa barabara na
ushuru wa forodha ni baadhi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa
kwa muda mrefu na wafanyabiashara mbalimbali wa nchi hizo.
“Serikali ipunguze gharama za ushuru wa
barabara na ushuru wa forodha ili kuwa na ushindani sawa na bandari
nyingine na hivyo kuzivutia kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema
Hanspope.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary
Chambo alikataa kuzungumzia lolote kuhusu suala hilo akisema halina
mantiki yoyote kwake.... “Hivi hilo jambo unaloniuliza lina sense
(mantiki) yoyote? Mie siwezi kujibu lolote nenda ukamuulize mwenyewe
(Hanspope) maana wakati akisema mimi sikuwepo.”
Alisema kujitoa kwa Rwanda na Uganda
kuitumia Bandari ya Dar es Salaam hakutakiathiri chama hicho tu, bali
uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hayo yanatokea wakati Rwanda ikiendeleza
vita yake ya maneno na Tanzania na mfululizo wa matukio ya kuitenga
Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Viongozi wa Kenya, Rwanda
na Uganda walikutana Juni 25, mwaka huu mjini Entebbe, Uganda na
kukubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara baina yao.
Kamati ya Bajeti
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Bajeti, Andrew Chenge alisema katika kikao kijacho cha Bunge, kamati
hiyo itaibana Serikali kuhusu mikakati inayofanywa kukabiliana na
ushindani wa kibiashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema sababu ya Rwanda na Uganda
kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam ni vikwazo katika barabara
ikiwamo mizani mingi ya kupimia mizigo.
“Mizani ni mingi pia kuna usumbufu
katika kupima mizigo yao na kwamba hali hiyo inawaletea usumbufu
wafanyabiashara wengi,” alisema.
Alisema vitendo vya askari wa usalama
barabarani kudai rushwa pia ni miongoni mwa vikwazo pamoja na urasimu
mkubwa katika utoaji wa mizigo bandarini ikilinganishwa na bandari
nyingine.
“Ni lazima tujifunze kwa majirani zetu
Msumbiji, upanuzi wa haraka wa Bandari ya Beira umekuwa kikwazo kwetu,
kampuni nyingi zimeanza kuitumia bandari hiyo,” alisema.
Chenge alikitaka chama hicho kuiandikia
kamati hiyo mapendekezo yake ikiwa ni hatua ya kunusuru uchumi wa nchi
ili waweze kuijadili bungeni.
Umoja wa nchi tatu
Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul
Kagame wa Rwanda na mwenyeji wao Yoweri Museveni walikutana mjini
Kampala, Uganda na kuamua kuitumia Bandari ya Mombasa kwa shughuli zao.
Waliahidi kuimarisha ufanisi katika huduma za Bandari ya Mombasa ili kuhakikisha bidhaa zinafika mapema Uganda na Rwanda.
Pia walikubaliana kujenga reli mpya ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Mombasa kwenda Kenya na Uganda.
Viongozi hao walikubaliana pia kushirikiana katika sekta ya nishati hasa ikizingatiwa kuwa Uganda imegundua mafuta.
Nchi hizo tatu ambazo zimeruhusu kwa
raia wao kusafiri kwa vitambulisho pale wanapotembelea nchi tatu
miongoni mwao, zitakutana tena Kenya mwezi huu.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment