KWA kawaida binadamu yeyote huzaliwa na kubatizwa jina ambalo hulitumia katika masomo na hata kazi yake.
Tofauti
na ilivyo katika fani nyingine, wasanii wamekuwa wakijibatiza majina ya
ziada (a.k.a). Mbaya zaidi, majina hayo huwa yanaanza kama utani lakini
inafika wakati msanii husika
analizoea jina hilo jipya na kulifanya
kuwa kama rasmi.
Leo Amani linakuletea orodha ya baadhi ya mastaa ambao majina waliyopewa na wazazi wao ‘yamekufa’, hawayatumii kabisa:
LULU
Jina lake halisi ni Elizabeth Michael, Lulu lilizoeleka
kupitia tasnia ya uigizaji. Alianza kulitumia wakati alipojiunga na
Kundi la Sanaa la Kaole.
Hadi leo hii, siyo rahisi kabisa mtu kutokea na kumuita jina la Elizabeth, wengi wanamfahamu kwa jina la Lulu.
RAY
Ray
ndiyo jina ambalo limezoeleka na wengi. Vincent Kigosi alilopewa na
wazazi wake ni kama limekufa. Kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu
alipokuwa kwenye Kundi la Sanaa la Kaole hadi sasa.
Jina la Ray ndiyo
watu wanalolifahamu zaidi ingawa hivi karibuni baadhi ya wasanii
wenzake wamekuwa wakijaribu kumuita Vincent ili kurudisha uhai wa jina
hilo.
JOHARI
Jina lake halisi ni Blandina Chagula. Johari
lilizaliwa kwenye Tamthiliya iliyobeba taito ya jina hilo. Akiwa katika
Kundi la Kaole, alianza kujiita Blandy, baadaye alibadilisha jina hilo
na kuwa Johari walipoingiza tamthiliya hiyo ambayo pia ilizaa filamu.
“Kuna wakati huwa najuta kutumia jina la a.k.a ambalo limefunika kabisa jina langu la asili,” anasema Johari.
DK. CHENI
Ameanza
gemu kitambo, tangu Kundi la Splended. Jina alilopewa na wazazi wake
ni Mahsein Awadhi, kwa sasa limekufa. Hakuna anayelitumia, hata yeye
mwenyewe.
Jina hilo lilizaliwa baada ya mazoea yake ya kupenda kuvaa
cheni kubwa kwenye michezo iliyokuwa ikirushwa Runingani, kwa sasa wengi
wanashindwa hata kulitamka jina lake.
ODAMA
Jina lake halisi
ni Jenniffer Kyaka, limekufa kabisa kwa sasa. Wengi wanamfahamu kama
Odama jina ambalo alilipata kwenye filamu iliyoitwa Odama miaka sita
iliyopita
Tangu ilipotoka filamu hiyo hadi leo, jina la Odama limegeuka kuwa ndiyo la asili.
BATULI
Jina
alilopewa na wazazi wake ni Yobnesh Yusuf lakini wengi hawalijui.
Alianzia kuigiza katika Kundi la Kaole. Alianza kujiita Nesh, baadaye
akabadilisha na kujiita Batuli baada ya kucheza filamu ya ‘Fake Smile’
ya marehemu Steven Kanumba.
Toka hapo, watu wote wakamfahamu kupitia
jina la Batuli, wachache sana wanaolijua jina la Yobnesh, zaidi ni ndugu
zake wa karibu.
JB
Majina mengi ya a.k.a ameitwa. Aliitwa Bonge la Bwana, Mtumishi, Eric Ford na mwisho jina la JB likasimama katika akili za watu.
Mwenyewe anasema jina la JB analipenda sana, kuna wakati hata yeye huwa anasahau kabisa kama anaitwa Jacob.
NORA
Jina
lake halisi ni Nuru Nassoro. Takriban miaka kumi iliyopita baada ya
kujiunga na Kundi la Kaole, jina la Nuru limekufa kabisa.
Familia yake nzima wanatumia jina la Nora na si Nuru tena, amelikubali na analipenda kutoka moyoni mwake.
RICHIE RICHIE
Huyu naye ni msanii wa muda mrefu, jina lake halisi ni Single Mtambalike. Wengi hawalifahamu jina lake halisi.
Wanamuita
Richie Richie utadhani ndiyo alilopewa na wazazi wake, jina hilo
alipewa takriban miaka kumi na tano iliyopita akiwa na Kundi la Nyota
Ensembles.
CATHY
Huyu anaitwa Sabrina Rupia, Cathy lilikuja
katika michezo kipindi hicho akiwa katika Kundi la Nyota Ensembles.
Limeendelezwa hadi leo na kipo kizazi ambacho hakilifahamu kabisa jina
la Sabrina zaidi ya Cathy.

No comments:
Post a Comment