01 August 2013

LICHA YA USISTADUU WAO… NI WATAALAM WA MAHANJUMATI


Na Imelda Mtema

MOJA kati ya sifa kubwa ya mwanamke ni kujua kupika. Zipo baadhi ya ndoa ambazo huvunjika kutokana na tatizo la mwanamke kutojua kupika.
Kwenye ulimwengu wa mastaa wa kike Bongo, wapo wengi wanaojua kupika chakula kizuri na wapo ambao hawajui.
Kizuri huwa kinajiuza siku zote, sifa njema huwa inazungumzwa na wengi ndiyo maana ni rahisi kuwasikia hata wakisifiana wenyewe kwa wenyewe pindi wanapobaini miongoni mwao yupo anayejua kupika zaidi.
Tathmini yangu ya kina katika safari zangu za kila siku kwenye tasnia ya habari, nimeweza kujifunza kuwa wapo mastaa ambao ni hodari kwa kupika na sifa zao zimekuwa zikikua siku hadi siku.
Mara kadhaa nimeshawahi kuwasikia mastaa wa kiume kama Jacob Steven ‘JB’, Vincet Kigosi ‘Ray’ Single Mtambalike ‘Richie’ wakiwasifia baadhi ya wasanii wa kike ambao wanajua kupika vizuri.
Katika makala haya nakuletea baadhi ya mastaa ambao wanaongoza kwa kutajwa kuwa ni ‘mafundi’ wa kupika madikodiko ambapo kila mmoja ana siri yake iliyomfanya awe anajua kukaangiza:

Aunty Ezekiel
Huyu ni staa ambaye kwa muonekano wa nje anaonekana ni sistaduu anayejipenda sana na ukadhani si mtu wa kuingia jikoni au kujishughulisha na kazi zozote za nyumbani, lakini ni mtaalam wa kupika balaa.
Mwenyewe anasema alikuwa akipenda kupika tangu akiwa mdogo na alikuwa hodari wa kuwaangalia watu aliokuwa akiishi nao na kuweza kupata ujuzi wa mapishi. Ni mtaalam wa kupika chakula chochote na ukibahatika kula utadhani kimepikwa kwenye mahoteli yenye hadhi.

WEMA SEPETU
Beautiful Onyinye, Wema Sepetu ‘Madam’ ni hatari ukimkuta jikoni, anapokuwa jikoni siyo yule unayemuona kila kukicha kwenye matukio mbalimbali, anapika vyakula ambayo mara nyingi huwa ni vigumu kwa wanawake wengi  kama katles, kababu, Sambusa na vyakula vingine vingi.
Wema anasema ufundi wa jikoni aliupata kutoka kwa mama yake mzazi, Mariam ambaye mara nyingi anapata tenda kubwa za kupika vyakula sehemu mbalimbali hivyo alikuwa makini sana kuiba ujuzi wake.

MONALISA
Yvonne Cherry ni msanii wa kitambo. Siku moja nilipata bahati ya kwenda nyumbani kwao, Yombo Buza ambapo nilimkuta akiwa jikoni na alipomaliza na kukionja chakula chake nilikubali, anajua kuchanganya vitu vingi kwenye chakula na kuleta ladha ya aina yake.
Monalisa anasema kuwa ufundi huo aliupata kutoka kwa bibi yake, mama Ngatwika aliyekuwa akimfundisha namna ya kupika vyakula mbalimbali. 

JACQUELINE WOLPER
Yeye huwezi kujua kabisa kama ni mtaalam wa jikoni. Ukibahatika kumkuta jikoni basi utagundua huwa anatumia muda mwingi kuandaa chakula kitamu ndiyo maana baadhi ya wasanii wenzake wanapenda kumpigia simu na kumwambia wanakwenda kula nyumbani kwake.
Wolper anasema kuwa utaalam wa jikoni aliupata toka kwa mama yake kwani nyumbani kwao watoto wote bila kujali jinsi wanafundishwa kupika.

JOHARI
Blandina Chagula ndiyo funga kazi. Ni mtaalam balaa wa mapochopocho yote ambapo wasanii wenzake akiwemo Irene Uwoya siku zote huwa anampigia ‘saluti’ na hata zinapotokea sherehe ndogondogo yeye ndiyo hupewa nafasi ya kuwa msimazi wa kupika.
Mwenyewe anasema ujuzi huo ni kipaji alichozaliwa nacho kwani toka akiwa mdogo, alikuwa na uwezo wa kupika chakula cha kula watu wa nyumba nzima na kila mmoja akaridhika. 

Source:Global Publisher

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname