Wiki hii kwenye kolamu hii tunaye mfalme wa muziki wa Mwambao Bongo,
Mzee Yusuf ambaye anafunguka juu ya utajiri wake na skendo ya ushirikina
ambayo imekuwa ikielekezwa kwake.
Mzee Yusuf ni Mkurugenzi wa Jahazi Modern Taarab ambayo aliianzisha rasmi mwaka 2006, maskani yake yakiwa jijini Dar.Mzee Yusuf na kundi lake wamejipatia mafanikio makubwa katika medani ya muziki wa taarab na kurudisha hadhi ya muziki huo ulioanza kupoteza mvuto miaka ya 2000.
Funguka: Kwanza Mzee Yusuf unazungumziaje muziki wa taarab?
Mzee Yusuf: Zamani muziki wa taarab ulikuwa na mashabiki hasa kipindi kile cha ushindani wa marehemu Nasma Khamis na Hadija Kopa. Walijitahidi sana kuupandisha kwenye chati lakini baadaye ukapotea ila kwa sasa tumeweza kuwarudisha mashabiki wetu na muziki unapendwa Tanzania nzima, siyo Pwani pekee kama ilivyokuwa zamani.
Funguka: Inafahamika kuwa wewe ni miongoni mwa wasanii wenye mafanikio na utajiri mkubwa Bongo. Nini siri ya mafanikio yako?
Mzee Yusuf: Ni kweli mafanikio ya kundi langu yamekuwa yakiongezeka kwa kujipatia mashabiki kila kukicha. Umaarufu wake nao umekuwa ukiongezeka kila siku kwani sisi hatubagui mashabiki.
Huwa tunawafuata hadi Uswahilini kwa sababu ndiko kwenye mashabiki wengi ambao hawawezi kupanda teksi kuifuata bendi mjini. Wakati mwingine huwa tunapiga shoo za ‘ndondo’ (mtaani), harusi na sherehe mbalimbali za watu binafsi tena kwa gharama nafuu. Hiyo ndiyo siri ya mafanikio yetu.
Funguka: Vipi kuhusu skendo ya ushirikina ambayo imekuwa ikielekezwa kwako?
Umati wa watu ikiwa katika moja ya show ya Mzee yusuph
Mzee Yusuf: Ushirikina upo sana hasa katika muziki wetu huu na tena
ukiuendekeza basi utakutawala. Wengi wanaoamini kuwa hakuna mafanikio
hadi kwenda kwa waganga huwa hawafanikiwi kabisa zaidi ya kuliwa fedha
na waganga wa mjini na wengine wakishafanikiwa husahau maagano. Kwangu
mimi hayo ni maneno tu, uchawi wetu ni kujituma katika kazi.Funguka: Je, ulishawahi kwenda kwa sangoma?
Mzee Yusuf: Siwezi kusema uongo kuwa sijawahi kwenda kwa mganga, nilishawahi kwenda tena nakumbuka wakati nazindua bendi yangu ya Jahazi mwaka 2006 pale Travertine Hotel, Magomeni, Dar.
Nilikwenda kwa mganga mmoja hivi maarufu sana nikamwambia nahitaji watu wajae kwenye uzinduzi, akaniambia watakuja watu elfu moja, nikamwambia nataka watu mia saba tu kwa sababu bendi yangu bado changa.
Mganga aliniambia nimpe laki tatu, ukweli sikuwa nayo ilibidi niweke bondi tivii yangu. Baada ya wiki moja, yule mganga akaniuliza kama nimetangaza huo uzinduzi kwenye vyombo vya habari na kuweka matangazo ya barabarani, nikamjibu ndiyo ila nilijiuliza sana kwa nini aniulize wakati alinihakikishia kuwa shoo itakuwa nzuri?
Siku ya tukio ilikuwa balaa, kwanza mvua kubwa ilinyesha watu wakanyanyua viti kujikinga, watu tuliowategemea hawakuja, ukweli nilipata hasara ambayo sikuitegemea, nikagundua kuwa kwenye muziki hakuna uchawi