MSHTUKO....Padre adaiwa kupigwa Risasi huko Zanzibar!. Angalia PICHA
.Padre Ambroze Mkenda amepigwa Risasi na Watu wasiofahamika kwenye
geti la nyumbani kwake wakati akifunguliwa gate aingie nyumbani kwake
maeneo Kitomondo Mjini Zanzibar akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha
pekee yake
Yadaiwa hali yake sio nzuri kwani Risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni
Father
Ambros Mkenda wa Parokia ya Mpendae katika Kanisa Katoliki Mjini
Zanzibar amepigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake majira
ya saa 12 jioni wakati akitokea kanisani
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Juma Mohammed
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema Father amepigwa
risasi na ameumizwa sehemu ya kichwa na amekuwa akitoka damu nyingi
kichwani na tayari anapatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Mnazi
Mmoja.
Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili
kubaini wahusika walifanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni kitendo cha kihalifu na
tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki kwa hivyo bado ni mapema
kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani kwa kuwa bado uchunguzi
wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusikana na tukio
hili” alisema Kamanda.
Kamanda Aziz akisimulia tukio hilo alisema walipata taarifa majira ya
saa 2 na kwenda katika eneo la tukio ambapo Father alikuwa akitokea
kanisani na kutaka kuelekea nyumbani kwake wakati akiwa ndani ya gari
ndipo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana na kuanguka.
“Tumekuta mabaki ya risasi ndani ya gari yake na katika vioo vyake vya
gari vimevunjika na tumekuta damu chini pale” alisema Kamanda.
Aidha Kamanda Azizi alisema Father Ambros yeye ni mhasibu pale kanisani
na hivyo mara nyingi watu wananaamini kwamba katika siku za krismass
mara nyingi sadaka hukusanywa fedha nyingi na hivyo wanamini kwamba
alikuwa fedha mikononi na ndipo inawezekana waliamua kumpiga risasi
wakitaka kuchukua fedha hizo.
Hata hivyo alisema uchunguzi wa awali ndio utakaoeleza ni suala gani
lililopelekea kupigwa risasi lakini wanaendelea na uchunguzi huo ambapo
uchunguzi ndio utakaojulikana sababu kamili ya tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Askofu Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikan la
Mkunazini amesema wamesikitishwa na wamepokea kwa mshituko mkubwa tukio
hilo hasa kwa kuzingatia matukio kama hayo hayajawahi kutokea ya
kuwahujumu viongozi wa dini.
Alisema tukio hilo ni miongoni mwa matukio ya kushtusha na yanaashiria
hali mbaya ya kiusalama na kuwaomba viongozi wa serikali kuchukua hatua
za tahadhari kubwa kwani matukio kama hayo yameanza kutokea kwa viongozi
wa dini ambapo mwanzo ilianzia kwa Sheikh Soraga na baadae kutokea kwa
Father Ambros.
“ Hii ni hali ya hatari katika nchi yetu na haipendezi lakini serikali
lazima ijue sisi hatuwezi kujua wala hatuwezi kujilinda lakini serikali
inapaswa kutulinda sisi ndio wananchi wake” alisema Askofu Hafidh.
Askofu Hafidh alisema hivi karibuni kumekuwepo vipeperushi
vilivyosambazwa na watu vikiwatisha watu wenye imani ya kikristo ambapo
alisema miongoni mwao walikuwa na khofu juu ya kusambazwa kwa
vipeperushi hivyo na kuiomba serikali iongeze ulinzi.
“Tumeona hivi vipeperushi na kwa kweli tulikuwa na khofu juu ya
vipeperushi hivi lakini ndio tunasema tunaelekea wapi katika maisha
haya” alisema Akofu Hafidh.
“Sisi hatuamini kwamba kuna kisasi kwa viongozi wa dini lakini
tunachukulia hilo ni tukio la kihalifu na pia hatuna vipeperushi vya
aina yoyote vinavyoelezea kuwatisha viongozi wa dini kwa hivyo
tunachukulia hayo ni matukio ya kihalifu na wala hatuamini kwamba
matukio haya ni ya dini fulani” alisema Kamanda Azizi.
Akielezea kuhusiana na hilo Kamanda Aziz alisema jeshi la polisi
limejipanga na kuzidisha ulinzi katika maeneo yote ya makanisa ambapo
kumesambazwa polisi wa kutosha kwa kuwa wanajua wakati wa sherehe mambo
ya kihalifu hujitokeza.
“Sisi kawaida huwa tunaweka ulinzi siku za sherehe zozote lakini kwanza
makanisa yote yamewekwa ulinzi wa kutosha kabisa lakini wahalifu
wanapotaka kufanya uhalifu huwezi kujua watatumia mbinu gani na saa
ngapi na watafanya uhalifu huo wapi, lakini ulinzi upo wa kutosha”
alisisitiza Kamanda Aziz.
source-jamiiforums