17 January 2016

RPC AKATIWA HUDUMA YA MAJI NYUMBANI KWAKE MOSHI




Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru      
Ni kutokana na malimbikizo ya madai ya miaka saba ambazo taasisi za umma zinadaiwa.
Moshi. Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Moshi (Muwsa), imekata maji katika makazi ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro na makambi ya askari polisi mkoani hapa.
Muwsa iliamua kuanza operesheni ya kuzikatia maji taasisi tatu nyeti za Serikali likiwamo Jeshi la Polisi, ambazo kwa pamoja zinadaiwa malimbikizo ya zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa miaka saba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muwsa, Joyce Msiru alisema jana kuwa hadi kufikia saa nne asubuhi, walikuwa wamekata maji kwenye nyumba za polisi.
Maeneo yaliyokatiwa maji ni kambi kuu ya polisi iliyopo Kiusa na nyumba za maofisa wa jeshi hilo zilizopo eneo la Msaranga.
Katika malimbikizo hayo ya madeni, ofisi ya RPC Kilimanjaro inadaiwa Sh528.6 milioni, Chuo cha Mafunzo ya Polisi (MPA) Sh401.9 milioni na Magereza Sh203.7 milioni.
Alipoulizwa kuhusu kukatiwa maji, RPC wa Kilimanjaro, Ramadhan Mungu alisema hakuwa na taarifa hizo kwa vile tangu asubuhi alikuwa msibani Marangu, Moshi Vijijini.
Baadaye Mungi alisema asingeweza kuzungumzia kwa kina suala hilo lakini akasisitiza kuwa inayodaiwa fedha hizo ni Serikali kupitia Idara ya Polisi.
Hata hivyo, Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alisema: “Nimepokea malalamiko ya askari kuwa kambini hakuna maji tangu asubuhi ndiyo nafuatilia kujua tatizo liko wapi. Sina hakika kama Muwsa wamekata au kuna tatizo jingine.”
Wiki mbili zilizopita, Msiru alisema wametoa notisi kwa taasisi hizo kulipa malimbikizo ambayo alisema yameathiri mipango ya Muwsa ikiwamo kuboresha huduma.
Alisema juhudi nyingi zimefanyika kufuatilia madeni hayo lakini Serikali imekuwa hailipi, ingawa mwaka jana walianza kulipa madeni kabla ya kusitisha.
“Tunajiuliza hii mamlaka itajiendeshaje wakati fedha zote zimeshikiliwa na taasisi hizo? Februari 28, 2015, bodi ya wakurugenzi ilikutana na uongozi wa MPA lakini imeonekana siyo walipaji,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika vikao hivyo, ilibainika kuwa Hazina ndiyo inayostahili kulipa malimbikizo hayo lakini hakuna mwanga wa kulipwa.
“Tuna miradi mingi ya kutekeleza ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha. Fedha za miradi hiyo tunazo lakini zimeshikiliwa na taasisi za Serikali,” alisema Msiru.
Mkuu wa MPA, Matanga Mbushi alisema wanaowajibika kulipa ni Hazina na wameshaandika barua ya kukumbushia.
Mkuu wa Magereza Mkoa Kilimanjaro, Venant Kayombo alisema kinachodaiwa siyo malimbikizo ya maji pekee, bali pia bili ya umeme na kwamba fedha kidogo zilizokuwa zikitumwa na Serikali zilikuwa zikilipwa kwa taasisi hizo.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname