Utangulizi
Mwezi Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji
wa kawaida wa shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na
hasara itokanayo na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa
viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika
muda mfupi.
Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo.
Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu
chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31
cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo
mengine walibaini miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya
kitanzania ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA).
Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji
wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa
sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania
Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger).
Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic.
Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani
milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda
mfupi kwa njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za
kibenki.
Taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic
kwa mujibu wa taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya
benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo
cha Financial Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na
Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA
kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The
Anti-Money Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic
ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa
shaka.
Mnamo 29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara
ya Serikali ya Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi
na Rushwa (Serious Fraud Office - SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya
kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya
Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania
Limited katika kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa
Serikali na kwamba ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma.
Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za
Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika, hata
hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti
hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye, Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa
faini ya jumla ya dola za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha
dola za kimarekani milioni 7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za
kimarekani milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1
ni riba).
Kwa kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha
EGMA na pia kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa
kuzingatia Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka
2006, Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3.
Sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika
kipindi cha siku ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari 2016.
Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika
kulipa faini hiyo.
Hitimisho
Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya
Stanbic na ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake
zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha, hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha
zisijihusishe na makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za
kibenki na ni uvunjaji wa Sheria za nchi.
Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya
fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na
Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
No comments:
Post a Comment