29 January 2016
Chadema wadai wako tayari kuchangisha fedha kuilipa TBC irushe Bunge lote 'Live'
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kiko tayari kuzunguka nchi nzima kuchangisha fedha kwa ajili ya kulilipa Shirika la Habari Nchini (TBC) gharama za kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vyote vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari akipinga sababu zilizotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuhusu uamuzi wa TBC kutorusha ‘Live’ vikao vyote vyote Bunge bali kurusha ‘Live’ baadhi ya sehemu ya vikao hivyo.
Nape alieleza kuwa serikali imechukua uamuzi huo kwa lengo la kubana matumizi kwa kuwa TBC imekuwa ikitumia shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya Bunge.
“Watafute namna gani ya kuweza ku-mobilize fedha ili ilipwe TBC au Taifa litafute Channel nyingine za kuweza kurusha matangazo hayo. Na Chadema tuko tayari kusaidia hilo. Tuko tayari kuhamasisha Watanzania mwenye shilingi moja, shilingi mbili au tatu atoe tuilipe TBC ili Bunge lirushwe moja kwa moja,” alisema Mwalimu.
Katika hatua nyingine, Mwalimu alionesha kutokubaliana na hesabu za shilingi bilioni 4.2 zilizotajwa na Waziri Nape kuwa gharama za kurusha matangazo ya Bunge ‘Live’ kwa TBC.
“Mimi nimekuwa mwandishi wa habari na nimefanya kazi kwenye TV. Kila nikichambua shilingi 4.2 bilion kwa ajili ya kurusha Bunge katika muda ambao sio ‘prime’… yaani kila nikipitia rate zote za Televisheni, sioni hiyo 4.2 bilioni zinapatikanaje,” aliongeza.
Wabunge wa upinzani leo pia walitoka nje ya Bunge hilo kushinikiza serikali kubadili tangazo lake kuhusu TBC na vikao vya bunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment