Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru amezitaka taasisi na mashirika ya
umma nchini kuacha utegemezi kwa Serikali, badala yake kupunguza
matumizi na wafanyakazi ili kuongeza mapato na ufanisi.
Mafuru alisema Serikali imebeba mzigo wa taasisi na mashirika hayo kwa
kutegemea izipatia fedha kutoka Hazina kwa ajili ya kujiendesha, na
kulipa mishahara ya wafanyakazi na kusababisha ufanisi wao kuwa mdogo.
Mafuru pia alitangaza kufuta posho za wabunge katika bodi za mashirika
na kuanzisha mchakato wa kuwaondoa katika mashirika hayo, ili wabaki na
jukumu lao la msingi la kuikosoa Serikali badala ya kuingia katika
utendaji.
Kuhusu uzalishaji
Msajili huyo alisema inashangaza kuona kwamba mpaka sasa kuna mashirika
ya umma ambayo bado yanaitegemea Serikali kulipa mishahara ya
wafanyakazi wake.
Aliyataja mashirika hayo kuwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kampuni ya Hifadhi za Reli (RAHCO) na
Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara).
Alisema hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuwa na mizigo hiyo isiyozalisha ikiwamo kubeba gharama za kuendesha mashirika hayo.
“Wenyeviti na wajumbe wa bodi, pamoja na watendaji wakuu wa kila shirika
mkae chini mjitafakari, kwa nini muendelee kuongoza mashirika hayo
wakati mmeshindwa kuzalisha. Rais ameniagiza kuwakumbusha kwamba mrejee
malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zenu,” alisema.
Mafuru alisema taasisi ambazo uzalishaji wake umeshuka lakini gharama za
uendeshaji ziko juu, hazina budi kupunguza wafanyakazi ili kulingana na
mapato yake.
“Kama hawataweza kufanya hivyo, watafute njia nyingine ya kuongeza
uzalishaji kwa kutumia wafanyakazi walionao. Kwenye sekta binafsi,
kampuni ikianza kufanya vibaya inapunguza matumizi yake na moja ya njia
wanazotumia ni kupunguza wafanyakazi. Huku serikalini utasikia mtendaji
mkuu akiandika barua, siyo proposal (mradi), kuomba fedha kwa ajili ya
mtaji. Hatuwezi kwenda mbele,” alisema.
Mafuru aliyasema hayo jana katika mkutano maalumu ulioitishwa kwa
maagizo ya Rais John Magufuli ili kuwakumbusha watendaji mbalimbali wa
taasisi na mashirika ya umma nchini, juu ya wajibu wao katika
kuwahudumia wananchi.
Mkutano huo uliwahusisha wenyeviti wa bodi, wajumbe wa bodi na watendaji
wa taasisi na mashirika mbalimbali ya umma ambayo kwa sasa yamefika
216, yakiwa na mali zenye thamani ya Sh20 trilioni.
Hata hivyo, alisema pamoja na mtaji huo, taasisi na mashirika ya umma yamekuwa yakichangia Sh185 bilioni kwenye Pato la Taifa.
“Kwa mtaji wa Sh20 trilioni, hicho ni kiasi kidogo sana ambacho kinarudi
serikalini. Kwa wenzetu wa sekta binafsi, ukimpatia mtaji huo basi
baada ya muda fulani unamkuta kapata mara mbili ya mtaji aliopewa,”
alisema Mafuru ambaye amefanya kazi kwenye taasisi za benki kwa miaka
15.
Alisema Rais Magufuli amemtuma kuwakumbusha kila mmoja kwenye taasisi
yake ahakikishe anapunguza kero zote zinazopatikana kwa kutumia
rasilimali alizonazo.
Alisisitiza kuwa kila mmoja atambue kwamba anawajibika katika kuleta maendeleo ya Taifa hili.
Msajili huyo aliongeza kuwa Serikali imekuwa hainufaiki na mashirika ya
umma ambayo ndiyo yangekuwa msaada mkubwa wa kupunguza mikopo ambayo
inadaiwa.
Hata hivyo, alisema mashirika yamekuwa yakiiacha kulipa madeni hayo licha ya kwamba yanapata faida kubwa kila mwaka.
“Siyo lazima faida inayopatika kwenye taasisi na mashirika ya umma irudi
serikalini, lakini mashirika yenyewe yanaweza kusaidia katika shughuli
mbalimbali za maendeleo ambazo Serikali ilitakiwa kufanya” alisema.
Mafuru alitoa mfano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akisema
linapopata faida kubwa, linaweza kuamua kujenga kipande cha reli kutoka
Dar es Salaam mpaka Morogoro na kuisaidia TRL na Serikali.
Wabunge kutopewa posho
Mafuru alisema wabunge ambao ni wajumbe wa bodi za mashirika hayo,
hawatalipwa posho za vikao vya bodi kwa sababu wanalipwa posho hizo
kwenye kamati zao.
Alisema kuendelea kufanya hivyo ni sawa na kuwalipa posho mara mbili kwa kazi moja, jambo ambalo halikubaliki.
Alisema kuna mpango wa kuwaondoa wabunge kwenye bodi hizo ili washiriki
kikamilifu kuisimamia Serikali na kwamba mbunge anapokuwa sehemu ya bodi
anakosa uhuru wa kufanya kazi yake kama mwakilishi wa wananchi.
“Shirika linapofanya vibaya wajumbe wote wa bodi wanahusika bila kujali
ni mbunge au la. Kuna mbunge mmoja alipata msukosuko wakati wa sakata ya
Tanesco, kwa hiyo tunajaribu kuwalinda ili wafanye kazi yao
kikamilifu,” alisema.
Kuhusu uteuzi wa wenyeviti wa bodi, Mafuru alisema Rais anawateua kwa
sababu anaamini wana uwezo wa kusimamia na kuongoza bodi hizo ili kuleta
matokeo chanya.
Alisema wenyeviti wengi wamekuwa wakichukulia nafasi wanazopewa kama
zawadi na kushindwa kusimamia majukumu ya mashirika au taasisi husika.
Alisisitiza kuwa uenyekiti ni jukumu kubwa ambalo linahitaji kuifahamu taasisi vizuri ili kutoa maamuzi sahihi.
Aliwataka wenyeviti wa mashirika ya umma kutambua wajibu wao na kuondokana na dhana kwamba wanapoteuliwa basi wanapewa ‘ulaji’.
Kwa upande mwingine aliyataka mashirika hayo kufanya ukaguzi wa hesabu zao na kuwasilisha ripoti katika ofisi yake.
Akitoa maoni yake kuhusu uendeshaji wa mashirika ya umma, Mkuu wa
Taasisi ya UsiMamizi wa Fedha (IFM), Profesa Emmanuel Mjema, alisema
Wakala wa Manunuzi ya Serikali (GPSA) amekuwa tatizo ambalo linapaswa
kuangaliwa. Pia, alisema Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa),
nao wamekuwa ni tatizo kwa kutopeleka magari kwa ajili ya kufanyiwa
matengenezo huku wakitoza fedha, lakini wanaambiwa wapeleke magari hayo
GS Motors.
Mafuru alisema amepokea maoni hayo na kuongeza kuwa ofisi yake imekuwa
ikipata malalamiko kutoka mashirika mbalimbali kuhusu GPSA na kuahidi
kufuatilia na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Albina Chuwa alitaka
mishahara ya watendaji wa taasisi na mashirika ya umma iangaliwe upya
kwa sababu wapo wanaopata mikubwa kiasi cha Sh36 milioni wakati wengine
wanapokea Sh3 milioni.
No comments:
Post a Comment