Wakati mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa
mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar yakiwa yamepamba moto, uamuzi wa
kufutwa matokeo ya uchaguzi umetangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali
la Novemba 6,
mwaka huu, hivyo kumaanisha uchaguzi huo sasa ni rasmi
utarudiwa.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, uamuzi huo umechapwa chini ya kifungu 119 (10) na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya Mwaka 1984.
Gazeti hilo pia limetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 3(1) na 5(a) vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Aidha gazeti hilo la serikali limeeleza kuwa, matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu yamefutwa kuanzia Oktoba 25, mwaka huu.
Kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Uchaguzi
kinasema: “Kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo tume ina mamlaka ya
kutunga au kutoa, itajaaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria
kama yametiwa sahihi na Mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi.”
“Mimi Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 119
(10) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa vifungu vya
391) na 5 (a) vya Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, natangaza
uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo yote ya Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25, Oktoba,” gazeti hilo la serikali
lilieleza.
Tangazo hilo kwenye Gazeti la Serikali
limetiwa saini na Mwenyekiti wa Zec Oktoba 28 mwaka huu na kwa msingi
huo wananchi wa Zanzibar watatakiwa kuingia tena katika uchaguzi ndani
ya siku 90.
Kabla ya kuchapwa kwa gazeti hilo,
wajumbe saba wa Zec walikutana na kujadili kufutwa matokeo ya Uchaguzi
Mkuu lakini kulitokea mvutano mkubwa kabla ya kuamuliwa kwa kutumia
akidi ya wajumbe wengi waliounga mkono. Katika kikao hicho, wajumbe wanne
waliunga mkono uchaguzi kufutwa na wajumbe watatu walipinga kufutwa kwa
matokeo ya uchaguzi huo, akiwamo Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Jaji Abdularhakim Issa Ameir.
Wajumbe wengine waliopinga matokeo
kufutwa ni, Ayub Bakar (CUF) na Nassor Khamis (CUF) na wajumbe waliounga
mkono walikua ni, Omar Ramadhan Mapuri (CCM), Salmin Senga (CCM) na
Haji Ramadhan (SAU).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mohamed Aboud, alisema baada ya tume kuchapa Gazeti la Serikali
juu ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu, kinachosubiriwa ni tume
kutangaza tarehe ya uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humo.
Alisema serikali itahakikisha uchaguzi
huo unafanyika kwa wakati kwa kuzingatia sheria na katiba ili wananchi
wapate haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wao kwa haki na utaratibu
wa kidemokrasia.
Alisema serikali imeanza kujipanga katika
matayarisho ya gharama za uchaguzi huo, ikiwamo utoaji wa elimu ya
uraia kwa wananchi kabla ya kufanyika. Hata hivyo, Kiongozi Mwandamizi wa
Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Janeti Fussi, alisema
umoja huo haukubaliani na uamuzi wa kurudiwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
“Tunamtaka Mwenyekiti wa Zec arudi kazini
akamilishe uchaguzi wa Oktoba 25 na kumtangaza mshindi wa uchaguzi
huo,” alisema Fussi ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kampeni
wa Cuf, Ismail Jussa, alisema Mwenyekiti wa Zec katika Gazeti la
Serikali ameshindwa kuonyesha kifungu cha katiba au sheria kinachompa
uwezo wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu.
Alisema kifungu cha katiba namba 119 (10)
cha Katiba ya Zanzibar alichokitumia kinazungumzia kiwango cha mikutano
ya tume na kila uamuzi lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi na
siyo kufuta matokeo ya uchaguzi.
Alisema msimamo wa Cuf upo palepale Zec
itengue uamuzi wa mwenyekiti wake warudi kazini kukamilisha utaratibu wa
kuhakiki na kutangaza matokeo ya majimbo yaliyobakia na kumtangaza
mshindi wa uchaguzi huo.
Gazeti la Serikali la kufuta matokeo ya
Uchaguzi Mkuu limetoka wakati viongozi wakuu wa Zanzibar wakiendelea na
mazungumzo ya kusaka ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi huo, akiwamo Rais
Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) na mgombea mwenzake kupitia Cuf, Maalim Seif
Sharif Hamad ambaye anadai yeye ndiyo mshindi kabla ya matokeo kufutwa.
Chanzo: Nipashe

No comments:
Post a Comment