Dar es Salaam. Mwandishi wa Mwananchi, Tumaini Msowoya
jana alipigwa ngumi kadhaa kichwani na mwalimu wa Shule ya Sekondari
Kitunda wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.
Msowoya alipigwa na mwalimu aliyefahamika kwa jina la Willibroad Samson
alipokwenda shuleni hapo kufuatilia madai kwamba baadhi ya wanafunzi wa
shule hiyo, wiki iliyopita waliandikishwa na kupewa vitambulisho vya
kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Msowoya alisema kwamba tukio
hilo lilitokea kati ya saa 4.30 na saa 5.00 asubuhi karibu na jengo la
ofisi za walimu. “Nilifika shuleni pale saa 3.00 asubuhi kwa ajili ya
kuonana na mkuu wa shule, sikumkuta ila nilipokewa na makamu mkuu wa
shule. Lakini wakati nikiendelea na mazungumzo ofisini kwa mwalimu huyo
tulisikia wanafunzi wakipiga kelele,” anasema Msowoya.
Alisema kuwa alipotaka kutoka nje baada ya kukamilisha mazungumzo na
makamu mkuu wa shule alisikia kelele zikipigwa huku mawe yakirushwa na
kupiga jengo la ofisi ya walimu wa shule hiyo. “Hivyo tukaufunga mlango
na baada ya muda mfupi nilitoka nje na kushuhudia wanafunzi wawili
wakipigana huku wenzao wakishangilia,” alisema.
Kwa mujibu wa Msowoya, alianza kupiga picha za tukio hilo, na punde
alimwona mwalimu Samson akiamulia wanafunzi waliokuwa wanagombana. Pia,
alimwona mwalimu huyo akimdhibiti Elia Simion, mmoja wa wanafunzi wa
kidato cha kwanza waliokuwa wanapigana huku akitoka damu mdomoni baada
ya kupigwa na mwenzake.
Katika tafrani hiyo, Msowoya alisema mwalimu huyo alimpiga huku
akimvutia katika ofisi ya walimu, lakini walimu wengine waliingilia kati
kumzuia.
Kutokana na kipigo hicho, alitoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kitunda
ambako alipewa fomu ya PF3, kisha akapatibiwa katika Zahanati ya
Kitunda.
Alipoulizwa makamu mkuu wa shule aliyejitambulisha kwa jina moja la
Masatu kuhusiana na tukio hilo alikiri kushuhudia lakini akasema mwalimu
aliyefanya tukio hilo anajitolea kufundisha, siyo mwajiriwa wao.
Mwalimu Samson alipoulizwa sababu za kumpiga mwandishi alisema kuwa
alikasirishwa na kitendo cha kupigwa picha wakati akiamulia ugomvi wa
wanafunzi. Hata hivyo, kuhusu madai kwamba wanafunzi waliandikishwa na
kupewa vitambulisho kwa ajili ya kupiga kura, Masatu alikanusha akidai
wanafunzi walipigwa na kupewa vitambulisho vya shule ambavyo mpigaji ni
mtu binafsi.
No comments:
Post a Comment