Shani Ramadhani
RIP! Kijana
aliyefahamika kwa jina la Shelitiael Steven Mbise, aliyekuwa akisoma
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) amefariki dunia kwa kuchomwa kisu na muuza
chipsi kufuatia kutofautiana.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Dodoma, denti huyo alikuwa akichukua masters akiwa kwenye mwaka wake wa kwanza.
“Marehemu alikuwa amepanga chumba nje ya
chuo, Mtaa wa Chako ni Chako lakini kipindi hiki chuo kimefungwa
alikuwa hapa na mara nyingi alikuwa akionekana yuko bize na masomo kwani
alikuwa akienda chuoni na kurudi.
“Kuna sehemu alishawahi kupanga chumba
na rafiki yake lakini baadaye akahama na kwenda kupanga chumba chake
mwenyewe,” kilieleza chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina.
Chanzo kiliendelea kuweka wazi kuwa siku
ya tukio, Alhamisi ya Septemba 10, mwaka huu Mbise alikwenda kwenye
chipsi ambapo ni jirani na anapoishi. Ndipo kukatokea mgogoro
ulisababisha muuza chipsi kumchoma kisu.
“Kulikuwa na ugomvi kati ya marehemu na
muuza chipsi. Sasa mashuhuda wanadai, msomi huyo aliomba chenji yake
baada ya kula, muuza chipsi akasema hajalipa na akamtaka alipe.
Wakazozana, mwishowe msomi aliamua kuondoka, ndipo mtu wa chipsi
akamfuata kwa nyuma na kumchoma kisu sehemu ya juu ya mgongo. Mbise
alianguka na kupoteza maisha palepale huku mtuhumiwa akishikiliwa,”
kilisema chanzo.
Kikaendelea: “Baada ya hapo, taarifa
ziliufikia uongozi wa chuo na mwili ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali
ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya uchunguzi na kisha Ijumaa usiku
ulisafirishwa kwao jijini Arusha.”
Kupitia simu ya mkononi, mwandishi wetu
alimpigia afisa habari wa chuo hicho ambaye alijitambulisha kwa jina
moja la Beatrice. Yeye alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi
huyo akisema:
“Ni kweli yule alikuwa mwanafunzi wetu
wa mwaka wa kwanza na kipindi hiki chuo kimefungwa lakini yeye alikuwa
maeneo ya jirani na chuo kwa ajili ya kuonana na supavaiza wake.
“Siku ya tukio marehemu alikuwa akienda
mjini, akapita sehemu wanayouza chipsi kwa ajili ya kupata chakula ndipo
ukatokea ugomvi uliosababisha yeye kuchomwa kisu lakini kesi tayari ipo
polisi na yule mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi
Dodoma.
Mwili wa Steven Mbise ulihifadhiwa kaburini Jumamosi iliyopita. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina
No comments:
Post a Comment