24 September 2015
Mastaa Kuhama Ukawa Kwenda CCM, Siri Nzito Yafichuka
NYUMA ya wimbi kubwa la mastaa waliokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuna siri nzito zilizojificha na Amani limechimbua kutoka kwa wahusika.
Hivi karibuni, mastaa mbalimbali akiwemo mwigizaji Aunt Ezekiel na Vincent Kigosi ‘Ray’ waliokuwa wakishabikia Chadema kinachoungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitangaza kuhamia CCM na kuzua taharuki kwa wafuasi wao.
Baada ya wawili hao kuhamia CCM, yaliibuka madai kuwa wamehongwa mamilioni ya shilingi ili waachane na Ukawa na wahamie CCM.
“Hawana lolote tunajua wamehongwa fedha na CCM ili waikane Ukawa, njaa hizi zitatuua jamani,” yalisomeka madai hayo katika mitandao mbalimbali.
Mwanahabari wetu baada ya kushuhudia madai hayo yakizidi kusambaa mitandaoni, kwa nyakati tofauti aliwapigia simu Ray na Aunt ambao kwa pamoja waliyakana na kuwataka Watanzania kusikia siri iliyowafanya wao kushtuka na kuhamia CCM.
“Jamani niwaambie ukweli, sijahongwa na chama chochote. Nimetafakari kwa makini na kuamua kuhamia CCM kutokana na ukweli ndiyo chama kilichotufikisha hapa tulipo na kinachoweza kutufikisha mbali zaidi.
“Ninawashangaa wanaozungumzia kuwa tumehongwa ili tuhamie CCM, mbona hawasemi Edward Lowassa na Fredrick Sumaye (mawaziri wa zamani-CCM) wamehongwa kuhamia Ukawa?
“Nisiwafiche, nafsi ilikuwa inanisuta sana kuwa Ukawa. CCM ndiyo kila kitu, maendeleo ya kweli yanaletwa na mtu anayezungumza sera na kumaanisha kile anachozungumza, CCM wamesimamisha mgombea ambaye hata kama wewe ni mpinzani utakubali tu ni mchapakazi.
“Niwasihi vijana wenzangu kujitambua, kusikiliza sera za wagombea wote na kufanya uamuzi sahihi, wasisukumwe na mhemko tu inayohusishwa na mabadiliko. Wampime mgombea anayehubiri mabadiliko anamaanisha?”
Kwa upande wake Aunt alisema: “Kwanza nikatae sijapewa hata shilingi na CCM. Kilichonihamisha Ukawa ni sera na Ilani. Sera na Ilani ya Chadema haizungumzi moja kwa moja kumkomboa Mtanzania wa hali ya chini.
“Wanahubiri mabadiliko tu bila kueleza watayaletaje? Busara wala kusisitiza amani hakuna. CCM ina sera na Ilani inayotekelezeka. Nimeilewa ndiyo maana nikaamua kuunga mkono. CCM ina viongozi waadilifu, wenye hofu ya Mungu, wasiokuwa na tamaa ya madaraka tofauti na wale wa Ukawa.
“Niwaase vijana na Watanzania wote ambao bado hawajashtuka, washtuke na kuja CCM ambako kunaeleweka.”
Chanzo: GPL
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment