Afisa Mtendaji Mkuu wa EAG Group Imani kajula Akiwa Pamoja na Rais Wa Simba Sport Club Evans Aveva wakati wa Uzinduzi wa Simba Day
Dhima ya Simba Sports Club ya kuendeleza mabadiliko ndani ya Simba bado inaendelea kushika kasi, Katika kipindi cha miezi mitatu sasa, mmekuwa mashuhuda wa Simba inayolenga kuleta mapinduzi makubwa katika jinsi mpira unavyoendeshwa, kujali wanachama, wapenzi wake na kukuza vyanzo vya mapato.Akizungumza wakati wa kutangaza rasmi Simba Week 2015 Rais wa Simba Evans Aveva alisema ‘’Kila mwaka timu yetu ya Simba imekuwa na utaratibu wa kuwa na siku maalum kwa ajili ya kufurahi, kuwatambulisha rasmi wachezaji, jezi za timu na kujiandaa kwa msimu mpya, siku hii imekuwa maarufu kama Simba Day. Tangu ianzishwe imekua ikiboreka siku hadi siku, mwaka huu tumeona ni muhimu kuiboresha zaidi na hususani kuangalia mchango wa timu yetu kwa jamii inayoizunguka’’.
Aliongeza kusema ‘’Hivyo basi mwaka huu tunaanzisha Simba Week ambayo lengo lake kuu ni kuwa wiki ya Simba Sports Club kufanya kazi za jamii, kukuza vipaji vya soka vya vijana, kutembelea wadau wa maendeleo na pia shughuli nyingine zenye tija kwa timu yetu na jamii kwa ujumla. Wiki hii itahitimishwa siku ya Simba Day ambapo mambo mengi mazuri yatafanyika. Tofauti na miaka mingine, tutatengeneza program ambayo itawashirikisha wana Simba Nchi nzima.
Tunategemea kuwa na siku za kujitolea kwa jamii, wapenzi wote wa Simba Nchi nzima watajitokeza kufanya shughuli za kijamii kwenye maeneo yao. Simba inaamini kwa dhati tukiunganisha Nguvu zetu tunaweza kuleta madabiliko makubwa sana Nchini kwetu’’.
Pia Rais huyo wa simba Alisema, Napenda kuwataarifu rasmi kuwa siku ya Simba Day, Simba Sports Club itacheza mechi na AFC Leopards ya Kenya kwenye mechi hii wachezaji wetu wapya wataonekana rasmi baada ya maandalizi ya kutosha, kabla ya mechi hii kutakuwa na mechi kali ya utangulizi kati ya Viongozi wa Simba na Bongo movie ambao watachanganyika na Bongo Flava, mechi hii nina uhakika itakuwa burudani tosha. Jambo jema na jipya ni kuwa Kiingilio cha siku hii ni BURE!. BURE kwa wanachama wa Simba ambao watakuwa na kadi mpya za Simba hivyo nawaomba wanachama wachangamkie fursa hii kwa kuchukua kadi mpya!. Simba itaendelea kujali wanachama wake mara zote!
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa EAG Group amabo ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Imani Kajula alisema ‘’ Siku ya Simba Day jezi mpya za Simba zitaanza kuuzwa rasmi, napenda kutumia jukwaa hili kutahadharisha wauza jezi feki kuwa mkono wa dora utawafikia.
Kwa wale wanaotaka kuwa mawakala au wauzaji wa jezi za Simba milango iko wazi wawasiliane nasi kwa anuani zilizopo kwenye tovuti ya klabu www.simbasports.co.tz au kufika kwenye klabu ya Simba. Pia wapenzi wanaotaka kuwa wanachama wanaweza kujiunga kupitia tovuti ya klabu na mawakala kwani kwa kuwa mwanachama wa Simba Sports Club mwanachama anapata faida nyingi ikiwemo bima ya maisha hadi 250,000 ikiwa mwanachama atafiwa na mwenza, mtoto au yeye mwenyewe akifariki’’
No comments:
Post a Comment