Hali
imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Ester Bulaya,
kutangaza kukitosa kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa
tiketi ya chama hicho.
Bulaya
ambaye alikuwa mbunge machachari kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni , ametangaza
kutogombea ubunge kupitia CCM wakati akizungumza baada ya kazi ya
kuchukua fomu ndani ya chama hicho na kurejesha kuhitimishwa rasmi
nchini jana.
Tangu
mwanzo mwa mwaka huu, Bulaya alitangaza kugombea ubunge katika Jimbo la
Bunda kupambana na Mbunge aliyemaliza muda wake ambaye ni Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Bulaya
amekuwa kada wa pili ambaye alikuwa mbunge kutangaza kutogombea ubunge
kwa tiketi ya CCM, mbunge wa kwanza kutangaza kutogombea ubunge kupitia
CCM baada ya James Lembeli, ambaye alikuwa Mbunge wa Kahama.
Hata
hivyo, Bulaya hakuweka wazi kama ana mpango wa kuhamia chama kingine
cha siasa na kutimiza azma yake ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu
wa mwaka huu.
Ingawa
Bulaya hajaweka wazi, vyama ambavyo vimekuwa vikitajwa kusubiri makada
kutoka CCM kujiunga navyo ili wawanie ubunge ni Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (Cuf).
Wakati
ikiwa hivyo kwa Bulaya, hali bado si shwari ndani ya CCM Wilaya ya
Monduli baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Edward
Sapunyo, Kupigilia msumari wa mwisho na kubariki hatua ya madiwani wake
20 kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Sapunyo
ambaye alikuwa Diwani wa kata ya Moita, alisema madiwani wake hawawezi
kusubiri hadi Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa,atoe kauli kuhusu hatma yake ya kisiasa ndani ya CCM.
Kauli
ya Sapunyo ambaye hatagombea udiwani uchaguzi wa mwaka huu, imekuja
siku moja baada ya madiwani 20 wa jimbo hilo kutangaza rasmi kukihama
chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Hatuwezi
kuona baba yetu anapigwa na kuanguka chini halafu tusubiri kauli yake,
ni lazima tuchukue hatua mara moja…hii haivumiliki, kitendo
alichofanyiwa (Lowassa) na vikao vya CCM mjini Dodoma hivi karibuni kwa
kukata jina lake pasipo kumpa haki ya kumsikiliza siyo cha
kidemokrasia,” alisema.
Lowassa
na makada wenzake wa CCM 38 walichukua fomu ya kuomba ridhaa ya
kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya kuwania kiti cha urais
katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Katika
kinyanyang’anyiro hicho, jina la Lowassa na wenzake yalikatwa katika
hatua ya mwanzo, hali ambayo imezua malalamiko kwamba ikidaiwa kuwa
hawakupewa nafasi ya kuhojiwa.
“Tumepigwa,
tumesambaratika (CCM) Monduli, hatuwezi kuchukua fomu za kuomba
kugombea au kutetea nafasi zetu ndani ya chama hiki, tumehamia Chadema,”
alisema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alidai kuwa siyo kweli kwamba madiwani wote wamekihama chama chao.
Kimaro alidai kuwa baadhi ya madiwani waliotangaza kukihama chama hicho wameanza kusalitiana.
Alisema
madiwani hao ambao anawaita ni makada baada ya Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Monduli kuvunjwa, walifanya mkutano kwa kushawishiwa na
mmoja wao.
Alisema
ushawishi huo unatokana na uchu wa madaraka alionao kwa kuwa tayari
wananchi wa Jimbo la Monduli, wanapenda aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum
CCM, Namelok Sokoine, kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo.
Alisema
kutokana na ugumu huo, diwani huyo wa zamani ametumia mbinu ya
kuwarubuni wenzake wakihame chama hicho ili agombea ubunge kwa tiketi ya
Chadema.
“Huo ni uchu wa madaraka aliyo nayo,” alisema na kuongeza: “Diwani huyo hakubaliki na wananchi wa kata yake.”
Alidai
kabla ya kutangaza kukihakama chama hicho, madiwani hao walikuwa
wameshafanya kikao na kuweka azimio la pamoja la kuondoka CCM, lakini
juzi walipotangaza uamuzi wao, walijikuta wapo madiwani watatu.
Alisema
baadhi ya madiwani walimfuata ofisini kwa lengo la kumuomba radhi
lakini yeye aliwaambia waende kuwaomba radhi wananchi katika kata zao.
“Madiwani
wachache walikuja hapa ofisini kuomba radhi kwa Katibu wa CCM Wilaya,
nikawaambia waende kuwaomba radhi wananchi,” alisema.
No comments:
Post a Comment