KAWAIDA wanasiasa ndiyo wamekuwa watu wenye ahadi nyingi sana linapofika suala la maendeleo kwa jamii.
Mara nyingi wamekuwa
wakieleza namna wanavyoweza kuwapatia manufaa wananchi kama
watawachagua, mfano kuhakikisha wanapata maji safi, barabara bora na
vinginevyo.
Wanasiasa wanajulikana kwa
kutotekeleza ahadi zao na wengi wao wamekuwa wakishindwa kuzitekeleza
kwa kutoonekana kabisa baada ya kupewa kura
Halafu, wanaonekana kipindi kama hiki cha uchaguzi kwa kuwa kwa mara nyingine wanataka kupata kura, yaani wachaguliwe tena.
Kabla ya uchaguzi mkuu
ambao unatarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu, huenda wanasiasa wanaweza
kujifunza kupitia Yusuf Said Bakhresa.
Yusuf ambaye ni mmoja wa
wamiliki wa klabu ya Azam FC na Azam Media Group inayomiliki Azam TV,
ameamua kumwaga takribani Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa barabara
jijini Dar es Salaam.
Yusuf ambaye ni wakala wa
kuuza wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa), tayari ameishajenga mitaa miwili na anatarajia kujenga mingine
miwili.
Mitaa yote ipo katika eneo
la Msasani jijini Dar es Salaam, karibu kabisa na yalipokuwa makazi ya
hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Ujenzi wa barabara hizo
umefanywa na wataalamu wa Kichina ambao badala ya kutumia lami kama
ilivyozoeleka, Wachina hao wamejenga kwa kutumia saruji, wakitupia zege
lenye unene mithili ya mikate mitatu iliyobebana!
Ujenzi huo umeanzia kwenye
mtaa unaotokea katika barabara ya Mwai Kibaki, unaingia hadi kwenda
kukutana na mtaa uliopewa jina la Ngome Road.
Mtaa huo ndiyo kuna makazi
ya milionea huyo upande mmoja akiwa amepakana na kampuni maarufu ya
upangishaji nyumba za kisasa ya Blue Mark.
Pamoja na kutengenezwa kwa
ubora wa hali ya juu, milionea huyo amehakikisha mitaa hiyo miwili
imewekewa taa na ing’ara kama New York.
Huenda ndiyo mitaa miwili
pekee inayoingia kutoka barabara kubwa yenye taa nyingi kuliko yoyote
ile jijini Dar es Salaam na Tanzania nzima.
Taa zake pia huenda ndiyo
ghali kuliko zote zilizo katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa
zinatumia mfumo wa solar, hazitegemei umeme wa Tanesco ambao hauna
uhakika, maana unaweza kukatika wakati wowote.
Kama hiyo haitoshi,
imeelezwa bajeti hiyo ya Sh milioni 400 itatumika kuitengeneza mitaa
mingine miwili ya Barakani Road na mwingine mdogo unaounganisha Barakani
Road na Ngome Road.
Ingawa wanaoishi katika
maeneo hayo wengi ni vigogo, imeelezwa Yusuf aliwachangisha kiasi kidogo
cha fedha ambacho huenda hakifiki hata asilimia 20 ya alichotoa.
“Alichofanya ni kama kutaka
kuonyesha ujirani, yaani ajue anashirikiana na watu wanaoishi karibu
yake. Lakini fedha zote anatoa yeye na hatua ya pili ni kujenga tena
mitaa hiyo miwili,” alieleza rafiki wa karibu wa Yusuf ambaye ni mmoja
wa watoto wa bilionea namba moja Tanzania na Afrika Mashariki, Said
Salim Bakhresa.
GETI LA KUINGIA NYUMBANI KWAKE
Juhudi za kumpata Yusuf alizungumzie suala hilo zilikwama baada ya kuelezwa yuko safarini nje ya nchi kikazi.
Lakini taarifa za uhakika
zinaeleza, hana mpango wa kugombea udiwani wala ubunge, badala yake
alifanya hivyo kama mchango wake kwa jamii na kuboresha mazingira ya
eneo hilo analoishi pamoja na majirani zake.
No comments:
Post a Comment