14 March 2015

Matajiri wa Zimbabwe wabugi Yanga

Platinum FC ya Zimbabwe ni klabu inayomilikiwa na matajiri wa madini kwenye Jimbo la Midlands lililopo Wilaya ya Zvishavane.
Timu hiyo itacheza na Yanga kesho Jumapili kwenye mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho na kocha wao, Norman Mapeza, ameyaambia magazeti ya Harare kwamba amebugi kupata video za Yanga.
Hata hivyo, ikabidi aingie kwenye mitandao mbalimbali ili kuijua, akaambulia taarifa za maandishi kwamba haina nguvu ila nzuri kuanzia katikati kwenda mbele lakini nyuma hawako vizuri. Kwa kufukunyua zaidi habari za uhakika zinadai kwamba Wazimbabwe hao walituma shushushu kwenye mechi dhidi ya Simba ili kuisoma Yanga ili kuijua zaidi lakini baada ya kuangalia rekodi za mechi hizo za watani wa jadi wakaambiwa na watu wao kwamba mmebugi kuifutilia Yanga kwenye mechi ya Simba kwa vile mchezo huo haunaga ufundi zaidi ya kukamiana. Wakashika kichwa.
Mbali na hilo, kocha wa Yanga, Hans Pluijm naye amewaambia kwamba wamechemka kwa vile kilichoonekana kwenye mechi dhidi ya Simba wakalala bao 1-0 ni ngumu kutokea kesho Taifa kwa vile amewanoa na kuwapanga upya wachezaji wake na kwamba wanataka kumalizia mchezo huo hapa.
Ikitumia dakika zaidi ya 480 katika mazoezi yao ya siku nne yaliyoanzia Jumanne ikijifua kwa masaa mawili kila siku katika Uwanja wa Taifa ambao ndiyo utakaotumika kwa mchezo huo wa Jumapili, imekuwa na mazoezi makali ya mbinu tayari kwa kuwavaa Platinum ambapo Pluijm na msaidizi wake, Charles Mkwasa, wameisuka safu ya ulinzi wakiwataka mabeki wao kumalizana na washambuliaji hao wa Zimbabwe mbali na eneo la hatari. Mchezo huo utachezeshwa na Djamal Aden Abdi wa Djibouti.

MABEKI NA VIUNGO
Katika mazoezi hayo mabeki wa Yanga wenye nafasi ya kuanza katika mechi hiyo Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir na Kelvin Yondani walikuwa wakipewa mazoezi maalum kwa kuwa makini kuwakaba wapinzani wao mbali na lango.
Mbinu hii ya Pluijm na Mkwasa walizitumia msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakati walipopambana na Al Ahly ya Misri na kusaidia kuwazima washambuliaji wasumbufu wa Waarabu hao ambao hawakufanikiwa kufunga bao lolote katika mechi mbili. Viungo nao wamekuwa wakipewa majukumu ya kutakiwa kupiga pasi za uhakika zinazosogeza timu juu kurahisisha mashambulizi makali, majukumu ambayo wamekuwa wakipewa Said Juma na nahodha msaidizi Haruna Niyonzima.
Katika jukumu hilo Pluijm amekuwa mkali akizuia viungo hao kupiga pasi za nyuma wala zile za pembeni akitaka mpira uende mbele.
Jana Ijumaa ilikuwa ni kazi ya makocha hao kuangalia safu ya ushambuliaji ambayo itaongozwa na Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Amissi Tambwe na Hussein Javu atakayeziba pengo la Danny Mrwanda anayeukosa mchezo huo.

MAJERUHI
Mbali na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Yanga pia itamkosa mshambuliaji wake Mliberia Kpah Sherman aliyepata maumivu ya nyonga pamoja na Mbrazili Andrey Coutinho anayeuguza goti lake huku Mbuyu Twite aliyekosa mazoezi ya juzi na kufanya ya peke yake jana asubuhi anaweza kuwa tayari kufuatia Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani, kuthibitisha kwamba hali yake inaendelea vyema.
Pluijm alisema: “Hii ni timu tofauti kabisa na ile iliyovaana na BDF, wanajua wanachokifanya uwanjani tunatakiwa kuwa makini muda wote wa mchezo, wana kasi watakuja na mbinu zao za kushambulia hata wakiwa ugenini wanashambulia tunatakiwa kuwa makini muda wote wa mchezo.
“Tunahitaji ushindi mkubwa hapa nyumbani, naona timu ipo tayari kwa mchezo hapa tunaingia katika mchezo ambao tunatakiwa tutambue muhimu kwetu ni kufunga mabao mengi, lakini pia tukizuia tusiruhusu bao kwetu.”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname