11 March 2015

Kauli ya Zitto Kabwe baada ya Kushindwa Kesi Aliyoifungua Dhidi ya CHADEMA

Mahakama Kuu ya Tanzania, leo imetupilia mbali shauri lililofunguliwa na Zitto Zubeir Kabwe mwaka jana, akipinga kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kumjadili, akikitaka chombo hicho cha sheria, kukielekeza chama chake, kusubiri kwanza rufaa yake aliyokuwa amekata katika Baraza Kuu.
Mahakama iliyoketi chini ya Jaji Mziray, ilikubaliana na hoja za mawakili wa Chadema, waliosema kuwa ufunguaji wa kesi hiyo ulikiuka baadhi ya vifungu vya sheria na hivyo kumtaka mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Baada ya hukumu hiyo, Zitto Kabwe amesema hakuwa na wito wa mahakamani leo na Jaji aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo amehamishiwa Tabora, hivyo mwanasheria wake ameenda kufuatilia mazingira ya hukumu hio.

"Hatuna taarifa ya Jaji Mpya. Mwanasheria wetu anafuatilia na atatoa statement", ameandika Zitto Kabwe katika ukurasa wake wa twitter.

Wakati Zitto akifungua kesi hiyo Januari mwaka jana, tayari Chadema ilikuwa imewafukuza uanachama Dr. Kitilya Mkumbo na Samson Mwigamba ambao pamoja na Zitto, walituhumiwa kupanga njama za kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya chama hicho.

Zitto alikuwa akitetewa na wakili Albert Msando wakati Chadema iliwakilishwa na Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Mallya.



No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname