BABY ni neno la Kiingereza lenye maana ya mtoto, tena mara nyingi
linatumika kwa mtoto mdogo. Pia lina maana nyingine ya mpenzi. Ni neno
maarufu sana siku hizi; hata wazee kabisa, utasikia wanaitana baby!
Mbali na hilo, yapo maneno mengine kama sweet, dear, honey na mengine
mengi. Maneno yote hayo ya Kiingereza, yana maana zaidi ya moja, lakini
kubwa zaidi ni kumaanisha mpenzi, mpendwa (hutumika katika kuonesha
mapenzi ya dhati kwa mwingine).
Leo nataka kukupa kitu kipya kabisa kichwani mwako. Unahitaji utulivu wa
hali ya juu ili kujifunza hili. Ni maneno mazuri sana, ya kipekee
lakini kwa upande mwingine ni hatari kwa sababu hukaribisha matatizo
ambayo hayakutarajiwa na mtumiaji.
HUTUMIKA WAPI HASA?
“Dear, naomba uniamshe saa 12:00 asubuhi, kesho nina vikao vingi sana
asubuhi,” inaweza kuwa kauli ya mume akimwambia mkewe, ambaye naye
anamjibu: “Sawa sweet, usijali.”
Kwa hakika ndipo sehemu sahihi zaidi kutumika. Ni maneno yenye mshawasha
mkubwa na huonesha penzi la dhati lililopo moyoni mwa mhusika kwenda
kwa mpenzi wake.
Husisimua na kuongeza ladha ya mapenzi ya kweli. Kumuita mpenzi wako kwa
majina ya kimapenzi huongeza zaidi upendo na msisimko wa moyo. Mwenzi
hujiona wa kipekee na mapenzi huzidi kukua.
Kwa maana hiyo basi, ni sahihi zaidi kwa wapenzi kuitana majina
niliyotaja hapo juu na mengine yanayofanana na hayo kwa lugha yoyote
ile, ila iwe inatambulika vizuri na anayetamkiwa.
ATHARI SASA!
Kwa upande mwingine kuna athari za kutumia maneno hayo. Zama hizi,
maneno hayo yanaonekana ya kawaida tu. Mtu yeyote anaweza kumuita yeyote
mpenzi, honey, baby n.k. Hapo ndipo kwenye tatizo lenyewe.
Kwa ujumla wanawake ndiyo wanaongoza zaidi kuitana majina hayo. Wakati
mwingine huenda mbali zaidi na kuwaita hata wanaume majina hayo ya
kimapenzi. Si rahisi kuona athari zake kwa haraka na moja kwa moja,
lakini zipo na wengi zimewasababishia matatizo. Ngoja tuone..
HUPUNGUZA THAMANI
Kama nilivyotangulia kusema awali, maneno
niliyotaja hapo juu husisimua na kuongeza mapenzi. Kwa kuyatumia
vinginevyo, basi kwa kiasi kikubwa huanza kukuathiri na kupunguza
thamani ya neno lenyewe.
Kama unaweza kumwita mfanyakazi mwenzako dear, mtu wa jinsi sawa na wewe
sweet ni wazi hata utakapomuita mpenzi wako au wewe kuitwa na yeye,
halitakuwa na nguvu sana ya mapenzi kwa sababu ni neno ulilolizoea kila
wakati.
HUKARIBISHA USALITI
Wakati mwingine unaweza kujikuta umeingia kwenye usaliti bila kutarajia.
Veronica, mfanyakazi wa saluni moja ya kiume iliyopo Sinza, Dar alitoa
ushuhuda ufuatao:
“Mimi naishi na mchumba wangu, tuna mtoto mmoja mwenye miaka mitatu.
Nafanya kazi saluni. Tangu nimeanza hii kazi, nimejifunza kutumia maneno
matamu ya kumfurahisha mteja na wakati mwingine kumfanya akupe tipu
baada ya kumaliza kazi.
“Kuna kaka mmoja nilizoeana naye sana. Kama kawaida, huwa namkaribisha
kwa kumuita dear au sweet. Wakati nikiendelea kumfanyia scrub,
mazungumzo yetu hutawaliwa na dear, sweet, nikajikuta nimezidi kumzoea.
“Kwa sababu tulibadilishana namba, mara akaanza kuwa na mazoea ya
kunitumia meseji, akija ananipa pesa, anaondoka. Mazoea yakazidi.
Nikajikuta nimemzoea na kuna siku ambayo siwezi kuisahau kabisa.
“Ni siku niliyomsaliti mchumba wangu...mbaya zaidi na huyo jamaa naye
ana mke wake. Niliumia sana, lakini naamini kama nisingekuwa na mazoea
ya kumuita majina ya kimapenzi nadhani nisingeingia mtegoni. Moyo wangu
unauma sana, najuta kumsaliti mpenzi wangu.”
Unaweza usione athari hii moja kwa moja, lakini ndugu zangu chukua jambo
hili leo; wanaume wengi wakiitwa kwa majina ya kimapenzi husisimka sana
– hujiona wenye bahati na mara hushawishika kuingia mapenzi.
Kama mwanamke hatakuwa makini atajikuta ametumbukia. Ya nini yote hayo, wakati unaweza kubadilisha mazoea hayo?
ANGALIA TOFAUTI
Rafiki zangu, kati ya maneno niliyoyataja, kuna ambayo yanakubalika
kutumiwa na wasio na uhusiano lakini wawe na undugu wa damu. Mathalani
baba, mama, kaka, dada, shangazi nk.
Hakuna tatizo kumuita mtu mpendwa, lakini siyo baby, sweet, mpenzi na
mengine yenye maana ya moja kwa moja ya kimapenzi. Umenipata? Akili za
kuambiwa, changanya na zako kisha unazifanyia kazi! Chukua kinachokufaa!
No comments:
Post a Comment