14 March 2015

CV YA MBUNGE VICK KAMATA WA CCM UTATA MTUPU!

Mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Vick Kamata.
 Stori: Mwandishi Wetu
Sifa za kitaaluma (CV) za mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Vick Kamata zilizopo kwenye tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania, zimezua utata kutokana na ‘makengeza’ zilizonazo. 


Habari zilizotua kwenye dawati za Uwazi Mizengwe kutoka kwa chanzo chetu kabla ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, zilieleza kuwa sifa za kitaaluma za mbunge huyo zilizoandikwa kwenye mtandao wa bunge, zilikuwa na dalili ya kupotosha baadhi ya mambo. 

Uwazi Mizengwe liliingia mzigoni na kubaini kuwa CV hiyo ya Mheshimiwa Vick, ilikuwa ikionesha kwamba mheshimiwa huyo ana shahada ya pili (masters degree) katika mambo ya utawala na biashara za kimataifa aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha Southampton Solent cha nchini Uingereza kuanzia mwaka 2008 hadi 2009. 

Pia CV hiyo ilionesha kwamba shahada ya kwanza ya uandishi wa habari (bachelor degree) aliipata kwenye Chuo Kikuu cha St. Augustine jijini Mwanza kuanzia mwaka 2001 hadi 2005. Kabla ya hapo, alikuwa na stashahada (diploma) ya mambo ya kompyuta. 

MKANGANYIKO ULIOPO
Katika CV hiyohiyo, kuna maelezo mengine yanayokinzana na ya awali ambayo yanaeleza kwamba mheshimiwa huyo, hana shahada ya uandishi wa habari bali alisomea kozi fupi ya uandishi wa habari (certificate) katika chuo hicho kilichopo jijini Mwanza kuanzia mwaka 2000 hadi 2001. 

Mkanganyiko mwingine uliopo, ni kwamba kama ni kweli mheshimiwa huyo hakuwa na shahada ya kwanza ya uandishi wa habari, isingewezekana kwenda kuchukua shahada ya pili nchini Uingereza kwani kisheria, ni lazima uwe na shahada ya kwanza ndiyo ukasomee ya pili. 

“Haiwezekani mtu mwenye diploma (shahada) tena ya kawaida tu aende kuchukua masters, ni lazima awe kwanza na digrii au advanced diploma,” alichangia mdau mmoja wakati akichangia mada hiyo mtandaoni. Baada ya kujiridhisha juu ya mkanganyiko huo, Uwazi Mizengwe lilimtafuta mbunge huyo ili atoe ufafanuzi lakini simu yake ya mkononi haikuwa ikipatikana hewani. Juhudi za kumtafuta bado zinaendelea na atakapopatikana, atatoa ufafanuzi kuhusu mkanganyiko huo.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname