Na Father Kidevu Blog
Mkurugenzi wa masuala ya sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Rugonzibwa Mujunangoma na Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Theophil Bwakea wamepandishwa kizimbani wakituhumiwa kupokea Sh milioni 485 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Washitakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka na Wakili Leonard Swai kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Bwakea anadaiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 161,700,000 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya VIP Engineering and Marketing ambaye alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya IPTL James Rugemalira.
Anadaiwa Februari 12, 2014 katika jengo la benki ya Mkombozi Ilala Dar es salaam, alipokea fedha kupitia akaunti namba 00410102643901 akiwa kama mjumbe aliyeandaa sera kuruhusu sekta binafsi kuzalisha na kuiuzia umeme Tanesco.
Mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru, Mujunangoma anadaiwa kupokea Sh milioni 323,400,000, baada ya kushughulikia masuala ya kampuni ya IPTL kama mfilisi jambo ambalo linahusiana na kazi yake.
Anadaiwa kupokea fedha hizo Februari 5, 2014, kupitia akaunti namba 00120102602001 kutoka kwa Rugemalira ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, Kesi hizo zitatajwa Januari 29 mwaka huu kwaajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini Januri 16 Mujunangoma atafika mahakamani kukamilisha taratibu za dhamana.
No comments:
Post a Comment