Na Makongoro Oging’/Uwazi
MWANAMKE mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Doreen
John Mlemba, mwenyeji wa Same mkoani Kilimanjaro, mwishoni mwa mwaka
uliopita alikamatwa kwa kuhusishwa na shehena ya madawa ya kulevya aina
ya Heroin, yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5.
Madawa hayo yalikutwa kwenye nyumba moja iliyopo eneo la Ununio,
Tegeta jijini Dar es Salaam, ambayo ni mali ya Mbunge wa CCM (Jina
linahifadhiwa) wa jimbo moja la mikoa ya Kanda ya Ziwa, Uwazi
limefukunyua.
Taarifa toka vyanzo mbalimbali makini, zinasema majirani wa nyumba
hiyo walikuwa na mashaka na kinachofanyika ndani ya nyumba hiyo, kwani
licha ya ukubwa na kukamilika kwa ujenzi wake, lakini haikuwa ikikaliwa
na mtu na mara chache, watu walionekana wakiingia na kutoka bila
kujulikana walichokuwa wakikifanya.
Kutokana na hali hiyo ya wasiwasi, wasamaria wema walitoa taarifa kwa
Jeshi la Polisi ambalo liliifanyia kazi habari hiyo na kufika kwenye
nyumba hiyo na kujaribu kugonga lakini bila mafanikio yoyote.
“Baada ya kugonga, ndipo polisi hao walipoamua kuvunja mlango na
kufanya upekuzi katika sehemu zote ndani ya nyumba hiyo, ambapo
walifanikiwa kulikuta sanduku ambalo baada ya kufunguliwa, zikagundulika
kilo 35 za madawa ya kulevya aina ya Heroin,” kilisema chanzo chetu
kilichoshuhudia zoezi hilo.
Kamanda wa Kikosi Cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya
nchini, SACP Godfrey Nzowa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa baada ya kukamata shehena hiyo, vijana wake walijikuta
katika wakati mgumu wa kumjua mmiliki wa nyumba hiyo.
Baada ya kutafuta nyaraka mbalimbali, hatimaye waligundua kuwa nyumba
hiyo inamilikiwa na mbunge huyo wa zamani ambaye alitafutwa na kuhojiwa
kwa saa kadhaa, ambapo alikiri kuimiliki, lakini akidai kwa muda huo,
alikuwa ameipangisha kwa watu aliowataja, bila kujua shughuli iliyokuwa
ikifanyika ndani yake.
Inadaiwa kuwa baada ya kupata ushirikiano huo kutoka kwa mbunge huyo,
askari waliingia mtaani kuwasaka wapangaji hao, ambapo Septemba 15,
mwaka jana, saa saba mchana, walifanikiwa kumkamata Doreen, akiwa
shambani kwake, eneo la Ruaha Mbuyuni mkoani Iringa alikokuwa akivuna
vitunguu, bamia na bilinganya.
“Tulifanya uchunguzi na tayari watu watano wameshakamatwa akiwemo
Doreen, nyumba hiyo waliifanya kama ghala la kuhifadhia madawa na mtu
mmoja bado tunaendelea kumsaka, baadhi ya waliokamatwa tulikuwa
tukiwasaka kwa muda mrefu,” alisema Kamanda Nzowa.
Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuwaomba waendelee hivyo
na kwamba donge nono litatolewa kwa watakaofanya hivyo huku majina yao
yakihifadhiwa.Gazeti hili lilimfikia Mbunge huyo mmiliki wa nyumba kwa
njia ya simu, lakini alikataa kulizungumzia suala hilo, akidai liko
chini ya polisi.
“Naomba suala hili umuulize Kamanda Nzowa, mimi siwezi kulizungumzia
kwa vile lipo chini ya uchunguzi wao, pamoja na kwamba nawatambua hao
wapangaji lakini siwezi kusema lolote,” alisema.
No comments:
Post a Comment