Kuna baadhi ya mastaa wanaojua kuyatumia majina yao, kwani licha ya kuwa mwigizaji na mtangazaji wa redio, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ hafanyi kazi hizo pekee bali ana kampuni inayobeba tenda mbalimbali katika sekta za umma na binafsi.
Akizungumza na Gazeti la Mwananchi,Monalisa alisema kuwa anapenda kufanya mambo yake chinichini ndiyo maana walio wengi hawajui anayoyafanya katika jamii.
Hata hivyo, alibainisha kuwa anafanya kazi katika kampuni zaidi ya tatu kila siku na anatenga muda wa kuwa na familia yake, hiyo ndiyo sababu pekee inayomwepusha kufanya mambo yasiyofaa.
“Mambo yangu huwa nafanya kimyakimya siyo lazima upige makelele watu wakujue taratibu watu watakujua tu lazima, nina kampuni yangu mwenyewe Sherry Company Limited na sasa hivi ni meneja wa Manday Entertainment. Hii ni kampuni mpya wa filamu na burudani, tuna studio za audio na video tunataka pia kuanza na usambazaji wa filamu,” alisema.
Monalisa alisema kupitia kampuni yake ametengeneza filamu nyingi. “Binti Nusa 1,2,3 nilitengeneza kupitia filamu yangu, mara nyingi nafanya tenda mbalimbali ingawa sijajitangaza sana,” alisema na kuongeza: “Inatengeneza vitu mbalimbali katika sekta za umma na binafsi. Ukiachana na kampuni hizi mbili, nafanya kazi ya utangazaji na pia tamthilia na filamu, niko bize kwa kweli.”
Kuhusu tasnia ya filamu, Monalisa alisema hakuna elimu ambayo haijatolewa kuhusu maisha ya kupendana kwa wanasanii.
“Tumeshahubiri umoja, watu tupendane kwangu mimi naona hapa kila mtu afanye kwa nafasi yake ili tufikie mahala tunapopataka,” alisema Monalisa na kuongeza: “Kuwa wasambazaji ni lazima kuwa makini na masilahi ya msanii mmoja mmoja.
“Wasambazaji nao wanataka kulifanya soko letu liwe gumu, nilikuwa kinyume na wao, namshukuru Mungu wizara ilishatoa tamko kuhusu bei ya filamu iliyopangwa na kampuni ya kusambaza filamu ya Steps kwamba isitishwe.
Filamu hazitauzwa tena Sh1,500, natumaini wataendelea na msimamo wao huohuo na watakuja na bei elekezi ili sote tufahamu kitakachokuwa kikiendelea
No comments:
Post a Comment