Harakati
za kuwania urais ndani ya CCM zimeingia katika hatua mpya baada ya
mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru kuibuka na kudai kuwa wote
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha
kutaka kuingia Ikulu.Kauli ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja
kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda
ikitajwa kuwa suala la maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa
hao ambao wanaongezeka kila kukicha.Akizungumza Dar es Salaam jana,
Kingunge alisema: “Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi
ya pesa na nikwambie ukweli, hao wanaotangaza urais wote wanatumia
pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”Kwa miezi kadhaa
sasa, baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakitajwa kufanya harakati
kichinichini na wengine kushiriki shughuli za wazi zinazoashiria kuwa
wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu. Hadi sasa makada wanne tayari wameweka
wazi nia yao hiyo.Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli
zinazowashutumu makada wengine wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya
fedha katika kushawishi uungwaji mkono.Hata hivyo, kauli za wanasiasa
hao zimedaiwa kuwa ni fitina za kisiasa kwa kuwa wagombea wote wanatoa
fedha, bali wanazidiana viwango tu.
Mbali na Makamba na Membe, wanaCCM
wengine waliotangaza au kutajwa kuwania urais ni Mbunge wa Nzega, Dk
Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani,
Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kauli ya Kingunge aliyoitoa kupitia
Televisheni ya ITV, imekuja wakati wanasiasa sita miongoni mwa hao
wanaotajwa wakikaribia kumaliza miezi 12 ya uangalizi kutokana na onyo
kali dhidi yao lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM Februari 18, mwaka jana
baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya “kuanza kampeni mapema na
kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya chama na ya jamii.”
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Lowassa, Sumaye, Njeleja, Makamba, Wasira na Membe.
Akisisitiza hoja yake hiyo bila kutaja
majina, Kingunge alisema makada hao wamekuwa wakitumia fedha nyingi
kujitangaza na kutengeneza ushawishi wa kukubalika kwa wananchi jambo
ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi.
Kingunge alisema mwanasiasa yeyote anayehitaji uongozi hapaswi kutumia fedha kushawishi wananchi wamchague.
“Kiukweli tukiangalia wote
wanaojitangaza hakuna msafi hata mmoja... hatuwezi kuchagua rais kama
vile tunachagua wachezaji wa mpira, haiwezekani. Tunataka kupata mgombea
wa urais ambaye atakuwa na uwezo wa kushughulikia kwa vitendo kero na
umaskini wa Watanzania,” alisema Kingunge.
Alisema badala ya viongozi kutumia muda
mrefu kumtafuta mchawi, ni vyema wakatazama namna ya kushughulikia suala
la maadili kwa sababu kati yao hakuna msafi hata mmoja.
Kuhusu watu wengi kujitokeza kutaka
urais, Kingunge alisema: “Kujitokeza kugombea urais siyo dhambi, ingawa
watu wanashangaa kidogo kwamba kila mtu anaibuka tu anataka urais,
kidogo inaleta kasoro lakini siyo kitu, wanataka kutumia haki zao.”
Mkongwe huyo wa siasa alisema wananchi
ndiyo wanaowajua wagombea hao na sifa zao, hivyo wakumbuke kuwa
anayechaguliwa ni rais na siyo mchezaji wa mpira.
“Mnachagua rais ambaye ataweza
kuwaunganisha kama Taifa, ataweza kuwatumikia kwa vitendo siyo
kujitumikia wenyewe, pia ataweza kutatua matatizo yanayowakabili
wananchi,” alisema.
Aliongeza kwamba kwa kuwa tatizo kubwa la wananchi ni umaskini, wananchi watazame mtu atakayeweza kuondoa hali hiyo.
Akizungumzia kuhusu namna viongozi wa
Afrika wanavyoyatumia madaraka yao, Kingunge alisema wamepiga hatua
kubwa lakini bado haitoshi kwa kuwa wanakosa namna chanya ya kutumia
madaraka ambayo Afrika iliyapigania kutoka kwa wakoloni.
“Tumeupigania uhuru ili tuendeshe nchi
yetu wenyewe, turudishe ile thamani yetu kama watu. Sasa madaraka
tumepata, lakini tunayatumiaje?” alihoji.
Kuhusu Mapinduzi
Kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotimiza miaka 51 jana, Kingunge alisema yamekuwa na faida kubwa kwa Wazanzibari.
Alisema Mapinduzi hayo ndiyo msingi wa
Muungano ambao umeleta mafanikio makubwa kwa pande zote licha ya
changamoto zinazoibuliwa.
“Haikuwa
na budi kufanya mapinduzi kwa kuunda kamati ya wapiganaji 14 ambao
waliongoza kazi hiyo baada ya kuona mfumo uliokuwa unatumiwa na Serikali
ya Sultan unawakandamiza wazawa. Baada ya mapinduzi hayo kufanikiwa,
ardhi iliyokuwa inamilikiwa na kundi moja la Waarabu ikagawanywa kwa
kila Mzanzibari akapata ekari tatu, pamoja na hali hiyo elimu
ilitangazwa kutolewa bure.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment