07 January 2015

Aliyeiokoa Yanga jana na Kuipeleka Robo fainali Alala Rumande......Ushirikina Watawala




YANGA SC walishinda 1-0 dhidi ya Shaba katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la Mapinduzi, lakini walikosa mabao mengi ya wazi wakiwa kwenye nafasi nzuri kabisa.

Mrisho Ngassa, Danny Mrwanda, Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Andrey Coutinho wote walikosa mabao ya wazi kipindi cha kwanza wakiwa kwenye nafasi nzuri kabisa za kufunga.

Kipindi cha pili, hali iliendelea kuwa hivyo na hata baada ya kocha Hans van der Pluijm kuwaingiza Amisi Tambwe, Kpah Sherman na Salum Telela dakika ya 59 kwenda kuchukua nafasi za Ngassa, Mrwanda na Said Juma ‘Kizota’ hali iliendelea kuwa ya kutengeneza nafasi za kushindwa kufunga.

Shabiki mmoja wa kike na mwanachama maarufu wa Yanga SC, Tuni aliyekuwa ameketi jukwaa kuu, eti akapandisha shetani likawa linasema kipa wa Shaba kuna vitu ameweka langoni vinamlinda asifungwe.

Akawaagiza mashabiki wanaume wakavitoe na wakati mchezo ukiendelea dakika ya 81, akaibuka shabiki na mwanachama mmoja maarufu wa Yanga SC, Carlos na kwenda kuchukua glavu za akiba za kipa wa Shaba, Bakari Shaweji.
Glavu za akiba za kipa wa Shaba, Bakari Shaweji zilizua balaa jana Uwanja wa Amaan
Carlos baada ya kuzichukua glavu hizo anaondoka nazo
Anaondoka nazo huku akifungua
Dakika tano baadaye, Andrey Coutinho akaifungia Yanga SC bao pekee la ushindi
Carlos akiwa kwenye gari la Polisi tayari kupelekwe rumande. Hata hivyo aliachiwa baada ya saa kadhaa.

Carlos alikimbia na glavu hizo na kwenda kuzitupa nje ya Uwanja wa Amaan, bahati mbaya kwake akakamatwa na Polisi waliokuwapo uwanjani hapo ambao pia walifungua geti kwenda kuzichukua glavu zile.

Glavu zikakabidhiwa kwa viongozi wa Shaba, wakati Carlos alipelekwa kituo cha Polisi, ambako hakulala, alitolewa baada ya saa kadhaa.

Wakati Carlos akiwa njiani kupelekwa kituoni, Yanga SC wakapata bao lililofungwa na Andrey Coutinho dakika ya 86 na mashabiki wa Yanga SC wakaanza kuimba; “Mungu, Mungu, Mungu”, wakimaanisha kweli kulikuwa kuna uchawi langoni mwa Shaba.

Imani za ushirikina zimekuwa sehemu ya soka ya Waafrika na inaaminika hata wachezaji wakubwa wanaocheza Ulaya, hususan kutoka Magharibi mwa Afrika wanaendekeza imani hizo.

Lakini ukweli ni kwamba vitu hivyo kwenye mpira havina nafasi, bali ni imani potovu inayoendekezwa, wakati mwingine kutokana na uelewa mdogo.

Kama ni kweli kuna uchawi, basi bao la Yanga SC jana sifa ziwaendee Tuni na Carlos na sio mfungaji Coutinho, au Juma Abdul aliyetia krosi! Ipo haja ya kubadilika

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname