By EDO KUMWEMB (email the author)
Na amefunga kazi kwa habari iliyotokea
majuzi kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaomlipa mshahara Haruna Moshi
Boban pale Friends Rangers.
MWAKA 2014 ulikuwa mwaka wa Diamond Platinumz.
Mwanamuziki aliye bize kujitangaza kimataifa. Mwanamuziki anayeshinda tuzo nyingi anazoshiriki.
Na amefunga kazi kwa habari iliyotokea
majuzi kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaomlipa mshahara Haruna Moshi
Boban pale Friends Rangers.
Huku katika soka ulikuwa mwaka wa
masikhara kama kawaida. Kuna upuuzi mwingi umeendelea kama kawaida. Ni
kama upuuzi wa mwaka juzi, mwaka huu, na ni kama itakavyoendelea kuwa
mwakani.
Wakati Diamond akiwa bize kujitangaza
kimataifa, hakuna mchezaji yeyote wa Tanzania aliyetoka kwenda
kujitangaza nje. Sanasana tulimpokea Shomari Kapombe aliyekuwa Ufaransa
akijiandaa kucheza soka la kulipwa.
Tulichoambulia ni picha yake tu akiwa na
nyota wa zamani wa Ufaransa, William Gallas. Ni mwaka ambao taifa
lilijaribu kupata wachezaji imara wa timu ya taifa kupitia kwa wachezaji
wasiocheza daraja lolote. Uongo huu ulioitwa Maboresho ulichekesha
sana. Lakini sasa wajanja wamebadili kauli na wameita wachezaji wa Ligi
Kuu na kuwaita maboresho.
Ulikuwa ni mwaka wa vioja kama kawaida. Lakini pia ulifanana na mwaka jana hasa lilipokuja katika suala la mechi ya mtani Jembe.
Yanga walimfukuza kocha wao Marcio
Maximo kwa staili ile ile waliyotumia kumfukuza Ernie Brandts.
Walimfukuza kwa mechi ya bonanza dhidi ya watani wao wa jadi, Simba.
Mwaka huu pia tulishuhudia mchezaji
kutoka Taifa la Brazil, Emerson akisajiliwa na timu kubwa nchini Yanga,
lakini alicheza kwa dakika 45 tu na kutimuliwa. Haikutimia wiki kamili
tangu aliposaini mkataba klabuni hapo. Ulikuwa mwaka wa vioja sana huu.
Acha upite.
Ni mwaka ambao tulishuhudia pia mfungaji
bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Amiss Tambwe akiachwa bure na klabu
yake, tena bila ya matatizo yoyote ya kinidhamu klabuni kwake. Acha huu
mwaka upite tu.
Ni mwaka ambao ndoto za Taifa Stars
kucheza michuano ya Afcon 2015 zilikoma rasmi katika ardhi ya Msumbiji.
Ina maana kama kuna uwezekano wowote wa kucheza Afcon, basi itakuwa
2017. Lakini kwa mwenendo wa soka la nchi yetu nina hofu kuwa kama Mungu
akitupa pumzi tunaweza kukutana Desemba 2016 kujadili jinsi tulivyokosa
kushiriki michuano ya 2017.
Na hukuhuku katika michuano ya
kimataifa, Yanga ilimsikiliza kocha wake, Maximo na kujitoa katika
michuano ya Kombe la Kagame. Walitoa sababu zisizoridhisha kupitia kwa
Maximo lakini niliamini kuwa ile ingekuwa michuano ambayo ingekiweka
kikosi chao fiti.
Matokeo yake walimfukuza kocha huyohuyo
kwa madai ya kwamba kikosi chao kilikuwa hakichezi vizuri mechi zake.
Wangechezaje vizuri wakati walikimbia maandalizi ya msingi
Rwanda?.Emmanuel Okwi namchukulia kama Mtanzania mwenzetu kwa sababu
alikuja nchini akiwa mdogo. Aliziwakilisha tabia zetu kwa kufanya mambo
yasiyoeleweka kidogo. Mwaka huu alifanikiwa kucheza timu mbili.
Ni kama ilivyokuwa kwa mwaka jana alivyocheza mechi mbili. Inaonekana kuwa kitu cha kawaida kwake.
Na inadaiwa kuwa katika siku ya uhamisho ya dirisha dogo la alikuwa anataka kwenda zake Azam.
Huu ulikuwa mwaka mwingine wa vurugu
katika soka na wala hauleti matumaini ya kutufikisha popote. Na ndiyo
maana haishangazi kuwa hata katika viwango vya Fifa, Taifa Stars ilikuwa
inapiga hatua tano mbele kisha inapiga hatua saba nyuma.
Ni kama mwanamuziki maarufu wa kizazi
kipya, Profesa J alivyoimba katika Wimbo wa Mtazamo alioshirikishwa na
Afande Sele. Na ndiyo maana haikushangaza kuifunga Benin mabao 4-0 kisha
wiki chache zilizofuata tukafungwa mabao 3-0 na Burundi. Hatujawahi
kuwa katika mwendelezo wa ubora. Mwaka 2015 unakuja. Hakuna kitu
tunachoweza kufanya katika michezo kama wadau wote hawawezi kubadili
fikra zao na kuufanya mchezo wa soka kuwa biashara kama zilivyo biashara
nyinginezo.
Tukiamini katika hilo tutaondoa uhuni
katika michezo. Tutatengeneza sera na katiba imara kwa ajili ya kuinua
michezo. Heshima itarudi kama ilivyo katika sekta nyingine.
Tusipofanya hivyo, mchezo wa soka utaendelea kuonekana wa kihuni daima milele katika ardhi ya Tanzania.
Taifa litaendelea kuzipoteza ajira
ambazo hatuzioni. Tutaendelea kupotea mabilioni ya kodi kutoka kwa
wanamichezo na klabu zetu. Kwa sasa hatuwezi kuziona kodi hizo kwa
sababu watu wanajitengenezea kiholela tu jezi za Yanga na Simba pale
Chang’ombe.
CREDIT:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment