Nyota wa kimataifa wa Simba, Mrundi, Amissi Tambwe.
NYOTA wa kimataifa wa Simba, Mrundi, Amissi Tambwe, anatarajia kuondoka nchini leo na kwenda kwao Burundi kwa ajili ya mapumziko lakini amepanga kuondoka na mizigo yake yote.
Tambwe ambaye hivi sasa hana raha katika kikosi cha Simba kutokana na
kuwepo kwa tetesi za kutaka kuachwa, amefikia hatua hiyo akihofia
kukutwa na balaa kama lililomkuta Mrundi mwenzake aliyewahi kuitumikia
klabu hiyo msimu uliopita, Gilbert Kaze.
Kaze ambaye alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kati katika kikosi cha
Simba, alifungashiwa virago bila ya yeye kujua wakati alipokuwa Burundi
kwa mapumziko hali inayomfanya naye ahofie kukutwa na balaa hilo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Tambwe alisema kuwa, mpaka sasa
hajui hatma yake katika kikosi cha timu hiyo, hivyo anaenda kwao Burundi
akiwa amejiandaa kwa jambo lolote litakalotokea hapo baadaye, ndiyo
maana anatarajia kuondoka na mabegi yake yote.
Alisema pamoja na kupewa moyo na viongozi wa timu hiyo, bado ana
wasiwasi kwa sababu hajafanya mambo makubwa msimu huu kama ilivyokuwa
ule uliopita.“Jambo jingine linalonipa wasiwasi ni kuhusiana na mkataba
wangu, kwani nimebakiza miezi michache tu, hiyo nayo inaweza kuwa
sababu lakini ngoja tuone itakavyokuwa.
“Natarajia kuondoka Jumatano (leo), kwenda nyumbani kwa mapumziko
lakini itabidi niondoke nikiwa nimejiandaa kwa kila kitu na kama
ikitokea nikaachwa basi nisihangaike tena,” alisema Tambwe ambaye msimu
uliopita ailiibuka mfungaji bora wa ligi kuu baada ya kufunga mabao 19.
No comments:
Post a Comment