Katika
zama hizi za utandawazi na muingiliano baina ya tamaduni zetu za asili
na tamaduni za kimagharibi, imekuwa ni kawaida kwa vijana wa rika
tofauti na jinsia zote kutoga ulimi, mdomo, kitovu ama kivimbe cha nyusi
kwa sababu tofauti tofauti sana. Hivyo basi, ni muhimu sana kufahama
ukweli kuhusu faida ama hasara za kutoga ulimi ama mdomo kabla
hujatekeleza azma yako ya kutoga viungo hivi vya mwili.
Kutoga Ulimi ama Mdomo kunaweza kukusababishia madhara yasiyotarajiwa.
Matokeo mazuri zaidi
ya kutoga ulimi ama mdomo ni kutokutokea kwa kidonda ama kivimbe, wakati
matokeo mabaya kutokea kwa baadhi ya watu ni pamoja na kuvunjika kwa
meno/jino, kuvuja kiasi kikubwa cha damu, ama maambukuzi ya bakteria
kwenye kidonda. Kutoga ulimi hujumuisha kutumika kwa sindano
inayopenyezwa katikati ulimi ili kupitisha na kuhifadhi kipini, ama
ndoana ama hereni ya urembo. Kazi hii ya kutoga ulimi mara nyingi ganzi
huwa haitumiki. Baada ya kutoga, kuvimba kwa ulimi na maumivu ya muda
hutokea.
Madhara ya kutoga Ulimi
Kuvuja damu kiasi
kidogo hutarajiwa, kuna hatari ya mishipa ya damu kuharibiwa wakati wa
kutoga ulimi, hali inayoweza kusababisha kuvuja damu kwa kiasi kikubwa
kuliko ilivyotarajiwa.
Ingawa kuvimba kwa
ulimi kunatarajiwa baada ya kitendo cha kutoga ulimi, wakati mwingine
ulimi huvimba kwa kiasi cha kuziba kwa njia ya hewa. Kuziba kwa njia ya
hewa kunaweza kusababisha kifo.
Ikiwa
fundi wako wa kutoga ulimi hana uzoefu wa kutosha kufanya kazi hiyo,
anaweza kuharibu mishipa ya fahamu ya ulimi hivyo kuharibu uwezo wa
ulimi kuhisi/kutambua hisia za joto,baridi ama ladha ya chakula na
vinyaji, vile vile kuathiri mienendo ya viungo vya eneo la kinywa na
uso. Kwani nyuma ya ulimi kuna mishipa ya fahamu,mishipa hii ikiharibiwa
ulimi utapooza hivyo kusababisha ganzi la kudumu, kuathirika kwa uwezo
kuongea na kushindwa kutambua ladha za chakula/vinywaji
Vilevile
kutoga ulimi kunakuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi kwenye ulimi
hasa ikiwa hutaweza kutunza hali ya usafi wa kinywa na meno kila
wakati, hivyo kusababisha wadudu jamii ya bakteria kupenya na kuingia
ndani ya ulimi na kusababisha maambuzi kwenye ulimi.
Hali ya kutoga ulimi
inapodumu kwa muda mrefu, inaweza kusababisha nyufa kwenye meno, ama
kuvunjika kwa nyuso za jino/meno kwa sababu ya msuguano wa muda mrefu
kati ya jino/meno na hereni/kipini ama ndoana ya chuma/plastiki
iliyohifadhiwa kwenye ulimi kwa muda mrefu. Nyufa hizi kwenye meno, kwa
kawaida husababisha maumivu makali ya jino/meno.
Hivyo basi meno haya
yenye nyufa yanaweza kutibiwa kwa kuvalishwa kofia “ dental crown”. Si
kawaida kupata magonjwa ya fizi ama kuta za ndani za shavu ikiwa umetoga
ulimi na unatunza afya ya kinywa na meno vizuri.
Kutoga Mdomo
Kutoga mdomo ni pale
pete ya urembo inapovalishwa ama kuhifadhiwa ndani ya mdomo. Majeraha ya
kutoga mdomo hupona haraka zaidi, hata hivyo unapaswa kutunza kidonda
cha jeraha hili kwa umakini mkubwa wakati wa kupona. Vyakula, vinywaji
na moshi wa sigara vinapofikia kidonda hiki, vinaongeza hatari ya kupata
maambukizi kwenye kidonda.
Kishikizo vishikizo
vya pete hii ya urembo kinaweza kusababisha vidonda kwenye fizi ama
kuharibu jino. Kwa baadhi ya watu, tiba ya kupandikiza fizi hutumika
kurejesha fizi zilizoathirika. Kama ilivyo kwa kutoga ulimi, kutoga
mdomo pia kunaweza kuathiri mshipa wa fahamu hivyo kuathiri mienendo ya
misuli ya kwenye eneo la kinywa na mdomo.
Je, una mpango wa kutoga Ulimi ama Mdomo?
Ikiwa unapanga kutoga
viungo hivi vya mwili, unashauriwa ufanye mambo yafuatayo yatakayo
kuwezesha kupata huduma ambayo haita athiri afya yako:
Hakikisha ngariba
mtoga ulimi ama mdomo sio tu ana uzoefu wa kutosha kwenye kazi
anayofanya, bali pia anazingatia usafi kufanya kazi zake.
Nenda hospitali kupata
ushauri tiba mara tu unapoona ama maumivu ni makali sana, kuvimba kwa
ulimi ama damu zinavuja kwa muda mrefu (zaidi ya dakika 30) ama ikiwa
jeraha linapata maambukizi ya bakteria.
Unapokuwa na hereni,
pete ama ndoana ya urembo kwenye ulimi ama mdomoni, unashauriwa kumwona
daktari wa kinywa na meno kila baada ya miezi sita (6). Daktari wa meno
atafanya kazi ya kuhakiki ikiwa kidude kilichovalishwa kina madhara
kwenye meno ama fizi, hivyo kudhibiti athari zinazoweza kutokea kwa
kutoga ulimi ama mdomo.
Wana michezo
wanashauriwa kutovaa hereni, pete ama ndoana ya urembo iliyopo kwenye
ulimi ama mdomoni wanapokuwa mchezoni, kwani vyombo hivi vya urembo
vinaweza kunasa kwenye ngozi bila kutarajia hivyo kusababisha madhara
yasiyotarajiwa.
No comments:
Post a Comment