21 September 2014

MATOKEO YA MECHI ZOTE ZA LEO LIGI KUU TANZANIA BARA HAYA HAPA


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara Azam fc wameanza ligi kwa kishindo baada ya kuitandika Polisi Morogoro 3-1 katika mchezo wa ufunguzi wa msimu wa 2014/2015 uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City kama ilivyokuwa msimu uliopita, wameanza ligi kwa kutoa suluhu pacha ya bila kufungana (0-0) katika dimba lao la Sokoine jijini Mbeya dhidi ya JKT Ruvu.
Afisa habari wa Mbeya City, Dismas Ten amesema mechi ilikuwa ngumu kwa timu zote na matokeo hayo ni ya kawaida katika mpira, lakini benchi la ufundi litakaa chini kufanya marekebisho.
Katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, bao pekee la Ramadhani Pela limetosha kuipa ushindi wa 1-0 Mgambo JKT dhidi ya Kagera Sugar iliyosafiri kutoka Kaitaba.
Kikosi cha Mbeya City fc
Katibu mkuu wa klabu hiyo, Antony Mgaya amesema kuwa wamefurahishwa na ushindi huo licha ya kupata upinzani wa kutosha, hivyo wanajipanga kwa mechi ijayo ili kuendeleza wimbi la ushindi.
Katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Tanzania Prisons ‘Wajelajela’ wamewatandika wenyeji wa uwanja huo, Ruvu Shootings mabao 2-0.

Huko Kambarage mkoani Shinyanga, Stand United wakiwa nyumbani wametandikwa mabao 4-1 na Ndanda fc kutoka mkoani Mtwara.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Ndanda fc walikuwa mbele kwa mabao 3-1 na kipindi cha pili wakaongeza bao la nne.
Katibu mkuu wa Ndanda fc, Seleman Kachele amesema walitawala mchezo huo na ni mwanzo mzuri kwao.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi moja kupigwa ili kukamilisha mzunguko wa kwanza ambapo wekundu wa Msimbazi Simba watakuwa nyumbani uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuivaa Coastal Union.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname