MAKABURI YA KINONDONI
Jana baada ya miili ya marehemu kuagwa Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni Dar msafara wa kuipeleka kupumzishwa kwenye makaburi ulianza huku wombolezaji, wakiwemo mastaa walisikika wakisema kwamba Makaburi ya Kinondoni yanazidi kumeza mastaa katika siku za hivi karibuni kwani ukimweka kando Recho, mastaa wengine kama Adam Kuambiana, Steven Kanumba, John Maganga, Zuhura Maftah ‘Melisa’ na wengine wamezikwa hapo.
KUAGA, MAZISHI
Mastaa kibao walizimia walipojumuika kuiandaa miili ya Recho na mwanaye kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kisha kuipeleka nyumbani kwa mjomba wake Evans Haule, Sinza-Palestina, Dar ambapo familia iliaga kabla ya kwenda Leaders Club na baadaye kwenye Makaburi ya Kinondoni.
JENEZA LA RECHO LASHINDIKANA KUINGIZWA NDANI
Hata hivyo, jeneza la Recho lilishindikana kuingia ndani ya nyumba ya mjomba’ake kwa vile mwili ulivimba hivyo liliandaliwa jeneza kubwa ambalo halikuweza kupita mlangoni na kuishia nje tofauti na taratibu.
NJE YA MAZISHI
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Recho, katika kipindi chote cha ujauzito marehemu alikuwa akijificha kama shosti yake, Jennifer Kyaka ‘Odama’ naye alipokuwa na mimba ili kukwepa macho ya ‘wabaya’.
AHAMA NYUMBA
Habari za uhakika kutoka kwenye chanzo chetu zinasema kuwa katika kipindi hicho, marehemu alikuwa akitokewa na mauzauza kibao hali iliyomlazimisha ahame nyumbani kwake Sinza, Dar na kwenda kuishi kwa Saguda, Kinondoni jijini Dar.
Chanzo kilisema uamuzi wa marehemu kuhamia kwa Saguda haukusaidia kuondokana na ‘madongoloji’ hayo kwani bado mauzauza yaliendelea kwa kadiri ujauzito ulivyozidi kukua.
Habari zilieleza kuwa miezi miwili kabla ya kukutwa na mauti, Recho aliamka asubuhi moja na kujikuta amechanjwa chale sehemu mbalimbali za mwili hasa kwenye mapaja kitendo kilichomshangaza sana.
MAUZAUZA LAIVU
Katika kuthibitisha hilo, marehemu alitundika picha yake kwenye Mtandao wa Instagram zilizoonesha chale hizo na kusema:
“Ya leo kali! Yaani naamka sasa hivi nakutana na hivi vitu (chale) mwilini mwangu.
“Wakati mpaka jana nalala majira ya saa nane usiku nilikuwa nipo sawa kabisa. Bado najiuliza hizi chale zimetoka wapi? Da! Eee Mungu naomba kama kuna ubaya wowote pigana na mimi (dhidi ya adui).”
Ilisemekana kwamba siku chache baadaye mambo yalimzidia akaandika tena kwenye ukurasa wake huo: “Watashindana lakini hawatashinda.”
“Kuna wakati mambo yalikuwa magumu ikabidi aende Songea (Ruvuma) kufanya tambiko kwa bibi yake, aliporudi mambo yalitulia kidogo. Nakumbuka hata ninyi (Global) mliandika habari hiyo,” kilisema chanzo na kuongeza:
“Kuna kipindi Recho alilalamika kwenye vyombo vya habari kwamba, kuna wasanii ambao hakuwataja majina alidai wana vijiba vya roho dhidi yake hasa mafanikio aliyokuwa akiyapata kwa kufanya kazi kwa bidii.
“Walipoona upande huo wamekwama akalalamika kuwa hawapendi uhusiano wake na Saguda ambaye ni cameraman wa muvi za Bongo. Ndiyo maana hata alipopata ujauzito hakutaka uonekane kwani alijua wabaya wake wasingefurahishwa.
USHIRIKINA BONGO MOVIE
“Huenda kweli kuna mkono wa mtu kwenye kifo cha Recho na mwanaye kwa maana Bongo Movie kwa ushirikina nao hawajambo,” kilisema chanzo.
Uchunguzi wa Ijumaa ulibaini kwamba watu wengi walikuwa hawaamini kama Recho ameaga dunia hadi walipoona jeneza hivyo kila mtu kusema lake.
SAGUDA ANASEMAJE?
Baada ya kunyetishiwa ishu hiyo, gazeti hili lilizungumza na mumewe Saguda ambaye alisimulia mambo mazito huku akilia kukosa mke na mtoto kwa mpigo.
MAMBO MAZITO
Saguda alisema mambo mengine ni mazito hawezi kuyazungumza hadharani hivyo yatabaki kuwa moyoni mwake milele ila ukweli ni kwamba yeye na marehemu wamepitia katika kipindi kigumu wakati wa ujauzito huo.
KUMBE ALITAKA KUZAA MAPEMA KABLA HAJAFA
Kumbukumbu kutoka kwenye makabrasha zetu zinaonesha kuwa, Septemba 12, mwaka jana, Recho aliongea na paparazi wetu na kusema kuwa, kutokana na vifo mfululizo vya wasanii ameamua kuzaa mapema kabla hajafa ili akifa aache urithi.
Marehemu aliyasema hayo akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa msanii wa filamu, Zuhura Maftah ‘Malisa’ ambapo alibainisha kuwa maisha ya sasa ni mafupi tofauti na zamani hivyo bora azae haraka.
“Maisha yetu siyo marefu kama yalivyokuwa ya wazee wetu, angalia wasanii wengi waliotangulia bado ni wadogo na wengine hata hawajaacha watoto, inauma sana. Mungu akipenda nitapata ujauzito muda wowote ili nizae maana hali ni tete,” alisema Recho kwenye mahojiano hayo.
BONGO MUVI KUNA NINI?
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya mastaa wa Bongo Movie walionesha kusikitishwa na msiba huo wakisema ni mzito haujawahi kutokea kwenye tasnia hiyo kwa mama na mtoto kuondoka pamoja.
Recho alifariki dunia Mei 26, mwaka huu baada ya kujifungua na kusumbuliwa na presha, kisukari na kifafa cha mimba.
Baadhi ya filamu alizocheza marehemu huyo ni pamoja na Danger Zone, Family Disaster, Long Hope (haijatoka), Mke Mwema, Gentlemen, Cindy, Life to Life, Loren, Men’s Day Out, Unpredictable na Figo.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina
No comments:
Post a Comment