Stori: Jelard Lucas
WANAWAKE na maendeleo, tufanye kazi, tusonge mbele, yelele…yelele… Hii
sehemu ya mashairi ya wimbo wa staa wa muziki wa kizazi kipya na Mbunge
wa Viti Maalum (UVCCM), Geita, Vicky Kamata anayetajwa kuwa na utajiri
balaa.
UWAZI LINA KILA KITU
Vicky amepata mafanikio
makubwa ambayo kila mwanamke Tanzania angependa kuyapata. Gazeti hili
lilimchimba kwa kina na kupata utajiri wote alionao kwa sasa.
KABLA YA SIASA, KABLA YA BONGO FLEVA
Kabla ya
siasa aliishi maisha ya dhiki ambayo hakutegemea kama angekuja kupata
mafanikio makubwa. Ni miongoni mwa Watanzania waliozaliwa katika familia
duni.
Katika kutafuta ‘kutoka’ kimaisha, Vicky amewahi kuwa
mwanamuziki wa Bongo Fleva na kutunga nyimbo mbalimbali, wimbo wa
Wanawake na Maendeleo ndiyo uliomtambulisha zaidi katika jamii.
“Nimezaliwa kwenye familia duni, nimeishi maisha ya dhiki sana, mbali
na muziki, nimewahi kuwa mwalimu wa shule ya msingi kule Moshi
(Kilimanjaro) katika harakati za kusaka maisha, baadaye nilikwenda
Morogoro.
“Kila kitu kinabadilika kama ukimwamini Mungu,” alisema Vicky mwenye
watoto wawili, Revocatus na Glory (jina la baba halikutajwa).
MAFANIKIO YAANZA
Mwaka 2006, Vicky alifanikiwa kuajiriwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwa ni afisa uhusiano.
Mwaka 2010, Vicky alifanikiwa kuwa mbunge wa viti maalum akiuwakilisha Mkoa wa Geita.
MJENGO WA GHOROFA MBILI
Akiwa mbunge, Mheshimiwa
Vicky ameingia kwenye orodha ya wanawake mabilionea nchini kwa
kuangusha mjengo wa kifahari wa ghorofa mbili Sinza jijini Dar es Salaam
wenye thamani ya shilingi bilioni moja na milioni mia nne.
Ndani ya ghorofa hilo kuna bwawa la kisasa la kuogelea ‘swimming pool’ ambalo linatumiwa na familia yake.
MAGARI YAKE SASA
Kama walivyo matajiri wengine,
mheshimiwa huyo anamiliki magari manne ya kifahari, yote yakiwa na
thamani ya shilingi milioni 261.
Ana Toyota Voxy- Noah ambalo alilitoa sokoni kwa shilingi milioni 16.
Kamata pia anamiliki BMW X5 likiwa na thamani ya shilingi milioni 130.
Mara nyingi anapokwenda bungeni, Vicky hutembelea gari linalomudu
mikiki ya barabarani, Toyota Land Cruiser ‘VX’ ambalo lina thamani ya
shilingi milioni 90.
Pia mwanamama huyo ana gari aina ya Toyota Altezza alilolinunua kwa shilingi milioni 25.
ANAMILIKI MGODI WA DHAHABU
Wakati hayo yakiwa
wazi, chanzo makini kilidai kuwa, mheshimiwa huyo amenunua mgodi wa
dhahabu Geita, jambo ambalo ni sehemu kubwa ya mafanikio yake.
“Vicky amenunua mgodi wa dhahabu Geita, mimi ni mtu wangu wa karibu,
hapendi kusema mafanikio yake wala watu wajue lakini ukweli ndiyo huo.
Eneo ni kubwa, muda si mrefu uchimbaji utaanza,” kilisema chanzo cha
habari kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
ANA SHAMBA LA EKARI 157
Utajiri wa mheshimiwa
huyo unaendelea kuanikwa kuwa, ni pamoja na shamba lenye ekari 150,
Kisarawe, Mkoa wa Pwani. Pia ana shamba la miti Kibamba, Dar lenye ekari
7.
NI MFUGAJI
Mbali na mambo mengine, Vicky ni mfugaji kama ilivyo asili ya Wasukuma. Anafuga ndege aina ya kanga, kuku wa kisasa na mbuzi.
ANASOMESHA WATOTO WASIOJIWEZA
Katika mambo
ambayo huenda yanachangia kuchota baraka, mheshimiwa Vicky anawalipia
ada ya sekondari watoto yatima, walemavu na wasiojiweza kimaisha, idadi
yao ikifikia 75.
KIPATO CHAKE KIKOJE?
Dodoso zinaonesha kwamba,
kwa kazi ya uheshimiwa, kwa mwezi anaingiza shilingi milioni 15
ukijumlisha posho zote za ubunge, ujumbe wa kamati ya bunge na mshahara.
AMFUNIKA ANNE MAKINDA
Uchunguzi uliofanywa na
gazeti hili umebaini kuwa, jumba la kifahari la Vicky Kamata
linalifunika lile la bosi wake ambaye ni spika wa bunge, mheshimiwa Anne
Makinda. Yeye nyumba yake ipo Kijitonyama.
ULINZI NYUMBANI KWAKE USIPIME
Uwazi lilipata
bahati ya kufika nyumbani kwa Vicky na kukumbana na ulinzi wa mitambo
ya kisasa ya kuzuia wezi na majambazi kwa saa 24.
Ili mgeni aingie ndani ya geti huhojiwa na walinzi kwa dakika zisizopungua kumi.
WABAYA WAKE WAMUUNDIA ZENGWE LA FREEMASON
Huwezi
kupendwa na kila mtu, hii ni baada ya mwandishi wa gazeti hili kuamua
kupiga kambi kwa muda wa siku mbili jirani na nyumba ya mheshimiwa huyo
ambapo baadhi ya watu waliohojiwa kuhusu ukwasi wa mbunge huyo mwanamke
walisema huenda ni memba wa Freemason.
“Mafanikio ya mbunge huyu bwana ni makubwa mno, tunasikia watu
wakisema huenda ni Freemason. Lakini ndivyo tulivyo Watanzania, mtu
akifanikiwa kidogo wanasema ni Freemason, ninavyomfahamu huyu dada
amepiga hatua, sijawahi kumsikia na mambo ya Freemason,” alisema jirani
mmoja na kuungwa mkono na wenzake.
MSIKILIZE VICKY
Katika mahojiano maalum na Uwazi kuhusu utajiri wake, Vicky alisema:
“Mafanikio yote yametokana na juhudi zangu za kujituma katika kufanya
kazi, namwamini Mungu siku zote. Hakuna dhambi mbaya hapa duniani kama
kukata tamaa.
“Tukifanya kazi kwa kujituma na kumwamini Mungu hakuna Mtanzania maskini.
“Kila mtu ana uwezo wa kubadilisha mfumo wa maisha akiamua, umaskini wa
watu si chaguo la Mungu, kila jambo litokealo kwa mwanadamu lina maana
kubwa kwa Mungu.”
KAULI YA UWAZI
Wanawake nchini waige mfano wa
Vicky kwa kukamata fursa mbalimbali na wanapofanikiwa wawasaidie
wengine, kama kusomesha yatima na wasiojiweza
No comments:
Post a Comment