07 February 2014
MGOMVI WA MKE WA ZUMA KUREJESHWA TANZANIA
Dar es Salaam. Mtanzania Stephen Ongolo anayekabiliwa na madai ya kutishia kutoa siri za mke wa Rais Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli (MaNtuli), huenda akarudishwa nchini na kuzuiwa kuitembelea Afrika Kusini milele.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Tawi la Uchunguzi wa Kesi, katika Jimbo la Kwa Zulu-Natal, Brigedia Clifford Marion, wakati kesi ya Ongolo ilipokuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Camperdown, jijini Durban.
Ilielezwa kuwa, Ongolo si raia wa Afrika Kusini na kwamba alirudi nchini humo Januari 19 mwaka huu baada ya kurejea kutoka katika mizunguko yake katika nchi kadhaa za Afrika zikiwamo, Tanzania, Malawi, Msumbiji na Ethiopia.
Ilielezwa kuwa visa yake inamalizika Februari 18 mwaka huu.
“Atarudi nchini mwake Tanzania na hatarudi tena Afrika Kusini,” alisema Marion.
Chanzo chetu cha habari kilichohudhuria kesi hiyo, kilisema Brigedia Marion alihojiwa kuhusu taarifa za mashtaka dhidi ya Mtanzania huyo ambapo alitoa ushahidi kuwa Ongolo amekuwa akituma ujumbe mfupi kwenye simu ya MaNtuli, akimtishia kuwa atatoa siri kuhusu uhalali wa mtoto wake (MaNtuli).
Inadaiwa kuwa Ongolo katika ujumbe wake alidai kuwa mtoto mmoja wa MaNtuli si wa Rais Zuma.
Kabla ya kukamatwa, Ongolo alikwenda katika vyombo vya habari kadhaa vya nchini humo na kudai kuwa, anafahamu siri nzito kati ya MaNtuli na Phinda Thomo, aliyekuwa mlinzi wa MaNtuli.
Thomo, alikutwa amejiua mwaka 2009 bafuni kwake, lakini Ongolo anadai kuwa Thomo hakuuawa na badala yake, kifo chake kilipangwa kutokana na uhusiano wa siri kati yake na MaNtuli.
Mashtaka ya kutishiwa kuvujisha siri zake, yalitolewa na MaNtuli ambaye alidai kuwa Ongolo amekuwa akimlazimisha kumkutanisha kibiashara na Rais Zuma.
Brigedia Marion alitoa ushuhuda mahakamani na kuiomba mahakama kukataa kutoa dhamana kwa Ongolo ambaye alikamatwa mwishoni mwa Januari mwaka huu.
“Tofauti na inavyoandikwa kwenye magazeti, Ongolo alikamatwa baada ya kufika ofisini kwangu akija kulalamika kuwa kuna kesi ya wizi na uvamizi kwenye nyumba ya dada yake ambayo inasimamiwa vibaya,” alisema Brigedia huyo.
Alisema, Ongolo alipofika ofisini hapo alijitambulisha kama Stephen Ongolo lakini baadaye alibainika kama Stephen John Masunga ndipo Marion akalikumbuka jina kwani MaNtuli alikuwa ameshawasilisha mashtaka hayo polisi.
“Kukamatwa kwake ilikuwa ni bahati. Nilipoona jina ni lilelile, nikaangalia namba ya simu niliyopewa na MaNtuli na kuanza kuipiga na simu ya Ongolo ikaita na hapohapo nikamweka chini ya ulinzi,” alisema Marion.
Ilidaiwa kuwa baada ya Ongolo kukamatwa, simu yake na hati ya kusafiria vilichukuliwa na alipotakiwa kumpigia simu wakili wake, hakufanya hivyo na badala yake alimpigia simu mwandishi wa habari wa gazeti la Sunday Independent, Nathi Olifant.
Marion alisema, alikusanya ujumbe mfupi kutoka kwenye simu za Ongolo na MaNtuli na kubaini kuwa wawili hao waliwahi kukutana mwaka 2010.
Source: Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment