KANISA la Romani Katoliki limeishukia tasnia ya
filamu Bongo (Bongo Movies) kutokana na matendo maovu yanayofanywa na
wasanii katika sinema zao hususan suala zima la kuheshimu imani za watu.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Thadeus Ruwa’ichi
amewaonya wasanii kuwa maigizo yao yasilenge kuchafua umma ama kikundi
chochote kwani wanaweza kuleta mgawanyiko katika taifa.
Akizungumzia msimamo wa kanisa kuhusiana na filamu ya Sister Maria ya
mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ ambayo kanisa hilo liliipinga kutokana
na madai ya kukiuka maadili, Askofu Ruwa’ichi alisema hawakubalini nayo
kwani mavazi ya masista yaliyotumiwa na wasanii hao, yalitumika vibaya
hivyo hawakubaliani nayo.
Akifafanua zaidi kuhusiana na filamu hiyo, kiongozi huyo wa kiroho
alisema alisononeshwa na kazi hiyo ambayo ilikuwa na dosari za kuingilia
imani ya kikatoliki kwani mavazi ya kanisa yalitumika kuvaliwa bila
staha.
“Ile filamu ilikuwa na lengo la kuhatarisha jamii, kamwe isiendelee
kwani ni hatari kwa watu ama mtu binafsi anayechukizwa na tatizo hilo,
“Maigizo yanayofanywa yanaweza kuwa na lengo la kutumbuiza, lakini
kutumbuiza kokote kule, hakupaswi kuhatarisha lengo la kulea ama
kuvuruga mambo ya watu fulani, kulinda heshima ya watu binafsi ama
taasisi, nidhamu inahitajika kwa kila jambo wanalolifanya,” alisema.
Askofu huyo alisema taifa lina mambo mengi na linajivunia kwa amani
ya muda mrefu, hivyo waigizaji hao wanapoigiza maigizo ambayo yanagusa
imani au jamii ya watu wengine linaweza kuwa tatizo kubwa huko mbele.
“Hakuna haja ya maigizo kuchafua watu wengine, heshima kwa wote ni
jambo jema ambalo linaweza kuongeza upendo kwa kila jambo ufanyalo kwa
jamii nyingine.
“Wakifanya kazi zao kwa ufasaha bado taifa litawaheshimu, hakuna mtu ama kundi ambao wangependelea kutokee vurugu eti kwa sababu ya maigizo ya mtu fulani, haiwezi kuungwa mkono,” alisema askofu huyo
“Wakifanya kazi zao kwa ufasaha bado taifa litawaheshimu, hakuna mtu ama kundi ambao wangependelea kutokee vurugu eti kwa sababu ya maigizo ya mtu fulani, haiwezi kuungwa mkono,” alisema askofu huyo
No comments:
Post a Comment