GRACE
Simon mwenye miaka 14 anateseka na uzito wa kupindukia wa kilo 111
(kama gunia moja la mahindi na viroba vitatu) hali iliyomsababishia
akatishwe masomo na walimu katika Shule ya Msingi Amani, Ukonga, Ilala
jijini Dar es Salaam alikokuwa anasoma.
Grace ambaye mwaka huu angekuwa darasa la saba lakini aliachishwa
shule mwaka 2010 akiwa darasa la nne na walimu wakimtaka akatibiwe.
MAMA MZAZI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi kuhusu
mkasa mzima wa mtoto Grace, mama yake mzazi, Ashura Bakari alisema binti
yake alimzaa salama mwaka 2000 lakini ilipofikia mwaka 2002 akiwa na
miaka miwili alianza kuvimba tumbo hali ambayo hakujua chanzo chake.
ATENGWA NA WANAFUNZI
Mama huyo akizungumza kwa masikitiko alisema kuwa, Grace alipofika
darasa la nne, akiwa na umri wa miaka kumi baadhi ya wanafunzi wenzake
walianza kumnyanyapaa kutokana na unene ambao ulikuwa ukiongezeka siku
hadi siku.
“Walikuwa wakimtania sana mwanangu hadi kukosa amani. Hali hiyo
iliwafanya walimu kumsimamisha masomo ili atibiwe. Hadi sasa sijapata
msaada wa kupona kwake,” alisema mama huyo huku machozi yakimtoka.
HOSPITALI ZIMESHINDWA?
Aidha, mama Grace aliongeza kuwa amekwishahangaika katika hospitali
mbalimbali za jijini Dar es Salaam, ikiwemo Muhimbili bila mafanikio.
“Muhimbili waliniambia ili mwanangu aweze kufanyiwa vipimo pamoja na
matibabu gharama zake ni shilingi laki nane (800,000) ambazo nimezikosa
na hakuna mtu wa kunisaidia,” alisema.
NDUGU NAO
Alisema mbali na kutafuta tiba
hospitalini, amekuwa akipita huku na huko kuomba msaada wa fedha kutoka
kwa ndugu na jamaa lakini hakuna aliyemsadia.
KWA NINI BABA MZAZI ASIMSAIDIE?
Katika hali ya
kushangaza, mama huyo alisema ili kupata fedha hizo anahangaika peke
yake kwa sababu baba mzazi wa Grace, Simon alikataa kutoa msaada wowote.
“Baba yake yupo hai, alikuwa anatoa msaada kipindi cha mwanzo lakini
miaka kama mitano imepita hakuna msaada anaonipa. Ni kweli hatuishi
pamoja lakini mtoto tulizaa wote,” alisema kwa masikitiko makubwa mama
huyo.
WALICHOKIONA MADAKTARI
Akizungumzia kiini cha
tatizo, mama huyo alisema: “Kwa mujibu wa madaktari mwanangu
anasumbuliwa na moyo kujaa mafuta mengi, kwa hiyo homoni zake zimekosa
uwiano na ini pia lina sumu nyingi.”
GRACE AWALILIA WATANZANIA
Akizungumza na
mwandishi wetu, mtoto huyo anayetamani kuendelea kusoma aliwaomba
Watanzania wamsaidie fedha ili aweze kutibiwa na kurejea darasani.
“Niliachishwa shule ili nitibiwe, nikipona nirejee shuleni, lakini
hadi sasa sijapata nafuu, na ninajua ni kutokana na kutopata matibabu
sahihi,” alisema Grace huku akilia.
UONGOZI WA SHULE
Mmoja wa walimu waandamizi wa
Shule ya Msingi Amani alipokuwa akisoma mwanafunzi huyo (hakuwa tayari
kutaja jina lake), alikiri kumtambua mwanafunzi huyo na kusema
aliachishwa shule kwa hofu ya uongozi wa shule.
“Hatukumwachisha shule kwa nia mbaya, lakini lengo letu lilikuwa
akatibiwe kisha arudi shuleni lakini matibabu anayopata hajaweza kupona
na hali aliyokuwa nayo inazidi kuongezeka siku hadi siku,” alisema
mwalimu huyo.
Akaongeza: “Mwaka huu Grace ilikuwa awe darasa la saba, lakini hata
kutembea ni tatizo hali ambayo tuliona kuwa unene ule si afya bali ni
ugonjwa.”
MSAADA UNAAOHITAJIKA
Kwa yeyote aliyeguswa na
tatizo la Grace ambaye anasaka shilingi laki nane tu ili atibiwe,
anaweza kuwasiliana na mama yake mzazi kwa simu: 0719 465445, ASHURA
BAKARI
No comments:
Post a Comment