Vinywaji
baridi vyenye lengo la kuongeza nguvu vinadaiwa kuwa hatari kwa afya ya
watumiaji baada ya kubaini baadhi ya kemikali husababisha madhara
mwilini.
Watumiaji wa vinywaji hivyo wamehadharishwa ikielekezwa utafiti
mbalimbali uliofanyika kwa miaka 10, inaonesha athari za matumizi ya
vinywaji hivyo.
Katika mitandao ya Yahoo na The Dailymeal, iliwekwa orodha ya
vinywaji vinavyodaiwa kuwa na kemikali hatari, miongoni mwake ikiwamo
Red Bull na Monster, vinavyotumika kwa wingi nchini. Vingine vilivyo
katika orodha hiyo ni VPX Redline, DynaPep na Rockstar Cocaine.
Akizungumza na mwandishi jana, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula
na Dawa nchini (TFDA), Gaudensia Simwanza alitaja kinywaji cha Red Bull
ambacho kimetajwa kuwa miongoni mwa vinywaji hatari kuwa ni salama kwa
matumizi ya binadamu.
Hata hivyo, alisema vinywaji vingi vyenye kemikali vikiwamo vya aina
hiyo vinaweza kuwa na madhara endapo vitanywewa kwa kiwango kikubwa.
Alisema vinywaji vingi vina athari ikiwa vitanywewa bila mpangilio.
Aliongeza kuwa vipo vinywaji ambavyo lazima vifikie viwango vya mataifa
ndipo viruhusiwe kuingia sokoni.
Simwanza alikuwa akizungumza na mwandishi aliyemhoji kuhusu hatari
ya vinywaji hivyo na iwapo zipo hatua zilichukuliwa za kuangalia athari
zake kwa watumiaji.
Alisema endapo upo utafiti uliofanywa kuona si salama, ni vema watafiti hao wakashirikisha mamlaka hiyo ili kubaini ukweli.
"TFDA imesajili Red Bull baada ya kujiridhisha kuwa ni salama kwa
matumizi ya binadamu, endapo wametafiti na kuona si salama,
watushirikishe na sisi katika utafiti waliofanya ili tufanyie kazi na
kuchukua hatua," alisema.
Akielezea suala zima la usalama, alisema wakati mwingine huenda soko
likawa limevamiwa na watu wasio waaminifu ambao wanazalisha vinywaji
hivyo vikiwa na madhara kwa watumiaji.
Alisema Mamlaka huwa inafanya utafiti wa bidhaa katika masoko mara
kwa mara, ikiwa ni pamoja na ukaguzi kwa lengo la kujiridhisha ubora na
usalama wake. “Ikitokea kuna taarifa zenye shaka kuhusu bidhaa huwa
tunafuatilia na kuzifanyia kazi," alisema.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya kwenye mtandao, imepokewa kwa hisia
tofauti wakiwamo wanaotetea vinywaji hivyo na kuchukulia kuwa propaganda
za kibiashara.
Kulingana na utafiti, inadaiwa vinywaji hivyo vya kusisimua mwili,
zimo kemikali zinazosababisha magonjwa ya moyo na kukosesha usingizi.
Aidha, inaelezwa kuwa vinywaji hivyo vyenye mchanganyiko wa kemikali
za L-phenylalanine, inositol na citicoline si salama hasa vinaponywewa
kwa wingi.
Kwa upande wa Red Bull, inatajwa kujaa kemikali za kusisimua mwili na
nyingine kusababisha meno kuoza kutokana na wingi wa sukari iliyomo.
Kinywaji cha Monster kimeshawahi kuchunguzwa na Mamlaka ya Chakula na
Dawa ya Marekani (FDA) kutokana na kuonekana kuleta madhara makubwa
kwa watumiaji. Inadaiwa kusababisha matatizo ya usingizi.
Kinywaji kingine kilichoko kwenye orodha ni VPX Redline ambayo
imetengenezwa kupunguza hali ya kutetemeka, inadaiwa kuleta mwako katika
mafuta. Inatakiwa inywewe kidogo mhusika akiwa amekula.
Aidha, DynaPep ina kemikali aina ya methylhexanamine; kisisimua mwili
ambacho wengine wanasema kinapoteza mwelekeo wa mtu na wakati mwingine
huongeza kasi ya mapigo ya moyo.
Rockstar ina gramu 62 za sukari na 280 za nishati. Full-Throttle,
inatajwa kwamba unywaji wake wa kupitiliza unaweza kuleta maumivu ya
tumbo, upotevu wa kumbukumbu na ongezeko la mapigo ya moyo.
Cocaine inadaiwa kuwa na kemikali inayosisimua mara tatu zaidi ya Red Bull. Pia husababisha hatari ya magonjwa ya moyo.
No comments:
Post a Comment