Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza Eng. Evarist Ndikilo kufuatia vifo vya watu wawili vilivyotokea
tarehe 15 Desemba, 2013 katika Kitongoji cha Kanyama Kata ya Kisesa
Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza.
Rais ametuma salamu hizo kwa Mkuu wa Mkoa kufuatia vifo vya BW. Clement
Mabina na Tenery Malimi vilivyotokea baada vurugu zilizosababishwa na
mabishano ya ardhi. Rais amemuomba Mkuu wa Mkoa kuwatahadharisha
wananchi kutokuchukua sheria mikononi mwao na pia kuwa waangalifu na
matumizi ya silaha za moto.
“Nimesikitishwa na kufadhaishwa sana na taarifa za vifo vya wananchi hao
wawili (2) vilivyosababishwa na mgogoro wa Ardhi ambao ungeweza kupata
suluhu kwa njia za amani. Ni vema wananchi kuwa na subira na kuwa
waangalifu katika kutatua migogoro yao”. Rais amesema na kuongeza kuwa “
ni vema subira na busara zikawa ndio muongozo wa kutatua migogoro yetu
katika jamii badala ya hasira”.
Aidha, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa amfikishie salamu zake za
dhati kwa familia na ndugu wa Marehemu Mabina pamoja na Wazazi na ndugu
wa Marehemu Tenery Malimi, ambao walifariki kutokana na vurugu hizo.
“Amewaomba familia zote mbili ziwe na subira wakati huu mgumu kwa
kuondokewa na wapendwa wao na kuviacha vyombo vya dola kuchukua hatua
kwa kufuata taratibu zilizopo”. Kwa ndugu Mabina, Chama cha Mapinduzi
kimepoteza mmoja wa viongozi wake mahiri na wa kutumainiwa. Aidha, kwa
marehemu Tenery taifa limepoteza mmoja wa vijana wake wanaochipukia
ambae angejaaliwa kuishi angeweza kutoa mchango muhimu kwa maendeleo ya
jamii na nchi yetu.
Mabina amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Diwani na Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Magu mwaka 2000 – 2005, Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi Mkoa wa Mwanza, mwaka 2007 – 2012.
Rais ameziombea nyoyo za marehemu wote Mungu azilaze mahali pema peponi Amen.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Desemba,2013
No comments:
Post a Comment