MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto
amesema atatembea na kuhutubia mikutano ya hadhara ya wananchi nchi
nzima bila kuogopa wala kukatazwa na mtu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara
kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini hapa jana, Zitto alisema hazuiwi
na maneno ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa aliyotoa
mkoani Tabora kwamba mikutano anayofanya nje ya jimbo lake ni kinyume
cha Katiba.
Alisema akiwa mwanachama hai wa Chadema
na mbunge, ana haki ya kutembea na kuhutubia mikutano ya hadhara mahali
popote na kudharau maneno yaliyotolewa na Dk Slaa kwamba ni kama kelele
za chura hazimzuii tembo kunywa maji.
Zitto aliongeza kuwa Dk Slaa ametoa maneno ya kutaka watu “waniambie niache kuhutubia mikutano hiyo kwa sababu inaweza kusababisha mimi kufukuzwa chama,” jambo ambalo kwake yeye amebainisha kama wanatoa hukumu. “Wamenipa
siku 14 kutoa utetezi wangu, kwanini wasinifukuze chama, siku hizo
zimeshakwisha lakini hawataki kukutana kutoa uamuzi, badala yake kila
kiongozi anatembea mikoani kivyake na kutoa maneno ya kunihukumu,” alisema Mbunge huyo.
Aidha, alituhumu uongozi wa Chadema
kumzushia uongo kwamba anahamasisha wajumbe wa Baraza Kuu kuomba mkutano
kujadili suala la zima wakati wanaoomba hayo ni viongozi ambao wako
madarakani chini ya viongozi wa Chadema, makao makuu na si chini yake.
Alisema mapokezi anayopata katika
majimbo ya Mkoa wa Kigoma yanawatia kiwewe viongozi wa chama hicho na
ndiyo maana wanatoa maneno ya kutaka kumwonesha kwa wananchi kuwa
kiongozi asiyefaa.
“Wananchi wanajua utendaji wangu,
wanajua kazi kubwa niliyofanya kwao ndiyo maana kila ninakokwenda
wanakuja kwa wingi kusikiliza nawaeleza nini, waniache niwaeleze
wananchi kinachoendelea wasiwazuie hawana uwezo huo,” alisema Zitto.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo
alisema anatafuta ushauri wa kisheria aweze kusajili jina jipya la Mwami
Ruyagwa alilotawazwa na wazee wa Wilaya ya Kasulu alipokuwa kwenye
ziara ya mikutano ya hadhara wilayani humo.
Source: Habari Leo
No comments:
Post a Comment